Sunday, February 26, 2017

TAARIFA: TCU YATOLEA UFAFANUZI UHAKIKI WA WANAFUNZI ULIOFANYIKA




TUME YA VYUO VIKUU TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UFAFANUZI WA
UHAKIKI WA SIFA ZA WANAFUNZI WA VYUO VYA
ELIMU YA JUU 2016/17

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inapenda kuuarifu
umma kuwa, uhakiki wa ubora wa wanafunzi wa elimu ya juu
hufanyika kwa mujibu wa Kifungu 5(1)(b)(c) cha Sheria ya
Vyuo Vikuu Sura ya 346 ya Sheria za Tanzania.

Katika kutekeleza jukumu hili Tume ilianza zoezi la uhakiki
kuanzia mwezi Agosti 2016. Hadi kufikia Februari 2017 zoezi
hilo lilikuwa limekamilika kwa vyuo 67 kati ya 84 vinavyotoa
shahada ya kwanza. Hii ni mara ya kwanza uhakiki wa sifa za
wanafunzi wa vyuo vyote nchini kufanyika kwa wakati
mmoja. Lengo la uhakiki lilikuwa kujiridhisha kuwa
wanafunzi waliopo vyuoni ni wale waliodahiliwa kwa mujibu
wa sheria na taratibu na kwamba wanakidhi vigezo stahiki.

Uhakiki ulifanyika kwa kulinganisha taarifa za TCU na zile
zilizowasilishwa na vyuo. Uhakiki huo ulihusisha jumla ya
wanafunzi 131,994 waliopo vyuoni kwa mwaka wa masomo
2016/17.

Baada ya kulinganisha orodha zilizowasilishwa na vyuo na ile
ya TCU ilibainika kuwa wanafunzi 123,827 sawa na asilimia
93.8 wana na sifa stahiki. Aidha jumla ya wanafunzi 8,167
sawa na asilimia 6.2 tu walibainika kuwa na kasoro katika
taarifa za sifa zao.
2
Kufuatia hali hiyo, Tume ilitoa taarifa kwa umma kuwaomba
wanafunzi kurekebisha dosari hizo kwa kuthibitisha taarifa
zao kupitia vyuo husika ifikapo tarehe 28 Februari 2017 ili
kuweka kumbukumbu sahihi za mwanafunzi.

Hata hivyo imebainika kuwa taarifa hiyo imepokelewa kwa
mtazamo na hisia tofauti na hivyo kusababisha mkanganyiko
vyuoni. Umma unaarifiwa kwamba haikuwa nia wala lengo la
Tume kusababisha mkanganyiko huo.

Kwa kuwa uhakiki wa sifa za wanafunzi ni kazi endelevu ya
Tume na kutokana na maombi ya wadau mbalimbali, Tume
sasa itaendelea kuwasiliana moja kwa moja na vyuo katika
kukamilisha zoezi hilo. Hivyo wanafunzi wote waliokuwa
wameorodheshwa katika taarifa iliyotolewa awali
wanaombwa kuwa watulivu na kuendelea na masomo yao
kama kawaida.

Aidha ifahamike kuwa wanafunzi waliokuwa
wameorodheshwa siyo kwamba wamethibitika kuwa hawana
sifa stahiki bali kuna dosari katika taarifa zao. Ndiyo sababu
Tume iliwaomba kuthibitisha taarifa zao ili kuondoa dosari
hizo.
Imetolewa na
Kaimu Katibu Mtendaji
24 Februari 2017

0 Responses to “TAARIFA: TCU YATOLEA UFAFANUZI UHAKIKI WA WANAFUNZI ULIOFANYIKA”

Post a Comment

More to Read