Friday, March 21, 2014

WARIOBA AWAGONGANISHA KIFICHO NA MWAKILISHI.


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.


Hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba katika Bunge la Katiba imewagonganisha  Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho na Mwakilishi wa Baraza hilo, Rufani Said Rufani.

Wakati Kificho akisisitiza kuwa Baraza hilo halikupendekeza muundo wa serikali tatu, Warioba alieleza kwenye hotuba yake kuwa kiini cha tume yake kupendekeza Muungano wa serikali tatu ni maoni ya wananchi na taasisi mbalimbali, likiwamo Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

 “Hii inaonyesha kwamba Tume yenyewe ilishakuwa na mwelekeo wa serikali tatu kwa sababu kama alivyoeleza Warioba kwamba walitafsiri maoni yetu kuwa ni yenye kuhitaji serikali tatu na wakati mwingine, tafsiri inaweza kukupa maana tofauti na maana halisi,” alieleza Kificho.

Kificho alisema Baraza hilo linaundwa na wawakilishi kutoka vyama mbalimbali, CCM na CUF ambapo CCM msimamo wao ni serikali mbili na kwamba hana uhakika kwa upande wa CUF, ingawa anadhani wana msimamo wa serikali tatu.

Hata hivyo, Rufani, ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Tumbe kupitia CUF, alikubaliana na alichosema Jaji Warioba kuwa ndicho kilichokubaliwa na baraza hilo.

“Ingawa sikuwa mjumbe katika kamati ya uongozi kwa nafasi yangu ya uwakilishi naafikiana kuwa maoni yaliyosomwa na Jaji Warioba bungeni ndiyo hasa tuliyopeleka na jinsi alivyoyatafsiri ndivyo tulivyomaanisha,” alieleza Said.

0 Responses to “WARIOBA AWAGONGANISHA KIFICHO NA MWAKILISHI.”

Post a Comment

More to Read