Saturday, March 22, 2014

TWITE NA KAVUMBAGU WAPEWA SIKU 30 YANGA.




MBUYU Twite na Didier Kavumbagu wa Yanga wana siku 30 tu za kuitumikia klabu hiyo kabla ya kufanya uamuzi mgumu wa kubaki au kuondoka Yanga. Siku hizo zinaanza leo mpaka Aprili 19 msimu utakapomalizika na Aprili 20 watakapokuwa na kikao Jangwani kutathmini msimu ikiwemo kupongezana kama watafanikiwa kutetea ubingwa wao.

Mastaa hao ni miongoni mwa wachezaji wanane wa Simba na Yanga ambao wapo sokoni na wanaweza kusaini mkataba na klabu yoyote muda wowote kuanzia sasa na siku ambazo klabu zao zitawamiliki kihalali hazizidi 30 kuanzia sasa.

Ingawa klabu zao zimekuwa bize kuwania nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, baadhi ya wachezaji hao wameanza nyodo na kusisitiza kwamba hawatasaini na klabu hizo mpaka mwisho wa msimu huku ikionekana kama wanataka kutingisha kiberiti wapewe dau nono.

Uchunguzi wa Mwanaspoti ambao umethibitishwa na wachezaji hao umeonyesha kwamba wachezaji wa Yanga ambao mikataba yao inamalizika mwezi Aprili 19 Ligi ya Bara itakapomalizika ni kipa, Ali Mustapha ‘Barthez’ ambaye habari za uhakika zinaeleza mazungumzo yake ya kurejea Simba yanakwenda vizuri, beki wa pembeni Mbuyu Twite, washambuliaji Didier Kavumbagu na Said Bahanuzi aliyegoma kutolewa kwa mkopo kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu.

Kwa upande wa Simba wachezaji wanne ambao mikataba yao ipo ukingoni ni viungo, Uhuru Selemani na Ramadhani Chombo ‘Redondo’, kipa raia wa Ghana Yaw Berko ambao wote hata hivyo hawajawahi kuwa na uhakika wa namba kwenye kikosi cha kwanza tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.Mchezaji mwingine ni beki wa pembeni Haruna Shamte. 

Twite amesisitiza kwamba hatasaini mkataba mpya na Yanga mpaka msimu utakapomalizika huku ikitafsiriwa kwamba anataka kutingisha kiberiti ili kurekebishiwa baadhi ya vipengele kwenye mkataba wake na amewaambia marafiki zake wa karibu kwamba hana raha kwa jinsi anavyoishi na vigogo wa Yanga kwa sasa.
Habari za ndani zinadai kwamba mchezaji huyo amewahi kufanya mazungumzo na viongozi wa Azam miezi michache iliyopita hivyo ana imani kwamba huenda wakampa ofa.

Kavumbagu ambaye amekuwa tegemeo kwenye fowadi ya Yanga alisema: “Bado sijasaini mkataba mwingine wa kuichezea Yanga, mkataba wangu unamalizika mwishoni mwa msimu huu (Aprili 19), ingawa tayari nimeanza mazungumzo ya awali ambayo bado hatujafikia muafaka wa kusaini mkataba mpya.”

Uhuru wa Simba ambaye amekuwa hana wakati mzuri kikosini alisema: “Nikikubali kubaki Simba naamini nitaua soka langu, hata kama wakinihitaji nibaki kwa kweli sibaki. Sasa nafikiria kuchezea timu nyingine tofauti na Simba kwani zipo nyingi zinazoweza kunisajili maisha popote na hilo linawezekana kutokana na kiwango changu nilichokuwa nacho, nikimaliza mkataba wangu niondoke.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah Bin Kleb alisema hawana presha na usajili wa wachezaji hao na kwamba wanachofanya sasa ni kupigana kiume kutetea ubingwa wao kwanza na wakishamaliza tu msimu watatatua suala la mastaa hao.
“Kwa sasa tunafikiria ubingwa kama unavyoona ligi imefikia katika hatua ngumu,” alisema Bin Kleb ambaye ana ushawishi mkubwa ndani ya Yanga kuanzia kwa wachezaji, wanachama mpaka viongozi wenzake.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspope hayupo nchini lakini wiki iliyopita aliisisitizia Mwanaspoti kwamba wana mpango wa kuipanga upya timu hiyo.

0 Responses to “TWITE NA KAVUMBAGU WAPEWA SIKU 30 YANGA.”

Post a Comment

More to Read