Monday, April 7, 2014
SERIKALI YASEMA HAITASAJILI SEKONDARI AMBAZO HAZINA MAABARA KUANZIA SASA.
Do you like this story?
KUANZIA
sasa, shule yoyote mpya isiyokuwa na maabara ya sayansi na maktaba
haitasajiliwa na wala kuruhusiwa kutoa huduma; Serikali imeagiza.
Wakati
agizo hilo linagusa shule za Serikali pamoja na za binafsi zinazojengwa, kwa
upande wa shule zilizopo ambazo hazina mahitaji hayo, unaandaliwa mkakati hatimaye
zote ziwe na maabara na maktaba.
Akizungumza
na mwandishi katika mahojiano maalumu, Kamishna wa Elimu Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eustella Bharalusesa alisema hakuna usajili
utakaotolewa kwa shule yoyote mpya bila kutimiza masharti hayo.
Hatua
hiyo ya Serikali ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wake wa Matokeo Makubwa
Sasa (BRN) katika sekta ya elimu kuwezesha upatikanaji elimu bora na yenye
viwango.
Kamishna
huyo wa Elimu alisisitiza, “hii inatokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete kwa
shule zote mpya zinazojengwa kuhakikisha masharti haya yanatekelezwa,
vinginevyo, shule husika hazitapewa usajili hata kidogo.”
Kwa
mujibu wa Profesa Bharalusesa, maabara zinapaswa ziwe zimekamilika kwa kuwa na
vifaa vyote vinavyohusu masomo ya Fizikia, Kemia na Bayolojia.
Vile
vile kwa upande wa maktaba, maelekezo ya wizara ni kwamba lazima ziwe
zimekamilika kwa ajili ya kuwezesha utoaji elimu yenye viwango.
Hivi
karibuni, vyombo mbalimbali vya habari, viliripotiwa juu ya baadhi ya shule za
serikali mkoani Arusha kushindwa kuanza muhula mpya wa masomo kutokana
kutokidhi masharti ya kuwa na maabara na maktaba.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, hivi
karibuni aliliambia gazeti hili kwamba yako mabadiliko mengi yanayotarajiwa
kufanyika katika sekta ya elimu.
Alisema
mipango mbalimbali pamoja na sera zitaundwa kukidhi mahitaji hayo. Alisema
mabadiliko hayo yatajitokeza kupitia Sera ya Elimu na Mfunzo inayopitiwa.
Kwa
mujibu wa Profesa Mchome, kama mambo yatakwenda vizuri, sera hiyo itakuwa
tayari mwakani na itatumika kutatua kasoro mbalimbali katika sekta ya elimu.
>>>HABARI
LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SERIKALI YASEMA HAITASAJILI SEKONDARI AMBAZO HAZINA MAABARA KUANZIA SASA.”
Post a Comment