Thursday, March 20, 2014

SERIKALI KUHAMIA DODOMA KESHO.




Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mh.Samuel Sitta(kushoto) na Makamu Mwenyekiti Mhe.Samia Suluhu(kulia).


UONGOZI wa juu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kesho utahamia katika Makao Makuu ya Tanzania, Dodoma, kushuhudia hotuba ya kihistoria itakayotolewa na Rais Jakaya Kikwete mbele ya Bunge Maalumu la Katiba.

Hotuba hiyo ya Rais inasubiriwa kwa hamu na Watanzania, kutoa dira kwa wajumbe wa Bunge hilo
Maalumu la Katiba, wakati watakapokuwa wakiandika Katiba mpya.

Mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo, ambaye ni mmoja wa wanasiasa wakongwe, aliliambia gazeti hili kuwa anatarajia hotuba ya Rais Kikwete itakuwa ya kujenga Bunge na sio kubomoa kwa kuzungumzia misimamo ya vyama.

“Yeye ni kiongozi wa Taifa, hivyo natarajia atakuja hapa kutupa njia na namna ya kushughulikia changamoto zilizopo wakati tunapoenda kuandika Katiba mpya,” alisema mwanasiasa huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Akizungumza jana na waandishi wa habari Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahya Khamis Hamad alisema Rais atahutubia Bunge saa 10 jioni na wageni waalikwa watatakiwa kuwa wameketi katika maeneo yao saa tisa alasiri.

Hamad alisema ratiba ya shughuli hiyo itaanza na kikao cha Bunge saa 9.10 na baadaye kikao hicho kitaahirishwa saa 9.20 kwa ajili ya kumpokea Rais Kikwete.

Wageni mashuhuri
Hamad alisema Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, amewaalika wageni mbalimbali kushuhudia tukio hilo muhimu la kitaifa, wakiwemo viongozi wa kitaifa na watendaji wakuu kutoka pande zote za Muungano.

Miongoni mwa wageni mashuhuri watakaokuwepo ni pamoja na mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere na marais wastaafu Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wengine ambao wamealikwa kuhudhuria tukio hilo ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, wajumbe wenzake na makamishna wote wa Tume hiyo.

Pia watakuwepo viongozi wengine wastaafu wa kitaifa ambao ni mawaziri wakuu wastaafu, Waziri Kiongozi mstaafu na maspika wa Bunge.

Wageni wengine walioalikwa ni kutoka taasisi za dini, taasisi zisizo za kiserikali, wawakilishi wa tasnia ya habari, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu na taasisi za elimu ya juu.

Pia vipo vyama vya watu wenye ulemavu, vyama vya wafanyakazi, vyama vya wafugaji, vyama vya wavuvi na wakulima pamoja na wawakilishi kutoka sekta binafsi.

Kuwasili kwa JK
Baada ya Rais kuwasili katika eneo la Bunge, atapokewa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba na baadaye kwenda katika jukwaa maalumu kupokea salamu za heshima na kukagua gwaride maalumu lililoandaliwa na Polisi.

Katibu wa Bunge alisema baada ya shughuli zote zitakazofanyika katika viwanja vya Bunge kumalizika, utaratibu umewekwa kwa viongozi kuingia bungeni kwa maandamano maalumu.

Viongozi watakaotangulia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Gharib Mohammed Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Rais Kikwete ambaye atakuwa amefuatana na mwenyeji wake ambaye ni Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta.

Baada ya Rais kumaliza kuhutubia Bunge Maalumu, wajumbe wote wa Bunge Maalumu watapata fursa ya kupiga picha ya pamoja mbele ya jengo la Bunge.

Rais atalihutubia Bunge ili kutoa nafasi kwa bunge hilo kuendelea na mjadala baada ya Jaji Warioba kuwasilisha rasimu ya pili ya Katiba, Jumanne wiki hii.

Hotuba ya Jaji Warioba ambayo ilijaa tafiti nyingi inaonekana kuwachanganya wajumbe wengi kwa kuamini kuwa imeibua mambo mengi ambayo yalikuwa yamefichika.

0 Responses to “SERIKALI KUHAMIA DODOMA KESHO.”

Post a Comment

More to Read