Friday, March 21, 2014

NDEGE NNE ZILIWAHI KUPOTEA TANZANIA.




Wakati tukio la kupotea kwa ndege ya Shirika la Ndege la Malaysia, MH370, linaendelea kuitikisa dunia, imebainika kuwa Tanzania si jambo jipya kutokana na kuwapo kwa kumbukumbu ya matukio manne tofauti kama hayo katika miongo minane iliyopita.
Ndege hiyo ya Malaysia ilipotea wiki mbili zilizopita ikiwa na abiria 227 na wafanyakazi 12 huku juhudi za kuitafuta zinazofanywa na nchi 26 zenye uwezo mkubwa wa kiuchunguzi zikiwa hazijazaa matunda.

Kwa matukio ya Tanzania, Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege kutoka Wizara ya Uchukuzi, John Nyamwihura amesema katika mahojiano maalumu na mwandishi wetu kuwa Tanzania imewahi kuingia katika kumbukumbu za ndege ndogo kupotea na  baadhi hazikuonekana kabisa na nyingine zilionekana baada ya miaka kadhaa kupita. Ndege ya kwanza kupotea ilikuwa mwaka 1937 iliyokuwa ikitoka Tanzania kwenda Madagascar. Ilikuwa na abiria wanane na haijaonekana hadi leo.

Mbali na tukio hilo ambalo limedumu kwa miaka 77 sasa, Nyamwihura alisema tukio la pili ni la mwaka 2003 wakati ndege iliyokuwa ikitoka Tanzania kwenda Zambia ilipopotea ikiwa na raia wawili wa Afrika Kusini, nayo pia haijaonekana hadi sasa.

Mkaguzi huyo alisema katika matukio mengine mawili, ndege zilizopotea zilionekana baadaye. Mwaka 1997, ndege ndogo iliyokuwa na abiria mmoja ilipotea katika bonde kwenye kilele cha Kibo, Mlima Kilimanjaro baada ya kutumbukia kwenye korongo na kuganda kwenye barafu bila kuonekana hadi baada ya miaka sita. Hata ilipoonekana haikuwezekana kutolewa.

“Ndege ile ilikuwa ikitoka Nairobi kwenda Zanzibar ikiwa na rubani wa Kitanzania peke yake,” alisema Nyamwihura.
Ndege nyingine iliyoingia katika orodha hiyo ni ile iliyoanguka katika Ziwa Victoria mwaka 1976 ikiwa na abiria 12 ambayo ilionekana miaka miwili baadaye.

Nyamwihura akisema sababu kubwa ya matukio hayo ni mabadiliko ya hali ya hewa na kuharibika kwa miundombinu, mambo ambayo husababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya waongoza ndege na marubani.

“Matukio mengi kama haya ni kuwa ndege hugonga milima na kuanguka. Zikianguka sehemu za milima ni vigumu kupatikana kwa sababu wakati mwingine huganda katika barafu au kuzama kwenye makorongo,” alisema.

Alisema hata ndege zinazoanguka kwenye maji, pia ni vigumu kuonekana kutokana na kina kirefu au barafu.
Mtaalamu huyo alisema kuna baadhi ya ndege ambazo hupotea kutokana na rubani kukata mawasiliano kwa makusudi kwa sababu ama za kigaidi au magendo.

0 Responses to “NDEGE NNE ZILIWAHI KUPOTEA TANZANIA.”

Post a Comment

More to Read