Tuesday, March 25, 2014

SERIKALI YAMTIMUA KAZI MKURUGENZI WA BODI YA UTALII NCHINI.




MKURUGENZI Mtendaji wa Bodi ya Utalii (TTB), Dk Aloyce Nzuki amevuliwa madaraka kwa madai ya utendaji usioridhisha pamoja na kusababisha Tanzania kuwa nyuma katika masuala ya utalii.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alitangaza uamuzi huo jana kwa waandishi wa habari. Amesema hatua yake hiyo, imetokana na Bodi ya Utalii, kumshauri amwondoe kazini mkurugenzi huyo.

Nyalandu amesema alipokea barua iliyosainiwa na wajumbe wote wa Bodi ya Utalii, wakimuomba amuondoe kazini Mkurugenzi huyo.

“Leo (jana) baada ya kufanya kikao na wajumbe wa TTB, nimeridhia kuondolewa kazini kwa Mkurugenzi huyo na Wizara itampangia kazi nyingine,” alisema Nyalandu.
Kikao cha pamoja kati ya Bodi na Waziri Nyalandu, kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri, Mahamoud Mgimwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Selestine Gesimba.

Kutokana na uamuzi huo, kuanzia leo Bodi ya Utalii imeagizwa kutangaza nafasi ya kazi hiyo na mwenye sifa atume maombi ndani ya siku 21.

Amesema baada ya siku 21, TTB ichague kampuni zitakazohusika kuchambua watu wenye sifa. Mchakato huo unaelekeza kampuni husika kupokea na hatimaye kupata majina tisa, ambayo pia yatachambuliwa na kisha kuwasilisha wizarani majina matano.

Wizara pia itachambua na kuwasilisha majina matatu kwenda kwa Rais, ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuteua jina moja la Mkurugenzi wa bodi hiyo.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Masoko, Devota Mdachi ameteuliwa kukaimu nafasi hiyo ya ukurugenzi wa TTB hadi hapo mchakato wa kumpata mkurugenzi, utakapomalizika.Nyalandu alisisitiza kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha utalii unakwenda popote duniani.

Awali, akizungumza, Mwenyekiti wa Bodi, Charles Sanga alisema Bodi hiyo ilimshauri Waziri kumuondoa kazini Mkurugenzi huyo kutokana na kutokuwa na imani naye na utendaji usioridhisha.

“Ili Bodi ifanye kazi kwa ufanisi, inahitaji utendaji mzuri ambao utakuwa umeboreshwa… hivyo tumemshauri Waziri, Dakta Nzuki aondoke, apishe nanafasi yake ichukuliwe na mwingine, kwani hatuwezi kufanya naye kazi,” alisema Sanga.
 CHANZOO:HABARI LEO

0 Responses to “SERIKALI YAMTIMUA KAZI MKURUGENZI WA BODI YA UTALII NCHINI.”

Post a Comment

More to Read