Tuesday, March 18, 2014

HOTUBA YA JAJI JOSEPH WARIOBA ALIYOSOMA KWENYE BUNGE MAALUM LA KATIBA LEO.





HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, MHE. JAJI JOSEPH SINDE WARIOBA, AKIWASILISHA RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA BUNGE MAALUM LA KATIBA, MACHI 2014  ________________ UTANGULIZI

Mheshimiwa Mwenyekiti.

Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba,
Kwa mujibu wa kifungu 20 (3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 na Tangazo la Serikali Na. 30 la tarehe 14 Februari, 2014, naomba kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la Katiba. Rasimu ya Katiba ninayoiwasilisha imeandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kukamilisha kazi ya kuratibu, kukusanya, kuchambua na kutathmini maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya. 2.

Mwanzo kabisa, nieleze kwamba, Maelezo haya ninayoyatoa, ni sehemu ya Randama (Memorandum) iliyoandaliwa na Tume kwa lengo la kufafanua kwa kina, maudhui ya kila Ibara iliyomo katika Rasimu ya Katiba na sababu za mapendekezo ya Ibara hizo. Hivyo, naomba maelezo yote yaliyomo katika Randama yawe sehemu ya maelezo yangu na yaingizwe katika kumbukumbu za Bunge hili. 3.

Rasimu ya Katiba ni miongoni mwa Nyaraka zilizoambatanishwa katika Ripoti ya Tume kuhusu Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuliyowakabidhi Waheshimiwa Marais tarehe 30 Desemba, 2013. Nyaraka nyingine ni:

Taarifa ya Maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba. Taarifa hii ina maoni ya Wananchi kuhusu maeneo mbalimbali ya kikatiba ambayo ndio msingi wa uandishi wa Rasimu ya Katiba; (b)

Taarifa ya Mabaraza ya Katiba ambayo inaainisha maoni ya Wananchi kuhusu Ibara zilizokuwemo katika Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba na jinsi zilivyofanyiwa kazi; (c)

Taarifa ya maoni ya Wananchi kuhusu Sera, Sheria na Utekelezaji. Taarifa hii ina maoni ya wananchi kuhusu mambo ambayo yanahitaji kufanyiwa uamuzi wa kisera, kutunga au kurekebisha sheria zilizopo au utekelezaji wa kiutendaji; (d)

Taarifa ya Utafiti Kuhusu Masuala Mbalimbali ya Kikatiba, ambayo ina taarifa nne ambazo ni: (i)

Utafiti Kuhusu Madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; (ii)

Utafiti Kuhusu Maadili ya Viongozi na Uwajibikaji; (iii)

Utafiti Kuhusu Masuala Yanayohusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar; na (iv)

Ushauri Elekezi Kuhusu Mifumo ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi, Tanzania (Final Report on the Review of Various  Aspects of Electoral Systems and the Electoral Commission in Tanzania). (e)

Taarifa ya Takwimu za Ukusanyaji wa maoni ya Wananchi ambayo inaainisha maeneo makuu yaliyotolewa maoni, jinsi, elimu na kazi za watoaji maoni; na (f)

 Viambatisho vya Ripoti ambavyo vinaainisha hatua mbalimbali za mchakato, uamuzi, hotuba za viongozi na miongozo mbalimbali iliyotolewa na Tume. 4.

Ripoti ya Tume na baadhi ya Taarifa zimegawiwa kwa kila Mjumbe na Taarifa nyingine zimewekwa katika Maktaba ya Bunge ili kuwawezesha Wajumbe kufanya marejeo. Tume inaamini kwamba Ripoti na Taarifa zinazowasilishwa pamoja na maelezo haya zitawasaidia Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kujadili na kufanya uamuzi sahihi kwa kila Ibara iliyopendekezwa kwa kuzingatia maslahi ya wananchi na Taifa kwa jumla
 

Rais, atabaki na madaraka ya kuwateua viongozi wa kitaifa, kama vile Mawaziri, Majaji, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu Wakuu wa Wizara na Wenyeviti na Wajumbe wa Tume za kitaifa. Pamoja na kubaki na madaraka hayo, Rais amewekewa utaratibu wa uteuzi. Baadhi ya viongozi watateuliwa moja kwa moja na Rais na baadaye watathibitishwa na Bunge, kwa mfano, Mawaziri. Wengine watapendekezwa na Kamati ya Uteuzi na baada ya kuteuliwa, watathibitishwa na Bunge, kwa mfano, Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi. Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama watateuliwa na Rais kwa kushauriana na Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa. Wengine watateuliwa kutokana na ushauri wa Tume za Utumishi, kama vile Majaji na Makatibu Wakuu.
Bunge

Mheshimiwa Mwenyekiti;


Kwa Bunge la Muungano, madaraka yake na mamlaka yatabaki kusimamia mambo ya Muungano. Kinachobadilika sasa ni Bunge kutokuwa na mamlaka juu ya mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika kama ambavyo imekuwa kwa upande wa Zanzibar. Hata hivyo, Bunge la Muungano litapata taarifa ya uratibu na utekelezaji wa mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika na ya Zanzibar kupitia Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali

Imependekezwa pia kwamba Spika na Naibu Spika wasitokane na Mawaziri, Naibu Mawaziri au Wabunge. Lengo la pendekezo hili ni kupata viongozi ambao wataonekana hawaegemei upande wowote. Imependekezwa pia kwamba Wabunge wasiwe Mawaziri. Pendekezo hili limetokana na maoni ya wananchi
 
kwamba wanahitaji Wabunge kuwa karibu na wapiga kura wao. Wengine wanaamini kwamba wabunge ambao ni Mawaziri wanapendelea majimbo yao ya uchaguzi badala ya kutumikia taifa kwa ujumla kwa usawa.

Lakini lengo jingine la pendekezo hili, ni kutenganisha madaraka ya mihimili. Kama Bunge likiwa na madaraka ya kuthibitisha Mawaziri itakuwa vigumu kwa Wabunge kuwakataa Wabunge wenzao watakaoteuliwa kuwa Mawaziri, kisha kuendelea kukaa pamoja kwa utulivu ndani ya Bunge

Tume imependekeza ukomo wa ubunge kuwa vipindi vitatu vya miaka mitano mitano. Hata hivyo, wananchi wanaweza kumwondoa Mbunge wao kabla ya kumaliza muda wa kipindi chake cha miaka mitano. Pendekezo hili linatokana na maoni ya wananchi waliotaka kuwepo ukomo wa ubunge ili kuondoa dhana ya umiliki wa jimbo la uchaguzi, kutoa fursa kwa wananchi wengine wenye uwezo kugombea nafasi ya ubunge, kuongeza uwajibikaji wa wabunge katika majimbo ya uchaguzi na kuongeza mamlaka ya wananchi kuwawajibisha viongozi wao.

Pia, ni maoni ya wananchi kuwa kusiwepo uchaguzi mdogo ili kupunguza gharama. Endapo nafasi ya ubunge itaachwa wazi kutokana na mbunge wa chama cha siasa kupoteza Ubunge, basi Tume Huru ya Uchaguzi itajaza nafasi hiyo kutokana na orodha ya majina yaliyowasilishwa na chama cha siasa husika na kwa kushirikiana na chama hicho. Uchaguzi mdogo utafanyika tu pale ambapo nafasi ya ubunge iliyo wazi imetokana na mbunge huru.
 
Mahakama

Kuhusu Mahakama, pendekezo kubwa ni kuundwa kwa Mahakama ya Juu na kwamba Mahakama hiyo na Mahakama ya Rufani ndizo ziwe Mahakama za Muungano. Mahakama Kuu ziendelee kutokuwa za Muungano kama ilivyo sasa. Hata hivyo, inapendekezwa kuwa Mahakama Kuu ya Tanganyika na Mahakama Kuu ya Zanzibar ziwe na mamlaka sawa katika kusikiliza na kuamua mashauri yanayohusu masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano (concurrent  jurisdiction). Hivi ndivyo ilivyo hivi sasa kwa upande mmoja, ambapo Mahakama Kuu ya Zanzibar, japokuwa si sehemu ya Mahakama za Jamhuri ya Muungano, lakini imepewa mamlaka na Katiba ya Jamhuri ya Muungano kusikiliza na kuamua kuhusu mashauri ya kesi za madai na jinai yanayohusu sheria za muungano. Pendekezo jingine ni kuuweka Mfuko wa Mahakama ndani ya Katiba.

0 Responses to “HOTUBA YA JAJI JOSEPH WARIOBA ALIYOSOMA KWENYE BUNGE MAALUM LA KATIBA LEO.”

Post a Comment

More to Read