Thursday, September 25, 2014
SERIKALI YAZINDUA KAMPENI YA UPIMAJI VVU KAZINI KATIKA MKOA WA NJOMBE UNAOONGOZA KITAIFA KWA MAAMBUKIZI HAYO NJO
Do you like this story?
Katibu Mkuu Utumishi George Yambesi(kulia) akipewa ushauri nasaha kabla ya kupima VVU kwa hiari wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kuhamasisha Upimaji VVU Mahali pa Kazi uliofanyika mjini Njombe juzi |
Akitoa nasaha zake kwa wawakilishi wa mikoa ya Iringa na Njombe walioshiriki uzinduzi wa kampeni hiyo |
Huyu Anjela Kayombo ambaye pia ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe anayeishi na VVU tangu mwaka 1999 |
Hilda Kapanda mmoja wa watumishi wa halmashauri ya Njombe anayeishi na VVU akitoa ushuhuda wake |
Baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo wakiwa katika foleni wakisubiri kupima afya zao wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo. |
KAMPENI ya
kuhamasisha Upimaji wa Virusi vya Ukimwi mahali pa kazi imezinduliwa kitaifa
mkoani Njombe huku baadhi ya watumishi wenye maambukizi hayo wakilalamika
kutelekezwa.
Kauli Mbiu ya kampeni
hiyo iliyoanza Septemba 23 na itakayofanyika hadi Desemba 1, mwaka huu inasema
“mfanyakazi jitambue, pima mapema, epuka maambukizi mapya, ubaguzi na
unyanyapaa, zuia vifo vitokanavyo na Ukimwi.”
Alipokuwa akiizindua
kampeni hiyo Katibu Mkuu Utumishi, George Yambesi alisema kampeni hiyo inalenga
kutoa msukumo wa utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti Ukimwi kitaifa na
kimataifa ili kufikia azma ya sifuri tatu.
“Sifuri tatu kwa
maana ya maambukizi mapya sifuri, vifo sifuri na unyanyapaa sifuri ifikapo
mwaka 2015,” alisema mbele ya wawakilishi wa mikoa ya Njombe na Iringa
waliohudhuria uzinduzi huo.
Wakati mkoa wa Njombe
unaongoza kitaifa kwa kuwa na asilimia 14.8 ya maambukizi, mkoa wa Iringa ni wa
pili kitaifa kwa kuwa na asilimia 9.1 ya maambukizi.
Alisema kampeni hiyo
inahimiza utekelezaji wa dhati wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) na
maazimio yaliyowekwa kwenye Mkutano Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI
uliofanyika mwaka 2001 Jijini New York, Marekani.
Mbali na Virusi vya
Ukimwi (VVU), Yambesi alisema kwa kupitia kampeni hiyo watumishi na wananchi
wengine watapata fursa ya kupima magonjwa sugu yasio ya kuambuzwa kama
kisukari, shinikizo la damu, moyo, saratani, pumu na kupooza.
Alisema magonjwa hayo
ambayo zamani yalikuwa yakihesabika kama magonjwa yanayowaathiri zaidi watu
wenye uwezo mkubwa kiuchumi hivisasa yanaoonekana ni ya kawaida kwa watu wa
kawaida.
Yambesi alisema
kutopima afya kuna athari nyingi hasa kupungua kwa nguvu kazi, kuongezeka kwa
gharama za matibabu na kupungua kwa tija inayoathiri ukuaji wa pato la taifa.
“Ili kuepuka matatizo
hayo kuna kila sababu ya kuhamasiha watumishi wa umma kujali afya zao na kupima
ili wachukue hatua kama wahenga walivyosema kinga ni bora kuliko tiba,”
alisema.
Alisema katika
kutekeleza ya wahenga ni muhimu kupima afya mara kwa mara kunasaidia kuepuka
maambukizi mapya na wale wenye VVU kupunguza athari ya kuambukizi wengine,”
alisema.
Alisema kwa takwimu
za mwaka 2013, Tanzania ina watumishi wa umma zaidi ya 500,000 ambao ni
sehemu muhimu ya nguvu kazi ya taifa hivyo wanaohitaji kuwa na afya bora ili
watekeleze wajibu wajibu wao.
“Tumekwisha weka
misingi mizuri ya kulinda afya zetu kwa kuandaa waraka kuhusu Ukimwi na
magonjwa sugu yasio ya kuambukizaa. Ni muhimu kwa taasisi za serikali
kutekeleza maelekezo yote ili watumishi wa umma wawe ni wale wenye afya bora,”
alisema.
Alisema watumishi
wanapaswa kuwa wazi baada ya kugundulika na maambukizi ya VVU ili waweze kupata
huduma muhimu ikiwemo ya matumizi ya dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs).
Watumishi wawili wa
idara ya afya ya halmashauri ya wilaya ya Njombe wenye maambukizi ya VVU,
Anjela Kayombo na Hilda Kapanda walisema pamoja na serikali kusisitiza mara kwa
mara kuwasaidia watu wenye matatizo hayo, ahadi hiyo imeendelea kuwa hewa.
“Tunajua serikali
inayo sera inayolenga kuwasaidia wenye VVU kwa dawa, lishe na vitu vingine,
lakini sisi hatujawahi pata chochote,” alisema Kayombo.
Kampeni hiyo
inafanywa kwa pamoja na serikali na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambalo katika
uzinduzi huo liliwakilishwa na Getrude Sima ambaye ni Mratibu wa Ukimwi mahali
pa kazi wa shirika hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SERIKALI YAZINDUA KAMPENI YA UPIMAJI VVU KAZINI KATIKA MKOA WA NJOMBE UNAOONGOZA KITAIFA KWA MAAMBUKIZI HAYO NJO”
Post a Comment