Wednesday, September 13, 2017

Bunge laziunganisha TRL na RAHCO



Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha muswada wa sheria ya reli ya mwaka 2017 (The Railways Act, 2017) ambao unapendekeza kuanzisha Shirika la Reli Tanzania (TRC) litakalokuwa na jukumu la kusimamia, kuendeleza miundombinu ya reli na kutoa huduma ya usafiri wa reli.
Hayo yamesemwa hii leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa alipokuwa akiwasilisha muswada huo, ambapo amesema kuwa dhumuni ya muswada huo ni kuweka mfumo madhubuti wa utoaji huduma ya usafiri wa reli, usimamizi na uendelezaji wa miundombinu ya reli.
“Muswada huu unaainisha utaratibu wa kuhamisha watumishi kutoka (Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Nchini (RAHCO) kwenda katika Shirika jipya,” amesema Prof. Mbarawa.
Amesema kuwa muswada huo pia unaainisha vyanzo vya mapato ambavyo ni pamoja na mfuko wa reli, ruzuku toka Serikalini, nauli za abiria pamoja na uhifadhi wa eneo la reli.
Prof. Mbarawa ameongeza kuwa TRL ilikuwa ikisimamia masuala ya usafiri wa gari moshi (treni) na RAHCO ilikuwa ikisimamia miundombinu, kwa kipindi chote ambacho taasisi hizo zimetenganishwa katika utendaji kazi kumesababisha kushuka kwa mapato na utendaji wa TRL.
Hata hivyo, amesema kuwa, Serikali imechagua Shirika kuitwa TRC kutokana na namna ambavyo Watanzania waliliamini shirika hilo kabla ya kubadilishwa jina kwenda TRL ambapo kumekuwa na changamaoto nyingi  ikilinganishwa na hapo awali.

0 Responses to “Bunge laziunganisha TRL na RAHCO”

Post a Comment

More to Read