Saturday, March 22, 2014
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,JAKAYA MRISHO KIKWETE, WAKATI AKIZINDUA BUNGE MAALUM LA KATIBA, TAREHE 21 MACHI, 2014, DODOMA .
Do you like this story?
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
WAKATI WA KULIHUTUBIA BUNGE MAALUM LA
KATIBA, TAREHE 21 MACHI, 2014, DODOMA
Mheshimiwa Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na
Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania;
Mheshimiwa Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni waalikwa;
Pongezi
Nakushukuru
sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa ya kuja kuzungumza na Waheshimiwa
Wajumbe wa Bunge letu Maalum la Katiba katika siku hii muhimu na ya kihistoria
kwa nchi yetu. Nimekuja kuwatakia heri na naungana na Watanzania wenzetu
wote kuwaombea baraka za Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya kazi yenu kwa
utulivu, hekima, umakini mkubwa na kuimaliza kwa salama na kwa mafanikio yanayoyatarajiwa
na Watanzania.
Natoa
pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge
hili maalumu na la kihistoria. Ushindi mkubwa mliopata ni kielelezo tosha
cha imani kubwa na matumaini waliyonayo Wajumbe wenzenu kwenu. Matumaini yao
ndiyo matumaini ya Watanzania wote, kwamba mtaliongoza vizuri Bunge hili, ili
liweze kutimiza kwa ufanisi mkubwa jukumu lake muhimu sana katika historia ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Niruhusu
pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa bahati ya
aina yake waliyopata ya kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Fursa hii hutokea mara chache sana katika historia ya nchi yo yote na
watu wake. Mkifanikiwa kuipatia nchi yetu Katiba nzuri majina yenu
yataandikwa kwa wino wa dhahabu, katika kumbukumbu za historia ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Ni
matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga Katiba itakayokubalika na wengi.
Katiba inayotekelezeka. Katiba itakayoimarisha Muungano wetu kwa kuondoa
changamoto zilizopo sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu mfumo bora wa
kuongoza na kuendesha mambo yetu. Katiba itakayoimarisha umoja, upendo,
ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania, licha ya tofauti
zao za asili za upande wa Muungano na maeneo watokako, au tofauti za jinsia,
rangi, kabila, dini na ufuasi wa vyama vya siasa. Katiba itakayodumisha
amani, usalama na utulivu nchini. Katiba itakayostawisha zaidi
demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria, utawala bora na kudhibiti
maovu.
Na,
mwisho ingawaje siyo mwisho kwa umuhimu, Katiba itakayoweka mazingira mazuri
kwa uchumi wa nchi kukua, na wananchi wengi kunufaika sawia na maendeleo
yatayopatikana.
Historia ya Katiba Nchini
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Hii
itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili
26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato wa kutunga Katiba mpya. Mara ya
kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya Muda na mara ya pili ni mwaka
1977 ilipotungwa Katiba ya Kudumu tuliyonao sasa. Tofauti na mara mbili
zilizopita, safari hii mchakato unahusisha watu wengi zaidi. Wananchi
wameshiriki moja kwa moja kutoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na
ndio watakaofanya uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba mpya kwa kura ya maoni.
Wananchi pia walipata nafasi ya kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya yaliyojadili Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Pia walipata nafasi ya
kutoa maoni yao kupitia Mabaraza ya Katiba ya taasisi. Katika Bunge hili
wapo wananchi 201 kutoka makundi
mbalimbali.
Katika
mchakato wa kutunga Katiba za mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo Tume za Kuandaa
Rasimu na Bunge Maalum la Katiba kama ilivyo katika mchakato huu. Hata
hivyo, kwa Katiba zilizopita Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pekee ndio
waliounda Bunge Maalum. Safari hii Bunge Maalum linajumuisha Wabunge,
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi 201 wanaotoka kwenye jamii,
wakiwakilisha asasi na makundi mbalimbali ya Watanzania kutoka Zanzibar na
Tanzania Bara. Mchakato wa sasa utaishia kwenye kura ya maoni
itakayoshirikisha wananchi wote wa Tanzania wanaoruhusiwa kupiga kura.
Michakato iliyopita iliishia Bunge Maalum pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tangu
kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili, 1977, mpaka sasa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko takriban mara 14. Mabadiliko
hayo yalitokana na kufanyika au kutokea kwa mabadiliko muhimu ya kiuchumi,
kisiasa na kijamii katika nyakati mbalimbali hapa nchini na katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Kwa
ruksa yako naomba nitaje baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:-
1. Mabadiliko
ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa Mahakama ya
Rufani ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki
mwaka 1977.
2. Mabadiliko
ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya Zanzibar, hivyo
kulazimu Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
3. Mabadiliko
ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa vipindi vya Urais ambao haukuwepo
kabla ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za Binadamu (Bill of Rights)
yaliingizwa kwa mara ya kwanza katika Katiba. Vilevile, Mahakama ya
Rufani ya Tanzania na mambo mengine ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki
yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
4. Mwaka
1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa
badala ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia utaratibu wa
uchaguzi wa Rais na Wabunge ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa vyama vingi
vya siasa. Vilevile utaratibu wa kuwa na viti maalum vya wanawake katika
Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia 15 ya Wabunge wote.
Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Bunge
lilipewa mamlaka ya kumwajibisha Rais na Waziri Mkuu kupitia kura ya kutokuwa
na imani.
5. Mabadiliko
ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais kupitia Mgombea
Mwenza.
6. Mwaka
2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika mabadiliko yaliyopanua wigo
wa Haki za Binadamu na kuongeza uwakilishi wa wanawake.
Umuhimu wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kufanyika
kwa mabadiliko hayo kunathibitisha utayari wa Serikali kufanya mabadiliko kila
ilipoonekana inafaa kufanya hivyo. Pamoja na kufanya yote hayo na
Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo na madai yaliyokuwa yanajirudia ya
kutaka Katiba ya Tanzania iandikwe upya. Wako watu walioimithilisha
Katiba yetu na nguo yenye viraka vingi mno kiasi kwamba ingefaa kununua mpya
badala ya kuendelea kuivaa.
Madai
ya kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi
vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai Katiba mpya kwa imani, eti kwamba,
itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo tu, hata katika mchakato wa
Serikali zetu mbili kushughulikia kero za Muungano, imedhihirika kuwa baadhi ya
changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya Katiba ili kuzipatia ufumbuzi wa
uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
kutambua ukweli huo na baada ya kushauriana na kukubaliana na viongozi wenzangu
wakuu wa Chama tawala na Serikali zetu mbili wakati ule, ndipo tarehe 31
Desemba, 2010, nikatangaza dhamira ya kuanzisha mchakato wa kutunga Katiba
mpya. Nilieleza siku ile kuwa katika mchakato huo tutakuwa na
ushirikishwaji mpana wa wananchi wa Tanzania kwa makundi yao ya jinsia, dini,
siasa na shughuli wazifanyazo kujipatia riziki na kwa maeneo wanayotoka katika
pande zetu mbili za Muungano.
Mchakato wa Katiba Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tarehe 16 Machi, 2011
Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya
kuliongoza taifa katika mchakato wa kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu
wa Sheria hiyo, mchakato wa kutunga Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa kuunda Tume
ya Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza maoni ya
wananchi mmoja mmoja na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao na kupitia
Mabaraza ya Katiba. Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya Katiba
mpya itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kujadiliwa na Katiba mpya kutungwa.
Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa wananchi kupiga kura ya maoni ya kuamua
kama wanaikubali au kuikataa Katiba mpya.
Tarehe 6 Aprili, 2012
nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuwaapisha
tarehe 13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi tarehe 2 Mei, 2012 na
kuikamilisha kwa mafanikio, hatua zote zilizoihusu na kukabidhi kwangu na kwa
Rais wa Zanzibar, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba,
2013. Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Joseph Warioba kuwasilisha
Rasimu hiyo mbele ya Bunge hili tukufu tarehe 18 Machi, 2014, kinahitimisha
rasmi kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi inayofuatia ni ya Bunge
hili kujadili, kuamua na kutunga Katiba mpya. Baada ya hapo Katiba mpya
itafikishwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga kura ya NDIYO
au HAPANA.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Rasimu ya Katiba
ilichapishwa kwenye gazeti la Serikali na magazeti mengine yanayosomwa na
wananchi kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba viliwekwa
wazi kwenye tovuti ya Tume kwa kila mtu kusoma. Inafurahisha kuona kuwa
watu wengi wameisoma Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba na kumekuwa na mjadala
mpana kuhusu nyaraka zote hizo muhimu. Watu wengi wametoa maoni yao na
wanaendelea kufanya hivyo. Kwa maoni yangu hili ni jambo jema sana na ni
kielelezo thabiti kuwa demokrasia imestawi na inazidi kuota mizizi
Tanzania. Pia, kwamba, Watanzania wako huru kushiriki na kutoa maoni yao
kwa mambo yanayowahusu.
Pongezi kwa Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa mara nyingine
tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba akisaidiwa na Mheshimiwa
Jaji Augustino Ramadhani, kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Kazi yao haikuwa
rahisi hasa ukizingatia ukubwa wa nchi yetu, wingi wa watu wake, utitiri wa
taasisi na pigo la kumpoteza Mjumbe mwenzao muhimu Dkt. Sengondo Mvungi
aliyetangulia mbele ya haki katikati ya mchakato.
Pamoja na hayo, kwa
bidii kubwa Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote nchini na kuwafikia
watu 351,644 waliotoa maoni yao
kwa mdomo na kwa maandishi. Halikadhalika, walipokea na kuchambua maoni 772,211 kutoka kwa wananchi na taasisi
mbalimbali. Baada ya kupokea maoni ya wananchi, kufanya utafiti na kwa
kutumia maarifa na uzoefu wao, Wajumbe wakafanya kazi ngumu, kuliko yote, ya
kutengeneza Rasimu ya Katiba iliyoko mbele ya Bunge hili. Ni kweli kwamba
Wajumbe hawakuweza kuwafikia wananchi wote wa Tanzania, lakini wameweza
kuwafikia wananchi wengi, ambao kwa kiasi kikubwa wanawakilisha taswira na
mitazamo mipana ya jamii yetu.
Baadhi ya Masuala Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa
Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imefanya kazi
nzuri, yenye thamani kubwa na ya manufaa kwa taifa la Tanzania. Rasimu
imeandikwa vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume imetoa mapendekezo
ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha Katiba ya nchi yetu, kwa namna
ya pekee. Katiba inayopendekezwa, imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya
yanayokwenda vyema na wakati tulionao na kuweka msingi mzuri kwa huko mbele
tuendako. Kwa taratibu za kawaida za marekebisho ya Katiba tuliyonayo,
isingekuwa rahisi kuingiza mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa
kilichosheheni mambo mengi. Kina kurasa 106, sura 17 na
ibara 271. Wajumbe wa
Bunge hili mnatakiwa kusoma na kuelewa vizuri kila kilichoandikwa ili muweze
kufanya uamuzi ulio sahihi. Mnawajibika kuchambua kwa kina na umakini
mkubwa kila kilichomo, sura kwa sura, ibara kwa ibara, sentensi kwa sentensi na
hata neno kwa neno. Hamna budi kujiridhisha kuhusu uandishi wa vifungu
vya Rasimu ya Katiba na kufaa kwa dhana mbalimbali zilizoingizwa na
kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kile ambacho Wajumbe
mtaona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au kufutwa msisite kufanya hivyo
ili Watanzania wapate Katiba iliyo bora. Msipofanya hivyo kuna hatari ya
kupata Katiba ambayo ni ngumu kuitekeleza. Aidha, tunaweza kuwa na Katiba
ambayo itanung’unikiwa na watu wengi na kusababisha madai ya kutaka ifanyiwe
marekebisho muda mfupi baada ya kupitishwa. Bunge hili linao wajibu
maalum wa kuzuia balaa hilo lisitokee katika nchi yetu. Ngazi mbalimbali
zilizowekwa katika mchakato huu ni kama chujio la kuepusha hali hiyo
isitokee. Kile ambacho hakikuonekana katika hatua moja kitaonekana katika
hatua inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo muitumie
vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza kuwa moja ya jambo
mnalotegemewa kufanya ninyi wenzetu mliopewa dhamana ya kutunga Katiba ya nchi
yetu ni kujiridhisha na uandishi wake. Yapo maoni yaliyotolewa kuhusu
uandishi ambayo naomba myatafakari na kuamua ipasavyo. Kwa mfano, kuna
baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi mno
kuliko inavyostahili Katiba kuwa (too prescriptive). Pia kuna mawazo
kwamba baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa katika Katiba bali yawe kwenye Sheria
zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako mambo
yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu hatakwenda
mahakamani kuidai Serikali impatie (non justiciable). Mambo yaliyotajwa
kwenye Katiba ni mazuri na yanavutia, lakini lazima yaendane na uwezo wa nchi
na uchumi wake kuhimili. Simaanishi kwamba tuyatoe kwenye Katiba, bali
yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi utakaporuhusu yatekelezwe.
Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali kujikuta inalaumiwa au hata
kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai ya jambo moja au jingine
ambayo haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo kama hayo muyatazame ili
tusije kuwa na Katiba ambayo ni ngumu kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Yapo pia maoni kuwa
baadhi ya vifungu vina upungufu katika uandishi wake, hivyo kuhitaji kufanyiwa
marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza kuwepo athari na nyingine
zinaweza kuwa mbaya. Kwa mfano, Ibara ya 2 ya Rasimu inayotambulisha eneo
na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo inasomeka kuwa “Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la
Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari”.
Maelezo hayo yameacha
kutambua, kwa upande wa Tanzania Bara, sehemu yetu ya maziwa na mito ambayo ni
kubwa sana. Kwa nini tuache kuitaja? Je hatutoi nafasi kwa nchi
tunazopakana nazo siku moja wakaja kupora sehemu zetu hizo na sisi kukosa
utetezi kwa kuwa hata Katiba yetu haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni yetu?
Hili ni jambo kubwa ambalo Bunge hili lazima mlirekebishe. Wakati
ndiyo huu hakuna mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo jingine kuhusu uandishi ni
mgongano kati ya pendekezo la msingi la Tume la kuwa na muundo wa Serikali tatu
na majukumu ya Serikali ya Muungano ambayo kimsingi ni majukumu ya Serikali za
nchi washirika. Katika Rasimu hii malengo ya taifa yameainishwa na
Serikali ya Muungano inatakiwa kuhakikisha kuwa malengo hayo yanatekelezwa na
itoe taarifa Bungeni. Katika mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa na
Tume masuala yahusuyo uchumi na maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo,
ufugaji, uvuvi, viwanda, biashara, pembejeo, elimu, hifadhi ya jamii na
kadhalika yako chini ya mamlaka ya Serikali za nchi washirika. Mamlaka ya
Serikali ya Muungano ni kwa mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na Mamlaka ya
Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na
Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru
wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Kwa Rasimu
kupendekeza muundo wa Serikali tatu na kuipa Serikali ya Muungano majukumu
ambayo haina mamlaka nayo, ni kuzusha utata na migongano kati ya Serikali ya
Muungano na nchi washirika. Mkichagua mfumo wa Serikali tatu, inawalazimu
muyaondoe mambo hayo kwani Serikali ya Muungano haistahili kuyatekeleza na wala
haina uwezo wa kuweka masharti kwa Serikali za nchi washirika kwa mambo yaliyo
kwenye mamlaka ya nchi hizo. Lakini kama mtaamua tuendelee na muundo wa
Serikali mbili, mambo haya mazuri yanatekelezeka na Serikali ya Muungano bila
ya matatizo. Katika uandishi wa Rasimu Utumishi katika Serikali ya
Muungano haumo katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Ni lazima liwemo.
Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo uandishi katika Rasimu. Naamini
mkiisoma Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua mengineyo.
Dhana Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu kuna
dhana mpya na mambo mapya kadhaa yaliyoingizwa ambayo yanabadili utaratibu wa
sasa wa uendeshaji wa nchi na mambo mbalimbali. Nawaomba mfanye uchambuzi
wa kina kwa kila kinachopendekezwa na kujiridhisha kuhusu kufaa kwake na
manufaa yake. Fanyeni hivyo ili tujihakikishie kuwepo kwa mambo
mazuri na uendeshaji mzuri wa shughuli katika taifa letu changa.
Mambo ni mengi na kwa
ufinyu wa muda sitaweza kuyazungumzia yote. Niruhusuni nizungumzie baadhi
ya dhana na mambo mapya yaliyomo katika Rasimu. Jambo la kwanza, kwa
mfano, linahusu Ibara ya 128 (2)(d) inayoleta dhana ya “Mbunge kupoteza Ubunge
iwapo atashindwa kufanya kazi za Mbunge kwa miezi sita mfululizo kutokana
na maradhi au kizuizi ndani ya gereza”.
Watu hawana tatizo na Mbunge kuwa
kizuizini ndani ya gereza kama amepatikana na hatia Mahakamani na kuhukumiwa
kifungo. Lakini, isijekuwa yuko rumande kwa tuhuma akisubiri kesi
kusikilizwa. Je akija kuonekana hana hatia na kuachiliwa? Naungana
na wale wanaoshauri kuwa jambo hili lifafanuliwe vizuri na kutambua Mbunge
kutiwa hatiani na kupata adhabu ya kifungo cha kipindi hicho.
Ni bora ifanyike hivyo sasa ili kuondoa mikanganyiko. Hakuna
haja ya kusubiri mpaka jambo hili lije kufafanuliwa baadaye kwa
Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande wa mtu
kupoteza Ubunge kwa sababu ya “kuugua
kwa miezi sita mfululizo” ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili
ambao haustahili kufanywa na Katiba. Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati
mwingine Mbunge anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake.
Anaweza kuugua kwa miezi sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi chake cha
Ubunge kufika mwisho. Kwa nini awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba
ya mwaka 1977 tunayotumia sasa haina sharti hilo. Watu wanauliza hoja na
haja ya kuwa na sharti hili kwenye Katiba mpya ni ipi? Wanasema kwa kweli
anachostahili Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake iimarike ili aendelee
kutumikia watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake. Tusiwatie watu
kishawishi cha kukatiza matibabu ili kukwepa sharti hilo. Ni vyema jambo
hili mkalitazama kwa makini, na muone kama linastahili kuwepo au hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu hii
imeingizwa dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa Wabunge. Tena
mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu mfululizo au la!. Jambo hilo
limezua mjadala motomoto katika jamii. Ni vizuri mkajiridhisha juu ya
sababu za msingi na manufaa ya kufanya hivyo hapa Tanzania. Mazoea yetu
na ya kwingineko duniani ni kuweka ukomo kwa Wakuu wa Nchi kwa sababu nzuri na
rahisi kuzielezea. Lakini, kuwawekea ukomo Wabunge ni jambo jipya na huenda
Tanzania tukawa wa kwanza. Nashawishika
kuungana na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema mno kuanzisha utaratibu
huo hapa kwetu.
Nachelea kuwa tutainyima nchi yetu
fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu mzuri wa uongozi kwa nafasi ya
Ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa bila ya sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine jipya
linalopendekezwa na Tume ni utaratibu wa kumuondoa Mbunge katikati ya kipindi
chake cha uongozi. Kwa hoja linaonekana kuwa jambo jema lakini naomba
athari zake mzitafakari vizuri. Kuna hatari ya kuanzisha misuguano kwenye
Majimbo na kuwaacha Wabunge wasifanye kazi zao kwa utulivu bali wawe wanajihami
dhidi ya wapinzani wao kuwatengenezea fitna za kuwatoa. Utaratibu
unaopendekezwa wa Chama chake kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi katika
mazingira hayo nao unaweza kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha vuguvugu la
kumuondoa Mbunge. Walioshindwa kwenye kura ya maoni wanaweza kufanya kazi
ya kuwachimba wenzao mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima faida na hasa
thamani inayoongezwa na kuanzisha utaratibu huo. Naomba tujiridhishe kama
jambo hili jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi kila miaka mitano kurudi kwa
wananchi hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo wa Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine kubwa
lililopendekezwa na Tume ambalo limevuta hisia za karibu watu wote nchini
linahusu muundo wa Muungano wetu kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za
sasa. Pendekezo hili limezua mjadala mkubwa tangu
lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza na kurudiwa katika Rasimu ya pili.
Wakati mwingine mjadala umekuwa mkali na wa hisia kali kwa kila upande.
Kwa kweli hili ndilo
jambo kubwa kuliko yote katika Rasimu kwa sababu linapendekeza kuanzishwa kwa
muundo na mfumo mpya wa kuendesha nchi yetu. Hii ndiyo agenda mama ya
Bunge hili ambayo kila Mtanzania anasubiri kwa hamu uamuzi wenu utakuwa
upi. Ombi langu kwenu ni kuwa watulivu mnapojadili suala hili.
Epukeni jazba ili mfanye uamuzi ulio sahihi. Lazima mtambue uamuzi
usiokuwa sahihi kwa jambo hili una hasara kubwa. Tunaweza kupoteza kitu
tulichokijenga kwa gharama kubwa kwa nusu karne iliyopita. Tanzania
inaweza kuwa nchi iliyojaa migogoro na matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe;
Kama alivyoeleza
Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, mara kadhaa, mjadala
au madai ya kutaka muundo wa Serikali tatu si jambo jipya. Ulikuwepo hata
wakati wa mazungumzo ya kuunganisha nchi zetu mbili mwaka 1964. Ulikuwa
kiini cha kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar mwaka 1984.
Muundo huu uliwahi kupendekezwa na Tume ya Nyalali mwaka 1992, ndiyo hoja
ya G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia na Tume ya Jaji Kisanga ya mwaka
1998. Lakini mara zote hizo mapendekezo hayo hayakukubaliwa.
Waasisi wa taifa
letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya
Tanganyika wakati ule na Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar wakati ule, waliamua kuchagua Muungano wa Serikali
mbili tulionao sasa. Walitoa sababu mbili kuu: “ni muundo unaoihakikishia Zanzibar kuwa
haimezwi na Tanganyika; na pia unaiepusha Tanganyika kubeba mzigo mkubwa wa
kugharamia Serikali ya Tanganyika na ile ya Muungano”.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Natambua kuwepo kwa
rai ya kutaka Mwalimu Nyerere asitumiwe katika mjadala huu. Nionavyo mimi
ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume katika
jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo kujadili na kukubaliana kuwa mfumo wa
Serikali mbili ndiyo bora kwa nchi yetu. Iweje leo tunapozungumzia
kuubadili, mawazo yao yawe hayafai kutumika au hata kuzungumzwa. Hivi
hasa mawazo ya nani pekee ndiyo bora zaidi kutumika? Tutakuwa
hatuutendei haki mjadala huu na sisi wenyewe tunaoshiriki katika mchakato
huu. Rai yangu kwenu ni kuwa mzitazame hoja zote kwa marefu na mapana
yake ili mpime kama zipo sababu za kuubadili muundo wa sasa wa Muungano wa
Serikali mbili na kuleta wa Serikali tatu. Na, kama zipo mabadiliko hayo
yaweje! Lazima mfanye uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye mashiko. (you must make an informed decision).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imetoa sababu
mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu. Sababu ya kwanza ni
kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote Zanzibar na Tanzania Bara.
Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania waliotoa maoni, yaani asilimia 60.2 wa kutoka Zanzibar
wanaunga mkono muundo wa Serikali ya Mkataba, na asilimia 61.3 wa kutoka
Tanzania Bara wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu. Sababu ya pili ni
kwamba muundo huo unatoa majawabu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za
muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazonung’unikiwa na watu wa pande zetu mbili
za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sababu hizi mbili kuu
zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii. Wapo wanaokubaliana na
Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema Tume imesema kweli
kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu, hivyo muundo wa
Serikali tatu hauepukiki. Ndiyo matakwa ya wengi hivyo msemo wa Kiswahili
usemao wengi wape uheshimiwe.
Lakini wapo wanaodai
kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo. Wanasema kuwa
taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa
Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664.
Kati yao ni wananchi 47,820 au
sawa na asilimia 13.6 ndiyo
waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa Muungano kwao
halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa. Wanahoji kuwa iweje
leo asilimia 13.6 ya Watanzania
wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanasema pia, kwamba
mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na 67), inaonesha kwamba
kati ya hao watu 47,820 waliotoa
maoni kuhusu Muungano, ni watu 17,280
tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo
waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia
29.8 walitaka Serikali mbili, asilimia
25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza Serikali moja. Hii hoja ya
Watanzania wengi kutaka Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Takwimu za Tume (uk.
57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211. Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano
bali mambo mengine. Hivyo basi wanahoji pia kwamba kama muundo wa
Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye
idadi ya watu waliotoa maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote
hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu
Muungano yalikuwa asilimia 10.4
ya maoni yote. Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania wengi
kutaka Serikali tatu uko wapi?”
Changamoto za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Kama
nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa kuhusu kufaa kwa
muundo wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu unajibu changamoto nyingi za muundo
wa Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri changamoto za muundo wa Serikali
mbili. Kwa upande wa Zanzibar wanalalamikia kile kinachoitwa Tanzania
Bara kuvaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo kutumia mamlaka ya
Serikali ya Muungano kujinufaisha yenyewe. Fursa hiyo Zanzibar
hainayo. Aidha, wanasema mipaka na mamlaka ya Serikali ya Muungano kwa
mambo ya Muungano, na kwa mambo ya Tanzania Bara haijaainishwa vizuri
ikaeleweka. Wazanzibari pia, wanazungumzia mkanganyiko kuhusu ugawanaji wa
mapato, na jinsi ya kuchangia shughuli za Muungano baina ya Serikali ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia
Rais wa Zanzibar kuondolewa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Aidha, kuna malalamiko kuwa orodha ya
mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka mambo 11 mwaka 1964 mpaka 22 mwaka
1992 imepunguza uhuru wa
Zanzibar kwa mambo yake ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande wa
Tanzania Bara, Tume inaeleza kuwepo kwa manung’uniko kuwa Muungano wa Serikali
mbili umepoteza utambulisho wa kihistoria wa Tanganyika na fursa ya watu wa
upande wa Tanzania Bara kutetea maslahi yao ndani ya Muungano. Wanasema
Zanzibar sasa imekuwa nchi huru; ina bendera yake, wimbo wake wa taifa na
Serikali yake. Aidha, wanasema Zanzibar imebadili Katiba na kujitambulisha kama
nchi na kuchukua madaraka ya Bunge la Muungano, kwa vile Sheria zinazotungwa na
Bunge lazima zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi kupata kibali cha kutumika
Zanzibar. Wananchi wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na haki ya
kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki hiyo
Tanzania Bara. Na wao vilevile wananung’unikia mkanganyiko kuhusu ugawaji
wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za Muungano
baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hizi ndizo baadhi
ya changamoto ambazo Tume inaona jawabu lake ili kuzitanzua ni kubadili muundo
wa Muungano kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa.
Faida za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imefafanua kwamba mfumo wa Serikali tatu utagawanya vizuri madaraka kati
ya mamlaka tatu za Muungano. Unawezesha Washirika wa Muungano kubaki na
utambulisho wao wa kihistoria na kiutamaduni na hivyo, utawezesha kuondoa hisia
za Zanzibar kumezwa na Muungano. Pia unawezesha kila upande wa Tanzania
kuendesha mambo yake yasiyo ya Muungano kadri wanavyoona inafaa. Vile vile
unaweza ukaleta ushindani wa kimaendeleo baina ya washirika na hivyo kusaidia
kukuza maendeleo ya nchi.
Faida za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na kuainisha
changamoto za muundo wa Serikali mbili na kupendekeza kuwa muundo wa Serikali
tatu ndio utakaosaidia kuzitatua, Tume haikuacha kutambua manufaa na mchango
muhimu uliotolewa na muundo wa Serikali mbili kwa nchi yetu. Tume inasema
kuwa muundo wa Serikali mbili unapunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za
umma. Umesaidia kujenga uhusiano na ushirikiano mzuri katika nyanja mbalimbali
baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano. Umezuia mkubwa kummeza
mdogo; na umedumisha Muungano mpaka kuufikisha hapa ulipo tangu kuasisiwa kwake
takriban miaka 50 iliyopita (1964). Aidha, umesaidia kudumisha amani,
umoja na utulivu hapa nchini.
Changamoto za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na kuelezea ubora wa muundo wa
Serikali tatu kama jawabu kwa changamoto za Serikali mbili, Tume inakiri kuwa
hata muundo huu nao una changamoto zake. Kwanza kabisa, Taarifa ya Tume
inaeleza kuwa kutakuwa na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za
umma. Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba alitutoa hofu kuhusu gharama
ingawaje mwaka 1993, Mwalimu alikuwa na mawazo tofauti. Alisema kwamba: “watu …wanaodhani kuwa
gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa ndogo, (Waulizeni
Wazanzibari) na wala gharama ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo
hata bila gharama ya mambo yasiyo ya Shirikisho”. Ni matumaini yangu
kwamba katika mjadala wenu mtajipa nafasi ya kulitafakari suala hili kubwa na
nyeti.
Tume imesema pia
kwamba, Muundo huu, unaweza kuibua tatizo la uchangiaji wa gharama za
uendeshaji wa shughuli za umma baina ya nchi washirika. Vilevile, kuna
uwezekano wa kuwepo sera zinazokinzana au kutofautiana juu ya masuala ya msingi
ya nchi na kuzua mgogoro kati ya washirika wa Muungano na baina ya nchi
washirika na Serikali ya Muungano. Aidha, upo uwezekano mkubwa kwa muundo huu
kuleta tofauti za kimaendeleo baina ya pande mbili za Muungano kutokana na kila
upande kuwa na sera na mipango tofauti.
Tume pia imeelezea
hatari ya muundo wa Serikali tatu kukuza hisia za utaifa (nationalistic
feelings) kwa nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha Muungano.
Muundo huu pia unaweza kuleta misuguano (paralysis and deadklocs in decision
making) katika kufanya uamuzi juu ya masuala muhimu ya kitaifa.
Changamoto hizo si tu zinaweza kuwa tishio kwa ustawi wa Muungano bali pia hata
uhai wake. Kwa ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali tatu kuna maana ya
kufanya kazi ya ziada ya kuzikabili changamoto hizi ili zisiue Muungano
wenyewe. Changamoto ambazo si ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanaounga mkono muundo wa Serikali
mbili wanasema kuwa kwa mlolongo huu wa changamoto zilizoainishwa na Tume
yenyewe, unadhihirisha kuwa muundo wa Serikali tatu hautapunguza matatizo ya
Muungano wetu bali utayaongeza maradufu kuliko ilivyo sasa. Wanakiri
kuwepo kwa changamoto katika muundo wa sasa wa Muungano. Hata hivyo, wanaamini
zinaweza kushugulikiwa na kupatiwa ufumbuzi bila ya kuhitaji kuwa na Serikali
ya tatu. Wanatoa mifano kadhaa ya jinsi Serikali zetu zilivyoshughulikia
changamoto za Muungano katika kipindi cha uhai wake na mafanikio
yaliyopatikana.
Katika kushughulikia
kero za Muungano, Serikali zetu mbili ziliunda Tume ya Shelukindo mwaka 1992 na
Kamati ya Pamoja ya Serikali zetu mbili mwaka 1993. Mambo mengi yaliyoainishwa
katika Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja yameshughulikiwa na kupatiwa
ufumbuzi. Kwa upande wa kero zilizoelezwa kwenye Tume ya Shelukindo,
ilipofikia mwaka 2006 yalikuwa yamebakia mambo 13 kati ya 31. Kwa
jumla, kwa kero zilizoibuliwa na Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja, hivi
sasa yamesalia mambo sita
tu. Kimsingi ni mambo yahusuyo maslahi ya kiuchumi na yote yapo katika
hatua nzuri za kuyamaliza. Mambo hayo ni:
1. Mgawanyo
wa mapato:
(a) Hisa
za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki
(b) Mgawanyo
wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
2. Utafutaji
na uchimbaji mafuta na gesi asili.
3. Ushirikiano
wa Zanzibar na taasisi za nje.
4. Ajira
kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.
5. Usajili
wa vyombo vya moto.
6. Tume
ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali zetu mbili
zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato huu wa mabadiliko ya Katiba
kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Mambo hayo ni matatu yafuatayo:
1. Utafutaji
na uchimbaji mafuta na gesi asili.
2. Ushirikiano
wa Zanzibar na taasisi za nje.
3. Tume
ya Pamoja ya Fedha.
Matatu mengine yatamalizwa kwa kutumia
taratibu za kiutawala. Hali kadhalika, katika kipindi cha mpito
kinachopendekezwa na Tume yaani 2015 – 2018 ni nafasi nzuri ya kushughulikia
masuala yenye migongano kati ya Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya
Muungano. Mimi naishi kwa matumaini na kwa vile tunayo dhamira njema ya
kuimarisha Muungano wetu, naamini tutaweza kuziondoa tofauti zilizopo.
Orodha ya Mambo ya Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kuhusu orodha ya
mambo ya Muungano kuwa 22 badala
ya 11 ya awali, napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
hazina kigugumizi wala upungufu wa dhamira ya kisiasa ya kuyapunguza yale yanayopunguzika.
Napenda kwanza kabisa, ieleweke kuwa kilichoongeza orodha hiyo si hila za
Serikali ya Muungano kutaka kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa mambo yake ya
ndani. Na, wala siyo udhaifu wa viongozi wa Zanzibar katika kutetea
maslahi ya nchi yao. La hasha.
Pili, naomba ieleweke
kuwa, kila kilichoongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano kilikuwa na sababu
inayoeleweka, inayoelezeka na iliyokubalika na pande zote mbili za
Muungano. Hakuna hata jambo moja lililoingizwa kwenye Katiba kwa
kificho. Taratibu stahiki za kikatiba na kisheria zilifuatwa. Hoja
ziliwasilishwa Bungeni na kujadiliwa kwa uwazi na uamuzi ulifanywa na Bunge kwa
kuzingatia kanuni ya theluthi mbili ya kura za kila upande wa Muungano.
Kumbukumbu zipo katika Hansard za Bunge la Muungano, ambazo ziko wazi kwa kila
mtu anayetaka kuzisoma asome. Nashauri mkazisome ili mpate kujua ukweli
na undani wa kila kilichoongezwa na sababu za kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nchi zetu mbili zilipoungana mwaka 1964
na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kulikuwa na mambo 11 kwenye Orodha ya Mambo ya
Muungano. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
1. Katiba ya Jamhuri ya
Muungano,
2. Mambo ya Nje,
3. Ulinzi,
4. Polisi,
5. Hali ya Hatari,
6. Uraia,
7. Uhamiaji,
8. Biashara ya nje na
mikopo,
9. Utumishi katika
Serikali ya Muungano,
10. Kodi ya Mapato, Kodi ya Makampuni,
Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
11. Bandari, Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kati ya mwaka 1965 na
1992 mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka 11 hadi kufikia 22,
kimsingi kutokana na mambo mbalimbali yaliyotokea nchini na kwenye ukanda wetu
wa Afrika Mashariki. Pande zetu mbili za Muungano zilikubaliana
kuwa mambo hayo yaongezwe katika Katiba na taratibu za kisheria na Kikatiba
zilifuatwa. Kwa idhini yako naomba nitoe maelezo kwa ufupi kwa yale
yaliyoongezwa na kitu kilichosababisha mabadiliko hayo kufanywa.
1. Jambo la kwanza
kuongezwa, yaani la 12 lilikuwa
ni “sarafu, mabenki na fedha za kigeni”. Hii ilifanyika tarehe 10 Juni,
1965 kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African
Currency Board) mwaka 1964. Kwa ajili hiyo, kila nchi mwanachama wa
Jumuiya ililazimika kuwa na sarafu yake na mipango yake ya kusimamia mambo yake
ya kibenki na fedha. Serikali zetu mbili zilikubaliana masuala hayo
yashughulikiwe na Serikali ya Muungano na Muswada husika wa Bunge uliidhinishwa
kuwa Sheria na Mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa akikaimu Urais tarehe 10 Juni,
1965.
2. Tarehe 11 Agosti,
1967 yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano:-
(a) Leseni za Viwanda na Takwimu,
(Jambo la 13)
(b) Elimu ya Juu, (Jambo la 14)
(c) Jambo la 15 lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya 10 ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Nyongeza hiyo ilikuwa na mambo 27 ambayo Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la uratibu.
Mambo hayo ni pamoja na Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, Utabiri wa Hali
ya Hewa, Utafiti, Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli, Barabara,
Usafiri wa Majini na kadhalika.
3. Tarehe 22
Julai, 1968 “rasilimali ya mafuta, petroli na gesi asilia” iliongezwa kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa jambo la 16. Kimsingi Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la kuagiza
mafuta ya petroli na gesi asilia kwa ajili ya nchi nzima. Baada ya
kupanga upya Orodha ya Mambo ya Muungano, suala la rasilimali ya mafuta likawa
la 15.
4. Tarehe 22 Novemba,
1973 Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na kuwa jambo la 16. Hii ilifuatia kuvunjika kwa
Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki mwaka 1971 na hivyo nchi yetu kulazimika
kuunda Baraza la Mitihani la Taifa mwaka 1973.
5. Mwaka 1984
yalipofanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya mwaka 1977, Orodha ya Mambo
ya Muungano ilipangwa upya. Mambo yaliyokuwemo kwenye Nyongeza ya 10 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kuorodheshwa kama Jambo la 15
katika Orodha ya Mambo ya Muungano yalipunguzwa na kubaki matano. Mambo hayo yalipewa
namba kama ifatavyo:- Usafirishaji wa Anga kuwa Jambo la 17, Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa la 19 na Takwimu kuwa la 20 na Mahakama ya Rufani ya
Tanzania ikawa jambo la 21.
6. Tarehe 17 Mei, 1992
likaongezwa jambo la “Uandikishaji wa Vyama vya Siasa” na kuwa jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa
Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa na hasa uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Bila ya shaka maelezo haya yatasaidia
kuelezea nini kimeongezwa na mazingira ya kuongezwa kwake ni yepi.
Kulikuwepo na sababu za msingi na wala siyo hila ya namna yo yote ile
iliyofanywa na mtu ye yote mwenye nia mbaya na Zanzibar. Kama tulivyoona
mambo mengi yalihusu kilichokuwa kinatokea ndani ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Kila yalipotokea mabadiliko katika uendeshaji wa shughuli za
Jumuiya ya Afrika Mashariki, huduma zilizokuwa zikitolewa na Jumuiya
zilikabidhiwa Serikali ya Muungano kubeba kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa
kiuchumi. Yale yaliyokuwa yanagusa sehemu zetu mbili za Muungano
yaliingizwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Mengineyo yaliachiwa kila
upande kushughulikia ilivyoona inafaa. Kwa maana hii basi, mambo ambayo
yalitokana na uamuzi wetu wenyewe ni mawili tu. Mambo hayo ni
rasimali ya mafuta na gesi asilia (1968), na uandikishaji wa vyama
vya siasa (1992).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni msimamo wa
Serikali zetu mbili, tangu mwanzo mpaka leo kwamba, iwapo Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar imeshajenga uwezo wake wa kufanya baadhi ya mambo katika Orodha ya
Mambo ya Muungano ipewe uhuru wa kufanya hivyo. Lililo muhimu ni kuwa
zisiondolewe tunu zenyewe za Muungano wetu. Ndiyo maana, mambo kama vile
bandari, takwimu, kodi ya mapato, leseni za biashara, utafiti na mengineyo,
yanasimamiwa na kuendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na
kuwemo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Imekuwa hivyo kwa miaka kadhaa
sasa na imethibitika kuwa Zanzibar inayamudu. Ni makusudio yetu kutumia
fursa ya mchakato huu sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na mengineyo
tutakayokubaliana kutoka kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa ajili hiyo
tumekubaliana kuliondoa suala la rasilimali ya mafuta na gesi asilia lisiwe
jambo la Muungano. Jambo hili tulishakubaliana tangu wakati wa Rais Amani
Abeid Karume tuliondoe na hata alipokuja Rais Shein msimamo
haukubadilika. Kilichotuchelewesha kutekeleza ni kuibuka kwa fikra za
kuwa na mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona kuwasilisha Bungeni Muswada wa
Sheria wa kuondoa jambo hili katikati ya mchakato huu, ingeweza kuzua matatizo
yasiyokuwa ya lazima. Tungeulizwa haraka ni ya nini tungeweza kukosa
majibu.
Hatimaye wakati wake
wa kulimaliza suala hili sasa umefika. Misemo ya wahenga ya “subira
yavuta heri” na “kawia ufike” imetuongoza vyema tumefika mahali tunaweza
kufanya hivyo. Zipo sababu mbili zilizotushawishi kuamua kuitoa rasilimali hii
kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Kwanza kwamba, siku hizi Serikali
haiagizi mafuta. Kazi hiyo hufanywa na makampuni binafsi. Pili,
kwamba, rasilimali ya mafuta na gesi yakipatikana Zanzibar ni suala la kiuchumi
ambalo lipo kwenye mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo karafuu, hiliki, mwani na
kadhalika. Au kama ilivyo dhahabu, gesi, pamba, kahawa na kadhalika kwa
upande wa Tanzania Bara. Hivyo, Zanzibar iachwe kumiliki rasilimali yake
ya kiuchumi.
Zanzibar na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine muhimu
ambalo Serikali zetu mbili zimelizungumza na kukubaliana tulitafutie ufumbuzi
ni kuhusu Zanzibar kupata fursa ya kujiunga na mashirika ya kimataifa, kukopa
na kupata misaada kutoka nchi za nje bila kizuizi. Kwa sasa fursa hiyo
ina vikwazo vya namna mbalimbali. Ni ukweli usiopingika kuwa jambo hili
limechangia kwa kiasi kikubwa kujenga hisia hasi kuhusu Muungano kwa upande wa
Zanzibar. Aidha, limechangia sana kuchafua hali ya hewa ya kisiasa
Zanzibar kwa nyakati mbalimbali. Hata zile kauli kwamba Tanzania Bara
imejificha kwenye koti la Serikali ya Muungano, na kutaka itoke ionekane ili
iache kunufaika isivyostahili, zinazochangiwa sana na mazingira haya iliyonayo
Zanzibar. Serikali zetu mbili zinaamini kuwa mambo haya yakipatiwa ufumbuzi
tutakuwa tumeondoa kizingiti kikubwa katika ustawi wa Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tumekubaliana kuwa, tutumie fursa
za mchakato huu kuyamaliza mambo haya yaishe! Bahati nzuri dhana iliyopo
katika Ibara ya 65(2) ya Rasimu inatoa jawabu mwafaka kwa tatizo hili.
Tukikubaliana, itaipa Zanzibar “uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano na
ushirikiano na jumuiya au taasisi yo yote ya kikanda na kimataifa kwa mambo
yaliyo chini ya mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi” bila kizuizi. Ni
maoni ya Serikali zetu mbili kuwa fursa hiyo inaweza kutolewa kwa
Zanzibar bila ya kulazimika kuwa na muundo wa Serikali tatu. Hatuuoni
ulazima huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa maoni yangu kitu
kingine muhimu cha kufanya ni kuongeza msukumo, utakaohakikisha kuwa Tume ya
Pamoja ya Fedha inatimiza ipasavyo majukumu yake. Wanaohusika na
utekelezaji wa maamuzi yake wabanwe ipasavyo kutimiza wajibu wao. Iwekwe
mifumo na masharti katika sheria au Katiba ya kuwabana watekelezaji kwa ajili
hiyo. Hali kadhalika ihakikishwe kuwa, Akaunti ya Pamoja inaanzishwa bila
ajizi na kutumika na pande zote. Aidha, mfumo wa mawasiliano na
ushirikiano baina ya Serikali zetu mbili yaani Kamati ya Pamoja ya Serikali ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya kisheria na kama
hapana budi upewe nguvu ya Kikatiba. Tukifanya hivyo tutafanikiwa
kuyaweka mambo yote sawa hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Katika mjadala kuhusu
mapendekezo ya kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali tatu, wananchi wametoa
maoni na mapendekezo mengi mazuri kuhusu changamoto za Serikali tatu
zilizoainishwa na Tume na namna ya kuzitatua. Tena yapo maoni ya watu
wanaopenda muundo wa Serikali tatu na wasiopenda muundo wa Serikali
tatu. Nawaomba myatafakari kwa uzito unaostahili. Yapo mambo muhimu
ya kuyatafutia ufumbuzi. Kwanza, kwa mfano ni ile hoja kwamba Serikali ya
Muungano inayopendekezwa haikujengeka kwenye msingi imara. Haina nguvu yake
yenyewe za kusimama. Inategemea mno ihsani ya nchi washirika. Kwa
sababu hiyo inaweza kuanguka wakati wowote, na Muungano kusambaratika, iwapo
itakosa ihsani ya nchi washirika. Tena inaweza kuwa hivyo hata kama ni
mmoja wa washirika amefanya hivyo.
Pili, kwamba,
haielekei Serikali hiyo ina chanzo cha uhakika cha mapato ya kuiwezesha
kusimama yenyewe na kutekeleza majukumu yake. Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa
unatiliwa shaka kuwa hautatosheleza mahitaji. Pia, kwamba, hakuna uhakika
wa fedha hizo kupatikana kwa vile, Serikali ya Muungano haina chombo chake
chenyewe cha kukusanya mapato hayo. Itategemea vyombo vya nchi washirika
kuikusanyia na kuipelekea. Kuna hatari ya shughuli za Serikali ya
Muungano kusimama wakati wo wote au hata kusimama kabisa kwa sababu ya nchi
washirika kuchelewa au kushindwa kuwasilisha makusanyo ya kutoka kwao.
Bahati mbaya Serikali
ya Muungano haina uwezo wala nyenzo za kuhakikisha kuwa mapato yake
yanawasilishwa. Serikali hiyo haina mamlaka ya kuzibana nchi washirika
kuwasilisha au kuziwajibisha zisipofanya hivyo. Katika mazingira hayo ni
rahisi kwa Serikali ya Muungano kukwama na kushindwa kutekeleza majukumu
yake. Huu ni muundo ambao inakuwa ni rahisi sana kwa Muungano
kuvunjika.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu ya
Katiba, Serikali ya Muungano inapewa fursa ya kukopa kama chanzo cha kujipatia
mapato ya kuendesha shughuli zake. Lakini, kwa sababu ya kukosa
rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa vigumu kwa Serikali hiyo kukopesheka. Kwa
jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake hauna nguvu iliyo thabiti, na watu
wengine wanaona kama vile ukuu huo haupo kabisa. Akitokea kiongozi ye
yote wa nchi washirika akatunisha misuli dhidi ya Rais wa Muungano au kupinga
maamuzi ya Serikali au chombo cha Muungano, Rais na Serikali yake watakuwa
hawana lo lote la kufanya. Kwa kweli uhai wa Muungano katika muundo wa
Serikali tatu ni wa mashaka makubwa.
Hofu hizi kuhusu
udhaifu wa Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa,
zinawasumbua hata wale wanaopendelea mfumo wa Serikali tatu kuwepo. Wao
wangependa iwepo Serikali ya Muungano yenye nguvu na inayoweza kusimama yenyewe
kwa kujitegemea. Wanaona kilichopendekezwa hakitoi matumaini hayo.
Hii ina maana kuwa lazima mawazo bora zaidi yatolewe ili kupata Serikali ya
tatu yenye ukuu unaoonekana na inayoweza kusimama yenyewe bila kuwa tegemezi na
egemezi kwa nchi washirika. Pia inaweza kuwa nguzo ya kutegemewa na nchi
washirika. Bila ya shaka Bunge hili likiamua tufuate mfumo huo linaweza kuonyesha
njia ya kuondoa hofu hizo. Kwa waumini wa Serikali mbili wanaona
kuwa huu ni uthibitisho wa ubora wa muundo wa Serikali mbili.
Changamoto za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika kuainisha
changamoto za muundo wa Serikali tatu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeyataja
mambo mengine mawili makubwa ambayo ningependa Waheshimiwa Wajumbe muyape
tafakuri stahiki. Mambo hayo ni mosi,
misuguano na mikwamo (deadlocks and paralysis) katika kujadili na
kufanya uamuzi kuhusu mambo muhimu ya Muungano. Na pili, ni kuibuka kwa hisia za utaifa (nationalistic
sentiments) wa zamani kwa nchi washirika. Nawaomba myatafakari kwa
makini sana mambo haya, kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu
ustawi na uhai wa Muungano, bali hata usalama wa raia na mali zao. Naona
hata Tume haikuweza kupata ufumbuzi ulio mwafaka kabisa kwa changamoto
hizi. Bila ya shaka katika mijadala yenu Waheshimiwa Wajumbe mnaweza
kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni lazima lifanyike
kila linalowezekana kuhakikisha kuwa maamuzi hayakwami kwani yakikwama maana
yake shughuli za Muungano zitakuwa zimekwama. Kama hazitakwamuliwa kwa
wakati ustawi wa Muungano utaathirika. Ikishindikana kabisa kupatikana
ufumbuzi Muungano unaweza kuvunjika. Kuibuka na kukua kwa hisia za utaifa
(nationalistic feelings) kwa nchi washirika, yaani Utanganyika na
Uzanzibari ni tishio kubwa sana kwa uhai wa Muungano. Hebu fikiria, watu
walioishi pamoja kidugu na kwa kushirikiana, kama watu wamoja na raia wa nchi
moja yaani Watanzania kwa miaka 50, kuja kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya
Watanganyika na Wazanzibari na siyo kati ya Watanznaia. Kwa mujibu wa
sensa iliyopita takriban asilimia 90
ya Watanzania waliopo sasa wamezaliwa baada ya mwaka 1964. Nchi wanayoijua
ni Tanzania. Litakuwa ni jambo lenye mshtuko mkubwa na athari zisizoweza
kutabirika, watu hao watakapojikuta ni wageni wanaotakiwa kutengenezewa
utaratibu maalum wa kusafiri na kuishi wakiwa upande wa Muungano ambao siyo
kwao kwa asili. Wanakuwa wageni na fursa walizokuwa wanazipata waendapo
popote haiwi rahisi tena kuzipata.
Katika mazingira hayo
ni rahisi sana chuki kupandikizwa na watu waliokuwa ndugu mara moja watajikuta
maadui. Aidha, watu wanaweza kujikuta wakilazimika kurudi kwao kwa asili
ama kwa kufukuzwa au kwa sababu ya mazingira kuwa magumu kiasi cha kuona bora
waondoke. Watu hao wanaweza kulazimika kuondoka huku wakiacha nyuma kila
kitu walichokichuma maishani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Changamoto hizi kubwa
mbili za mfumo wa Serikali tatu ambazo Tume imeziona, ni za kweli. Si
mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta watu wenye asili ya Tanzania Bara
ya kuchomewa moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012 na watu wenye hisia kali za
Uzanzibari, na kuwataka watu wa Bara waondoke Zanzibar, huenda yakawa
madogo. Matukio ya namna hii yanaweza kutokea pande zote mbili na
kusababisha maafa makubwa. Itaanza baina ya watu, baadaye itakuwa baina
ya Serikali zetu mbili na kuzifikisha nchi zetu mbili zilizokuwa ndugu na
rafiki, kwa nusu karne, ghafla kuwa maadui wasioombana chumvi na wasiotakiana
heri. Umoja wetu utatetereka na Muungano wetu unaweza kuvunjika.
Kwa nini tufike huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sisi viongozi
tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba ya wananchi wetu, hatuna budi kuyapima
mambo haya kwa umakini mkubwa ili tufanye uamuzi ulio sahihi. Tusije
tukajutia uamuzi wetu tutakapoona watu wanafukuzana, wanauana na mali zao
kuporwa. Na, tukifikia hatua hiyo Muungano kusambaratika halitakuwa jambo
la ajabu.
Kwa kweli,
unapoyatafakari haya, ni rahisi kuelewa kwa nini wazee wetu waasisi waliamua
walivyoamua. Waliona mbali. Tusipuuze fikra zao na maono yao.
Kuna hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza kila kitu tulichokijenga kwa
miaka 50. Badala ya kujenga tunaweza kujikuta tumebomoa hata msingi
katika nchi washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka
1993 alituasa kuhusu hatari hiyo: “Hamuwezi
kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu… na adhabu nyingine zimo mle mle
ndani ya kitendo hazisubiri.”
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Siku moja kiongozi
mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini aliniuliza: “Hivi Serikali mbili zikiwa na
matatizo jawabu ni kuongeza ya tatu? Si matatizo ndiyo yatazidi? Je,
matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu si kila mtu atachukua njia yake?
Mtakuwa mmepoteza kila kitu. Mimi nawashauri msichoke kutafuta
majawabu kwa matatizo ya hizi mbili! Huko mnakotaka kwenda kuna hatari
nyingi”.
Pengine
na ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Kazi Yenu Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mambo ya kuyasemea ni
mengi mno lakini kwa sababu ya ufinyu wa muda, nisingeweza kuyazungumzia
yote. Naamini, mtayaona katika kuipitia Rasimu na kwenye
majadiliano yenu. Napenda kusisitiza kwenu kuwa kazi iliyo mbele yenu ni kubwa
sana. Ni kubwa kwa maana mbili. Kwanza, jukumu lenyewe la kutunga
Katiba ya nchi ni zito sana. Taswira ya nchi yetu itakuwaje na
itaendeshwa vipi kwa miaka mingi ijayo iko mikononi mwenu. Ipeni nchi
yetu hatima njema. Pili, ni kubwa kwa maana ya uzito wa mambo ya
kujadili na kuyafanyia uamuzi. Kwa ajili hiyo, ni muhimu sana kuisoma
Rasimu na Taarifa ya Tume kwa makini na kuzielewa. Jipeni muda wa
kutafakari kila neno, kila sentensi, na kila dhana ili muweze kufanya uamuzi
ulio sahihi. Mkifanya hayo mtakuwa mmeisaidia nchi yetu na Watanzania
wote kupata Katiba nzuri.
Nimefarijika sana
kusikia kuwa mtajigawa kwenye Kamati 12 wakati wa kujadili Rasimu. Huu ni
utaratibu mzuri kwani mkiwa katika vikundi vya watu wachache, mtakuwa na
mijadala ya kina zaidi. Watu wote wanaweza kupata fursa ya kutoa maoni
yao, kwa kila kifungu na kila jambo linaloibuliwa na kuzungumzwa. Kwa
kufanya hivyo, mtatimiza kwa ukamilifu jukumu lenu la kutunga Katiba.
Wote mtakuwa mmeshiriki kujadili kila sura na vipengele vyake vyote.
Mkimaliza kazi yenu mtapokea kwa haki sifa nzuri kama Katiba itakuwa nzuri, au
lawama stahiki iwapo itakuwa kinyume chake.
Pongezi kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nitakuwa mwizi wa fadhila
kama nitamaliza hotuba yangu bila ya kutambua kazi nzuri iliyofanywa na
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi,
alipokuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hili. Kazi yake haikuwa rahisi hata
kidogo, lakini kwa umahiri na ustadi mkubwa ameweza kufanikisha mambo kwa kiasi
ambacho anastahili pongezi zetu sote. Anastahili pongezi kwa sababu yeye
aliendesha Bunge hili bila ya kuwepo kwa kanuni. Tatizo hili hatakuwa
nalo Mwenyekiti wa Kudumu kaka yangu Mheshimiwa Samuel Sitta.
Napenda pia
kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa hatua
mliyofikia. Hata hivyo, mmechukua muda mwingi katika hatua ya awali hivyo
hamna budi kuongeza kasi. Naomba niwakumbushe kuwa mijadala yenu hii
inafuatiliwa kwa karibu sana na Watanzania. Wamewekeza sana matarajio yao
kwenu. Hamna budi, haiba na taswira ya uongozi muionyeshe wakati wote wa
kuendesha mijadala yenu kwa lugha na vitendo vyenu. Wakati wa semina na mjadala
wa kupitisha Kanuni za Bunge hili, baadhi ya wananchi wamekwazika sana na
mwenendo wa baadhi ya Wajumbe. Hawakutegemea kuyaona matendo
waliyoyaona mkifanya na kusikia maneno waliyoyasikia kutoka kwenye vinywa vya
baadhi yenu.
Ni matumaini yangu na
ya Watanzania wote kuwa hali ile haitajirudia tena katika awamu
hii. Tusiwafikishe mahali Watanzania wakakata tamaa na Wajumbe wao
au na hata chombo hiki muhimu sana kwa mustakabali wao na wa nchi yao.
Tutoe hoja badala ya kupiga kelele (argue don’t shout) au
kuzomea. Hakuna haja ya kutumia lugha isiyokuwa ya staha katika
kujieleza. Hakuna haja ya kukingiana ngumi, kutishiana hili na lile
au hata kugombana. Ni utovu wa uungwana usiotegemewa kutoka
kwenu. Tusiwaangushe wananchi wa Tanzania wanaotutegemea sana.
Wekeni Maslahi ya Taifa Mbele
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ombi langu la mwisho
kwenu ni kuwasihi kuwa wakati wote muongozwe na kujali maslahi mapana ya nchi
yetu na watu wake badala ya kujali maslahi yenu binafsi au ya makundi
yenu. Naomba kaulimbiu yenu iwe “Tanzania
Kwanza”. Najua kila mmoja wenu amekuja na maoni yake au atakuwa
nayo kwa kila jambo litakalojadiliwa. Wengine wamepewa misimamo na vyama
vyao au makundi yao. Si jambo baya na ni hatua muhimu ya kuleta
mafanikio, kama misimamo hiyo na mawazo hayo ni ya kujenga.
Hata hivyo,
mnachotegemewa kufanya ni kuwa tayari kuwianisha na kuunganisha mawazo yenu
mazuri na ya wenzenu, ili kupata msimamo wa pamoja na uamuzi wa pamoja ulio
bora. Kwa sababu hiyo, hamna budi kuwa tayari kusikiliza mawazo ya
wengine, hata kama ni tofauti na yenu mliyokuja nayo. Tafuteni kilicho
chema kwa yale yanayosemwa na watu wengine hata kama ni watu
usiokubaliana nao au huwapendi au hampendani. Kunaweza
kuwepo kitu chenye manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Nawaomba muwe hodari
wa kushawishi badala ya kulazimisha. Mkifanya hivyo hamtalazimika kutumia
muda mwingi wa kula njama za namna ya kuwazidi maarifa wale mnaotofautiana nao
kwa mawazo. Lazima pia mtafute namna ya kushirikiana na kuwasiliana na
makundi mengine. Msitafute kushindana, hili ni jambo ambalo lazima wote
mtoke hapa mkiwa washindi. Yaani lazima Watanzania wote washinde kwani
wao ndiyo wenye Katiba yao. Nawapongeza
viongozi wa vyama vya siasa na asasi mbalimbali kwa kutambua na kuthamini
umuhimu wa kuwa na taratibu za mawasiliano, mashauriano na
ushirikiano. Daima muwe watu wa kutafuta maridhiano. Mmefanya vizuri
katika hatua ya awali. Mmejiwekea taratibu nzuri za kufanya hayo,
tafadhalini zitumieni. Jengeni madaraja imara zaidi katika
awamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Naomba nimalize kwa
kuwaomba Watanzania wote tukiongozwa na viongozi wetu wa dini tumuombe Mola
wetu ajalie rehema zake ili mchakato wa kutunga Katiba uende salama.
Aliongoze Bunge hili na Wajumbe wake waweze kufanya uamuzi ulio sahihi na wenye
manufaa kwa taifa letu kwa kila watakaloliamua.
Baada ya kusema
maneno yangu mengi hayo, nirudie kukushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa
fursa hii adhimu ya kulihutubia Bunge Maalum la Katiba. Nawatakieni kila
la heri na mafanikio mema. Katiba
Mpya Inawezekana, Timiza Wajibu
Wako.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Libariki Bunge Maalumu la Katiba!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,JAKAYA MRISHO KIKWETE, WAKATI AKIZINDUA BUNGE MAALUM LA KATIBA, TAREHE 21 MACHI, 2014, DODOMA .”
Post a Comment