Wednesday, September 13, 2017
Mugabe amzuia msanii wa kike kuingia Zimbabwe kwa kutovaa nguo za ndani
Do you like this story?
Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe ameripotiwa kumpiga marufuku
mtumbuizaji wa kike wa Afrika Kusini, Zodwa Wabantu kutumbuiza nchini
humo kutokana na tabia yake ya kupanda jukwani bila kuvaa nguo za ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufungua kituo
cha taarifa za jamii cha Bindura nchini humo (Bindura Community
Information Centre) hivi karibuni, Rais Mugabe alisema kuwa amemzuia
Zonda kwakuwa vitendo vyake vya kupanda jukwaani bila nguo ya ndani
haviendani na maadili ya nchi hiyo.
Mugabe aliwaomba radhi wanaume ambao alidai kuwa amesikia wakilalamika kuhusu uamuzi huo.
“Hatutaki mtu yeyote msumbufu kuja nchini kwetu akiwa mtupu kwa ajili
ya kusababisha matatizo. Nini hasa lengo lake la kuja hapa? Rais
Mugabe alihoji.
“Ili wanaume waweze kukuona? Poleni. Tumewaangusha wanaume wengi
ambao walikuwa wanalalamika. Nimesikia walikuwa wanataka [Zodwa] aje.
Hayo ni mawazo ambayo hatuyataki, acha hayo yafanyike huko anakotoka
(Afrika Kusini),” anakaririwa na mtandao wa Zimbabwe wa Bulawayo24.
Zodwa ambaye ni mtumbuizaji maarufu anayepanda jukwaani akiwa na nguo
zake isipokuwa nguo za ndani, alikuwa amealikwa kushiriki tamasha
maarufu la kimataifa jijini Harare la ‘Harare International Carnival’.
Vyombo vya habari vya Zimbabwe vimeeleza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Maadili ambaye pia ni Waziri wa zamani wa nchi hiyo, Aeneas Chigwedere
alisema kuwa vitendo vya Zodwa ni kinyume cha maadili na kwamba uamuzi
wa Serikali umelenga kuwalinda vijana na jamii kwa ujumla dhidi ya
kumomonyoka kwa maadili.
Tamko la Serikali hiyo lilitolewa muda mfupi baada ya baadhi ya
wasanii wa nchi hiyo kulalamikia kitendo cha waandaaji wa tamasha hilo
kutaka kuwatumia zaidi wasanii wa nje ya nchi na kuwaacha wasanii wa
ndani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “Mugabe amzuia msanii wa kike kuingia Zimbabwe kwa kutovaa nguo za ndani”
Post a Comment