Friday, March 21, 2014

WAKO: MSIPUUZE MAONI YA WANANCHI.


Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Serikali ya Kenya, Seneta Amos Wako akizungumza jana, wakati wa Semina ya Bunge Maalumu la Katiba. Picha na Salim Shao


Mwanasheria Mkuu (AG) mstaafu wa Kenya, Amos Wako amewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutokupuuza maoni ya wananchi katika kutunga Katiba ya nchi vinginevyo watazua mgogoro.

Wako, ambaye kwa sasa ni Seneta wa Busia ya Mashariki nchini Kenya, alitoa ushauri huo jana katika semina kwa wajumbe wa Bunge la Katiba kuhusu uzoefu wa namna nchi hiyo ilivyopitia misukosuko ya kuipata Katiba mpya.

Wako ambaye kwa miaka 21 alikuwa katika wadhifa wa AG, amesema matukio mengi yaliyosababisha Kenya kutokupata Katiba yao kwa wakati, yalitokana na kutokuwashirikisha wananchi moja kwa moja katika mchakato.

Katika hotuba yake iliyodumu kwa saa 2: 11, mwanasheria huyo aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba ya Kenya alionya pia kuwa Katiba inayotengenezwa hapa nchini isiwe ya kunukuu kutoka katika mataifa mengine kwa sababu mahitaji yanatofautiana kwa kila nchi.

“Katiba isiwe ya mazungumzo kutoka kwa viongozi pale Dar es Salaam, kwani itakuwa ni mali ya watu wachache na ambayo lazima itapingwa, hata sisi tulianza hivyo lakini tulishindwa vibaya,” alionya Wako.

Aliimwagia sifa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni Jumanne iliyopita, kwamba kwa mtindo ilivyowasilishwa inaonekana kuwajali na kuwapa nafasi zaidi wananchi wa hali ya chini.

“Pamoja na hayo, lakini Katiba hii ikiingiliwa zaidi na kutekwa na wanasiasa au kikundi cha watu wachache kwa masilahi yao, inaweza kuharibika kama ilivyotokea kwetu Kenya ambako Kanu walikuwa wakipinga kila kitu wakatufanya tuingie katika mgogoro.”
Amesema kuwa mitazamo ya wanasiasa huwa ni tatizo na hatari katika kutafuta Katiba mpya na dawa pekee na ya maana ni kutoa nafasi kwa wananchi waamue wenyewe.

“Mfumo uliowekwa katika mchakato wa kuunda Katiba mpya nchini kwenu, kwamba Rasimu ya mwisho ya Katiba itoke bungeni na kupelekwa moja kwa moja kwa wananchi ni mzuri, ni muhimu maoni ya wananchi ya awali yazingatiwe,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, Bunge Maalumu limeaminika kufanya kazi hiyo ili kuwasaidia wananchi kufikia malengo yao.
Akizungumzia uzoefu wa Kenya katika kupata Katiba mpya alisema walianza kwa kukabiliana na changamoto kubwa ya ukabila ambayo kila jamii ilikuwa haiamini kundi jingine katika kutafuta usawa, jambo alilosema ni tofauti na Tanzania.

0 Responses to “WAKO: MSIPUUZE MAONI YA WANANCHI.”

Post a Comment

More to Read