Friday, February 24, 2017
WAZIRI MWAKYEMBE AANDIKIWA BARUA YA ONYO
Do you like this story?
Chama
cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS) kimemwandikia barua Waziri wa
Katiba na Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe kikimtaka aache kuingilia
uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Barua hiyo imekuja
baada ya Dkt. Mwakyembe kudaiwa hivi karibuni kutishia kuifuta TLS kwa
madai kwamba imeanza kuingiliwa kisiasa.
Barua hiyo iliyoandikwa na kusainiwa na
Rais wa EALS, Richard Mugisha, inasema TLS si chama cha kisiasa na
kimeanzishwa kwa kufuata sheria zote. “Mheshimiwa Waziri, tumesikitishwa
na taarifa ambazo zimeenea kwenye vyombo vyote vya habari na gazeti la
East African la Februari 18 ambalo limekunukuu ukisema kwamba Chama cha
Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kina muingiliano wa kisiasa,” inasema
sehemu ya barua hiyo.
Katika barua hiyo, Mugisha anasema
wanasheria wanatakiwa wapewe uhuru, wasiingiliwe na serikali kama ilivyo
kwa nchi nyingine kwani kuingilia ni sawa na kuvunja sheria za nchi.
Rais wa sasa wa TLS, John Seka amesema
kuwa chama chake kimefurahishwa na barua hiyo kwa Waziri na kwamba nao
pia wanafanya taratibu kumuona ili kujadili mustakabali wa chama hicho.
Alisema kuwa TLS inaendelea na mchakato wa uchaguzi kama ulivyopangwa na
kuwataka wagombea wote kujiandaa kwa uchaguzi huo ambao alisema ni
halali.
Uchaguzi wa chama hicho unatarajiwa
kufanyika machi 18 mwaka huu, huku wagombea kutoka vyama vya upinzani
wakiwa wamejitokeza kuwania nafasi ya uongozi wa juu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI MWAKYEMBE AANDIKIWA BARUA YA ONYO ”
Post a Comment