Saturday, April 26, 2014

HII NI HISTORIA YA MIAKA 50 YA MUUNGANO TANGU NCHI YA TANGANYIKA NA ZANZIBAR ZILIPOUNGANA NA KUZAA NCHI YA TANZANIA







Kumbu kumbu zinaonyesha Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ziliingia mkataba tarehe 22 Aprili 1964 huko Zanzibar kwa lengo la kuunganisha nchi hizo mbili baada ya kutiwa saini na viongozi wa nchi hizo kwa wakati huo ambao ni aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.
  • Baada ya kutiwa saini kwa mkataba huo au kama unavyojulikana hati ya Muungano baadae mkataba huo ulipelekwa kwenye mabunge yote mawili yaani Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi tarehe 26 Aprili, 1964 ili uridhiwe rasmi kuwa sheria ya Muungano ambapo nchi mpya inayojulikana "Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar" ilizaliwa ambapo sherehe kubwa zilizofana za kuchanganya udongo wa pande zote mbili zilifanyika.
Hata hivyo nchi hii mpya iliendelea kujulikana kwa jina hilo la"Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar" hadi Oktoba 28, 1964 lilibadilishwa rasmi kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jina linatumika hadi hivi leo kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria namba 61 ya mwaka 1964.

Kwa ujumla Muungano huo wa kuunganisha nchi mbili kwa hiari umekuwa ukisifiwa kwamba ni Muungano wa kipekee barani Afrika Professa Paramagamba Kabudi Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yeye anasema katika utafiti wake amegundua ni Muungano huo ndio pekee wa hiari uliodumu hadi hivi leo.
Muundo wa Muungano uliokubaliwa
Nchi mpya iliyozaliwa yaani Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni muungano wenye Muundo wa vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji ambavyo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pia vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki ambavyo ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar;
na pia vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma ambavyo ni Bunge la Jamuhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi.

Katika utekelezaji wa shughuli zake Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenyewe imepewa mamlaka ya kushughulikia mambo yote ya Muungano kama yalivyoainishwa katika Katiba ya Tanzania na mambo yale yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenyewe imepewa mamlaka ya kushughulikia mambo yote yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Zanzibar.
Mambo ya Muungano
Mambo ya Muungano ya kwanza kabisa yaliyoanishwa kwenye Katiba ya muda ya mwaka 1965 yalikuwa ni 11 ambayo ni
• Katiba na Serikali ya Muungano
• Mambo ya Nchi za Nje
• Ulinzi
• Polisi
• Mamlaka juu ya mambo yanohusika na hali ya hatari
• Uraia
• Uhamiaji
• Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje
• Utumishi katka Serikali ya Jamhuri ya Muungano
• Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika,
ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa
nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha.
• Bandari mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na
simu.
Hata hivyo Baadae Mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka kumi na moja (11) hadi ishirini na mbili (22)
Likiwemo suala la sarafu na benki kuu ambapo nchi zote zilianza kutumia sarafu moja hadi hivi leo.

Mbali na mafanikio yaliyopatikana Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar umekuwa ukipitia safari ya mabonde na malima ambapo wapo wanaona kuwa umewapa manufaa huku wengine wakidhani muungano hauna faida.

Kwa sasa Tanzania ipo kwenye mchakato wa kuandika Katiba Mpya ambapo suala la Muundo upi wa Muungano unaofaa kati ya Muundo uliopendekezwa kwenye rasimu ya Katiba wa serikali tatu na muundo wa sasa unaopigiwa debe na chama tawala wa serikali mbili ni mjadala uliopamba moto katika nchi hii.
Hata hivyo kwa vyovyote vile pamoja na changamoto na matatizo yote hayo ni wazi muungano huo kufikisha miaka 50 sio jambo dogo.

0 Responses to “HII NI HISTORIA YA MIAKA 50 YA MUUNGANO TANGU NCHI YA TANGANYIKA NA ZANZIBAR ZILIPOUNGANA NA KUZAA NCHI YA TANZANIA”

Post a Comment

More to Read