Tuesday, February 21, 2017
MPAKA MPYA MATUMIZI BENDERA,WIMBO ZANZIBAR VYATAKIWA KUTUMIKA IPASAVYO
Do you like this story?
BARAZA la Wawakilishi Zanzibar
(BLW) limepitisha sheria mpya ya Bendera ya Zanzibar, Nembo ya Serikali
na Wimbo wa Taifa ambapo wasanii na wafanyabiashara wamepigwa marufuku
kuvitumia kwa matangazo ya biashara.
Muswada wa sheria hiyo uliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed.
Akifunga mjadala wa muswada huo, Waziri
Aboud alisema serikali imeamua kuweka utaratibu mzuri wa kisheria wa
kutumia Bendera ya Zanzibar, Nembo ya Serikali na Wimbo wa Taifa wa
Zanzibar.
Alisema wanamichezo na wasanii
wataruhusiwa kutumia Bendera ya Zanzibar wanapokua katika mashindano,
yakiwemo ya kimataifa katika kuendeleza na kuimarisha utaifa.
“Nembo ya Serikali ni alama nyeti (hivyo
ni) marufuku kutumika kwa matangazo,” alisema Waziri Aboud. Marufuku
hiyo inahusu pia Bendera ya Zanzibar.
Alisema baada ya sheria hiyo kupitishwa,
kutatungwa kanuni ambazo zitaweka utaratibu mzuri wa matumizi yake,
ambapo pamoja na mengine shule za umma na binafsi zitatakiwa wanafunzi
wake kuimba wimbo wa taifa kila siku.
Waziri Aboud alisema Bendera ya Zanzibar
itakuwa ikipandishwa saa 12 asubuhi na kuteremshwa saa 12 jioni na
wakati ikiteremshwa wananchi katika maeneo husika watatakiwa kuheshimu,
ikiwemo kusimama kwa muda.
Alisema sheria hiyo itasadia kujenga
uzalendo na umoja wa kitaifa na viwango vya ubora vya kitambaa cha
Bendera ya Zanzibar kitazingatiwa kama walivyopendekeza wajumbe wa
Baraza hilo.
Hata hivyo, wakichangia mswaada huo
baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipinga marufuku ya kutumia
bendera na wimbo kwa matangazo ya biashara.
Wajumbe waliopinga ni Hassan Hafidh
Khamis (Welezo), Simai Mohamed Said (Tunguu), Suleiman Sarahan
(Chakechake), na Ali Suleiman Ali (Kijitoupele).
Walisema bendera kutumika katika
matangazo ya biashara na kazi za sanaa kunasadia kuitangaza nchi pamoja
na kuongeza uzalendo na umoja wa kitaifa kwa wananchi wake.
Simai alisema zipo nchi nyingi duniani
zinatumia bendera za nchi zao katika kuitangaza nchi kupitia bidhaa
wanazozalisha, kazi za sanaa na michezo.
“Mheshimiwa Spika, kama wamasai
wanatengeneza vitu vya mapambo na kutumia rangi za Bendera ya Taifa,
wanatangaza nchi na kuonyesha uzalendo wao; kwanini Zanzibar
wafanyabiashara na wasanii wazuiwe?” Alihoji Sarahan.
Sarahan alisema wananchi wanapoipenda
nchi yao hufikia hata kujifunga bendera kiunoni, kichwani na kucheza
ngoma, na wengine hata kufikia kutandika na kulala juu ya bendera.
Mwakilishi Jaku Hashimu Ayoub alitaka kufahamu kama kuwapo kwa nyimbo mbili za taifa si kuleta mkanganyiko nchini.
“Mheshimiwa Spika mie elimu yangu ndogo
ndiyo maana sijateuliwa kuwa waziri wala Naibu Waziri, naomba
kuelimishwa inakuwaje kuwapo wimbo wa Taifa na wa Zanzibar?” Alihoji
Jaku.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MPAKA MPYA MATUMIZI BENDERA,WIMBO ZANZIBAR VYATAKIWA KUTUMIKA IPASAVYO”
Post a Comment