Thursday, March 20, 2014

MIRADI KUKABILI FOLENI YASUASUA.






Kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam inaonekana si ya kuridhisha licha ya ukubwa wa tatizo lenyewe.

Miradi hiyo ilitangazwa bungeni na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli katika hotuba yake ya Bajeti ya Mwaka 2013/2014.
Baadhi ya miradi iliyotangazwa na waziri ni pamoja na ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara  (flyover).

Mradi huu bado haujaanza kutekelezwa licha ya Dk. Magufuli kulieleza Bunge kuwa wakati ule walikuwa katika mchakato wa kumpata mkandarasi.

Mradi mwingine ni ujenzi wa kivuko au boti kutoka Dar es Salaam mpaka Bagamoyo chenye uwezo wa kubeba watu 300.
Mradi huu pia ungesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano kwani baadhi ya watu wangesafiri kwa kutumia kivuko au boti maalumu mpaka Bagamoyo.

Dk. Magufuli alisema katika hotuba yake kuwa mkandarasi wa mradi huo alikuwa amepatikana na usanifu wa maegesho matatu ulikuwa unaendelea.

Mpaka sasa hamna shughuli zozote zinazohusu mradi huo zinazoendelea, licha ya tamko hilo kutolewa na waziri mwenyewe.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamkama alisema ujenzi wa kivuko unaendelea mjini Bangladesh, India na mwezi wa tano kivuko hicho kitawasili nchini.

Ndyamkama alisema Tanroads wameanza maandalizi ya ujenzi wa Flyover maeneo ya Tazara na mpaka sasa wameondoa mabango ya matangazo, mabomba na nguzo za umeme  eneo ambako litajengwa daraja la juu.

“Kuhusu barabara alizozisema waziri, tayari makandarasi wameshapatikana na mikataba yote tuliyoingia ipo kwa Mwanasheria Mkuu. Utekelezaji utaanza baada ya Mwanasheria Mkuu kupitia mikataba hiyo,” alisema Ndyamkama.

Tatizo la msongamano wa magari Dar es Salaam  limeongezeka zaidi kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo  ujenzi wa mradi mwingine wa barabara za Mabasi Yaendayo Kasi (Dart).

0 Responses to “MIRADI KUKABILI FOLENI YASUASUA.”

Post a Comment

More to Read