Thursday, March 20, 2014

JAZIBA IEPUKWE KATIKA KUJADILI RASIMU YA KATIBA.





Hatimaye Rasimu ya Pili ya Katiba iliwasilishwa bungeni jana baada ya kutokea sintofahamu juzi na kusababisha  kusitishwa kwa kikao cha Bunge Maalumu la Katiba pasipo Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuiwasilisha bungeni kama ilivyokuwa imepangwa. Mtafaruku huo ulitokea baada ya baadhi ya wajumbe kupinga kuruhusiwa kwa Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo kabla Rais Jakaya Kikwete hajalihutubia Bunge kama Kanuni za Bunge zinavyoelekeza.

Kuwasilishwa kwa Rasimu hiyo jana kulitokana na kupatikana kwa maridhiano juzi usiku kati ya uongozi wa Bunge na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unaovishirikisha vyama vya upinzani na wajumbe wanaotokana na makundi yaliyotajwa katika kifungu cha 22(1)(C) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Umoja huo ulianzishwa kwa lengo la kuhakikisha mchakato wa Katiba unaiwezesha nchi yetu kupata Katiba Mpya na iliyo bora.

Ni vigumu kuelezea ukubwa wa vurugu zilizotokea bungeni juzi kutokana na ufinyu wa nafasi katika safu hii. Hata hivyo, viongozi wa Ukawa walitangaza mapema juzi kwamba wangepinga, pamoja na mambo mengine, ukiukwaji wa Kanuni na wangezuia ratiba  kuendelea hadi kwanza yasikilizwe madai yao ya kumtaka Rais Kikwete afungue Bunge kabla ya kuwasilishwa kwa Rasimu ya Katiba.Ndiyo maana Jaji Warioba aliposimama kwenye mimbari ya Bunge tayari kuwasilisha Rasimu hiyo, baadhi ya wajumbe walipiga kelele na kugonga meza, hivyo kumfanya ashindwe kufanya kazi hiyo. Kama tulivyodokeza hapo juu, uwasilishaji huo ulifanyika jana baada ya maridhiano kupatikana.

Sisi hatuwezi kuunga mkono vurugu Bungeni lakini tunadhani kwamba tukio hilo litakuwa limetoa fundisho kwa Mwenyekiti wa Bunge kwamba kamwe hataweza kuongoza chombo hicho pasipo kufuata Kanuni zilizotungwa kuendesha shughuli zake.

Mwenyekiti huyo anapaswa kujua kwamba alivunja Kanuni ya 7(1)(g) na (h) ambazo zimeweka mpangilio wa shughuli zote za Bunge la Katiba. Ratiba hiyo ilionyesha wazi kwamba hotuba ya ufunguzi ambayo itatolewa na Rais, itatangulia na kufuatiwa na uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba.

Tunashawishika kusema ukiukwaji huo wa Kanuni ulifanywa kwa makusudi, hasa tukizingatia uzoefu alioupata akiwa  Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano. Yatakuwa makosa makubwa iwapo atadhani kwamba makundi yenye wajumbe wachache yatakubali kuburuzwa, kwani Bunge la Katiba ni tofauti na Bunge la kawaida ambalo limekuwa na dhana potofu kwamba kundi lenye wabunge wengi ndilo lina haki ya kusikilizwa. 

Tunakubaliana na viongozi wa Ukawa wanapohadharisha kwamba Katiba hii itatumiwa na vizazi na vizazi, hivyo ni lazima itengenezwe kwa misingi ya kujali utu wa kila mtu, kuheshimiana na kukubaliana.

Ubabe na kukiuka Kanuni kwa kisingizio cha ‘busara za Mwenyekiti’ havikubaliki, isipokuwa tu pale Kanuni zinapokuwa hazielekezi chochote.

Tukio kubwa lililokuwa likisubiriwa ni uwasilishwaji wa Rasimu ya Katiba ambao ulifanywa jana na Jaji Warioba kwa utulivu, umakini, busara na ustadi mkubwa.

Alipewa muda wa kutosha kutoa ufafanuzi wa masuala mazito na alifanya hivyo bila ya kuwaburuza. Wajumbe sasa wanayo Rasimu mbele yao ambayo watapaswa kuijadili bila ya jazba, bali kwa kuzingatia hoja badala ya kuangalia nani anatoa hoja.

0 Responses to “JAZIBA IEPUKWE KATIKA KUJADILI RASIMU YA KATIBA.”

Post a Comment

More to Read