Friday, February 24, 2017

MWENYEKITI CUF MBARONI KWA TUHUMA ZA UBADHIRIFU WA FEDHA


Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi  ameagiza Jeshi la Polisi kumkamata Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kijitonyama kwa tiketi
ya Chama cha Wananchi (CUF), Philip Komanya kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za ushuru wa taka, pamoja na za mchango wa ukarabati wa mfereji wa mtaa  Sh. 55,000 zilizo changwa na wananchi wa mtaa huo.
Hapi alitoa agizo hilo baada ya kupata taarifa za malalamiko ya mkandarasi wa taka wa mtaa huo, ya kutolipwa pesa zake za ukandarasi za mwezi Novemba, 2016 kiasi cha Sh. milioni 4.5.
“Kila mwenyekiti afanye kazi zake kwa mujibu wa sheria, pesa zinazokusanywa ziwekwe katika akaunti za benki pia tumieni mashine za EFD na mtoe risiti. Mimi sitamuonea mtu na siwezi kunyamaza, kila mtu atabeba msalaba wake,” amesema Hapi.
Licha ya malalamiko hayo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kijitonyama, Elizabeth Minga alidai kuwa mwenyekiti huyo alikuwa anafanya ubadhirifu wa fedha za ushuru wa taka kwa kutumia akaunti mbili, ambazo moja ilikuwa ya wajumbe wakati nyingine ikidaiwa kuwa ya kwake binafsi ambayo alikuwa anaingiza asilimia kubwa ya makusanyo ya pesa za taka kinyume cha sheria.
Kabla ya Komanya kukamatwa, Hapi alimtaka kutoa maelezo juu ya fedha za ushuru wa taka zilipo au matumizi yake na sababu ya mkandarasi huyo kutolipwa fedha zake ilhali wananchi walitoa.
Lakini alishindwa kueleza pesa hizo mahali zilipo au taarifa sahihi za matumizi yake badala yake alidai kuwa ana vielelezo vinavyoonyesha mkandarasi  kuchukua sehemu ya malipo yake mil 2.4 huku akishindwa kufafanua zilizosalia.
“Mimi na mtendaji wa mtaa tulikuwa na mgogoro, na alificha kitabu cha hundi. Ila  Baadae tulilimpa mkandarasi milioni 2.4 kwa ajili ya shughuli za  uzalishaji na vielelezo vipo nilimpelekea mtendaji wa kata,” alisema Komanya.
Lakini Afisa Mtendaji wa Kata ya Kijitonyama alikana madai hayo na kudai kuwa hakukabidhiwa taarifa au vielelezo vinavyoonyesha kuwa mkandarasi alilipwa sehemu ya fedha anazo dai huku akimtuhumu Komanya kuwa alikataa kuzipeleka pesa za ushuru katika akaunti ya benki licha ya mkaguzi wa ndani wa Kata hiyo kumuagiza kuiweka katika akaunti sahihi ya mtaa.

0 Responses to “MWENYEKITI CUF MBARONI KWA TUHUMA ZA UBADHIRIFU WA FEDHA”

Post a Comment

More to Read