Thursday, March 20, 2014

SITA YU MSALABANI, KUONGOZA BUNGE MAALUMU LA KATIBA.




Mkanganyiko pekee na uliobakia kwa Watanzania  wakiwamo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ni viporo kwenye kanuni za 37 na 38, vinginevyo hali ya hewa ndani ya Bunge hilo imetulia.

Wajumbe wa Bunge hilo wapo tayari kuanza kibarua cha kwanza cha kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya, kazi ambayo  hakuna shaka ndiyo iliyowaweka Dodoma.

Hata hivyo, kabla ya mwenyekiti mteule Samuel Sitta kushinda kinyang’anyiro  cha kuongoza Bunge hilo wiki iliyopita, chama chake, CCM kimekuwa kikionekana kuwa na mkakati wa nguvu wa kushawishi na hatimaye kupitisha mapendekezo na matakwa yake, yakiwamo ya Serikali mbili.

Sitta ambaye amechaguliwa kwa asilimia 86.5 ya kura za wajumbe ana mtihani mzito aliobebeshwa mabegani ukiwamo wa kutetea msimamo wa chama chake au kuukana.

Akisaidiwa na Samia Suluhu Hassan ambaye naye amechaguliwa kwa asilimia 74, wawili hawa wana kibarua mbele yao.
Yeye (Sitta), ni muumini wa Serikali mbili kama ilivyo CCM, ingawa inaaminika kuwa amebadili msimamo kutoka ule wa awali wa Serikali tatu.

Tayari, ameahidi mbele ya wajumbe kulinda muungano kwa njia yoyote ile kupitia rasimu hiyo.
Mtego mpya kwake ndani ya Bunge ni imani kubwa ambayo  wajumbe hao wanayo kwake kwani bila kujali itikadi zao wamempitisha kuwa mwenyekiti wao kwa idadi ya kura 487, sawa na asilimia 86.5

Hii ni ishara ya kumwamini kwamba, atahakikisha anatetea masilahi ya Watanzania wote badala ya chama chake.
Matumaini hayo yanakuja baada ya kujijengea uaminifu mkubwa kupitia uongozi wake wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano kupitia kaulimbiu yake ya ‘kasi na viwango’.

Wapo  Watanzania wanaosema kuwa nafasi hiyo kwa Sitta inaweza kumjengea umaarufu ama kumwondolea imani kwao, endapo hatakuwa mwangalifu katika kuliongoza Bunge hilo.

0 Responses to “SITA YU MSALABANI, KUONGOZA BUNGE MAALUMU LA KATIBA.”

Post a Comment

More to Read