Friday, February 24, 2017

SERIKALI YAAHIDI KUENDELEZA VITA YA KUZUIA VITENDO VYA UKEKETAJI KWA WANAWAKE


Serikali ya Tanzania imesema itaendeleza vita kupinga vitendo vya ukeketaji ambavyo wamekuwa wakifanyiwa wanawake na wasichana katika maeneo mbalimbali nchini kwani hicho ni kinyume na sheria ya Tanzania na ni ukiukwaji wa haki za wanawake.
Hayo yamesemwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Ackson Tulia katika semina ya siku moja iliyoandaliwa na Balozi wa Italia nchini kwa lengo la kubadilishana uelewa kuhusu ukeketaji na jinsi umevyoathiri jamii ya Tanzania.
 
Naibu Spika wa Bunge, Dk. Ackson Tulia.
Dk. Tulia alisema Serikali inatambua kuwepo kwa sehemu ambazo zimekuwa zikifanya vitendo hivyo na itaendelea juhudi zake za kuzuia vitendo hivyo na kumaliza kabisa na itandelea kushirikiana na mataifa na mashirika mbalimbali ambayo yanaunga mkono mpango wa Serikali wa kumaliza vitendo hivyo.
“Serikali inafanya jitihada mbalimbali kumaliza vitendo hivi vya kikatili ambavyo wanafanyiwa wanawake ikiwepo kutoa elimu kwa kutumia vyombo vya habari … niwahakikishie Bunge la Tanzania na Serikali kwa ujumla itaendelea kushirikiana na wadau kupambana kumaliza vitendo vya ukeketaji kwa wanawake na wasichana,” alisema Dk. Tulia.
 
Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland Van De Geer.
Nae Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland Van De Geer alisema EU imekuwa na mipango mbalimbali ambayo imekuwa ikifanya kwa ajili ya kusaidia nchi ambazo zimebainika kuwepo kwa vitendo vya ukeketeaji kumaliza vitendo hivyo na itandelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha vitendo hivyo vinamalizika.
“EU ilitenga pesa kwa ajili ya kusaidia wanawake na wasichana na moja na mipango ya pesa hiyo ni kumaliza vitendo vya ukeketaji, EU inaamini kuwa wanawake wanahusika sana katika shughuli za maendeleo na ni muhimu kwao kulindwa na jamii nzima ili wawe salama,” alisema Van De Geer.
 
Balozi wa Italia nchini Tanzania, Roberto Mengoni.
Nae Balozi wa Italia nchini, Roberto Mengoni alisema Serikali ya nchi yake inapinga vitendo hivyo na tayari inashirikiana na Serikali za nchi za Afrika zilizo na vitendo vya ukeketaji na Tanzania ikiwa ni mojawapo, hivyo wataunga mkono juhudi za Serikali kuelimisha jamii iachane na vitendo hivyo.
Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ni moja ya nchi 29 za Afrika ambazo wanawake wa nchi hizo wanafanyiwa ukeketeaji ambapo asilimia 14.6 ya wanawake nchini wanakadiriwa kufanya vitendo hivyo na mkoa wa Manyara ukiongoza kwa asilimia 58 kwa wanawake wanaoishi katika mkoa huo kufanyiwa vitendo vya ukeketaji.

0 Responses to “SERIKALI YAAHIDI KUENDELEZA VITA YA KUZUIA VITENDO VYA UKEKETAJI KWA WANAWAKE”

Post a Comment

More to Read