Thursday, March 20, 2014

TRA MBEYA YAKIRI WINGI WA KODI NCHINI.


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mbeya imekiri kuwepo kwa utitiri wa kodi kwa wafanyabiashara ambazo sasa ni kero kwao na kwamba sasa inaangalia upya  njia sahihi ya kuzikusanya kwa pamoja.

Afisa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kissa Kyejo alitoa kauli hiyo mjini Chunya juzi,  wakati akijibu  kero mbalimbali za wafanyabiashara, kwenye semina iliyoandalia na TRA.

Semina hiyo ilihusu umuhimu kwa mfanyabiashara kulipa kodi kwa kutumia Mfumo wa Mashine za Ki-eletroniki (EFDs).

Kissa amesema wafanyabiashara maeneo mengi wamelalamikia kuwapo kwa utitiri huo na kwamba hata TRA  wameliona, na sasa walishapeleka ombi kwao ili ziweze kuunganishwa kwa pamoja.

Awali wafanyabiashara hao walilalamikia kuwapo aina mbalimbali za kodi   ambazo walidai  zimekuwa  kero kubwa kwao, ikiwamo usumbufu wanaoupata kutoka kwa maafisa  wa Serikali.

Mfanyabiashara wa Chunya Mjini, Ayubu Omari amesema: “Leo anakuja mtu wa TRA, tunamalizana naye, kesho mtu wa ardhi, mara wa  maji, hujakaa sawa watu wa  halmashauri nao wamefika wanataka ushuru. Sasa huu utitiri wa kodi kwetu tunaona ni usumbufu na kero.’
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro aliwataka wafanyabiashara hasa wachimbaji wadogo wa  dhahabu  kupitia Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mbeya, (Mberema) kuanza kulipa kodi. Amesema wachimbaji  wengi  wanapata fedha nyingi, lakini hawalipi kodi na hivyo kuikosesha serikali mapato.

0 Responses to “TRA MBEYA YAKIRI WINGI WA KODI NCHINI.”

Post a Comment

More to Read