Tuesday, April 1, 2014
SITTA AMPA BARUA MTIKILA AENDE KWA JK.
Do you like this story?
Ombi la Mjumbe wa Bunge la Katiba, Mchungaji
Christopher la kutaka Bunge hilo livunjwe, limekuwa zito kwa Mwenyekiti Samuel
Sitta.
Kutokana na ugumu huo, Sitta amelazimika
kumpatia barua Mtikila ili awasilishe hoja yake kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye
kisheria ana mamlaka hayo ya kuvunja Bunge la Katiba, ambalo limekuwa
likionekana kwenda mrama.
Mtikila, ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha
Kidemokrasia na mjumbe wa Bunge la Katiba aliwasilisha barua yenye hoja binafsi
akitaka bunge hilo livunjwe na wajumbe warejee makwao kwa madai kuwa chombo
hicho cha kutunga Katiba mpya hakijali maslahi ya umma na uongozi umekuwa
haumtendei haki.
Majibu ya barua hiyo yalikuwa hivi:
“Nimeagizwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu nikujulishe kwamba Bunge Maalumu
halina uwezo wala mamlaka ya kujitangaza kwamba ni haramu na hivyo livunjwe ;
na kwamba hoja hiyo haistahili kuwa hoja ya Bunge Maalumu,” inasomeka barua
hiyo iliyoandikwa na katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad.
Akizungumza na Mwananchi jana, Sitta alikiri
kumpatia barua hiyo Mtikila ili aende kwa Rais Kikwete kwa sababu hoja yake
kutaka kuvunjwa Bunge haiwezi kusikilizwa na chombo hicho kwa kuwa mwenye
madaraka ya kuvunja Bunge ni Rais pekee.
“Ni kweli ametuletea hoja ya kuvunja Bunge.
Ameandika mambo mengi, akitumia lugha ya uchochezi, kama kudai kwamba
‘Tanganyika imekuwa koloni la Zanzibar kwa muda mrefu’, lugha ya namna hii
hatuwezi kuikubali,” alisema Sitta.
Sitta alisema siyo kila kitu ambacho mjumbe
anasema, ni lazima kifuatwe katika mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya.
“Mtu akija anasema anataka Bunge livunjwe
amfuate aliyetuteua, siyo sisi wenyewe kujivunja,” alisema Sitta.
Alisema hoja ya Mtikila, ambaye alitishia
kufungua kesi ya kuzuia Bunge la Katiba kufanya kazi, ya kutaka Bunge kuvunjwa
imekwenda kinyume kabisa na taratibu za Bunge.
“Hoja hii imekwenda nyuzi 180 kwa sababu
aliyetuteua alitaka sisi tutunge katiba kutokana na rasimu, ili sisi tupeleke
kwa wananchi rasimu iliyopendekezwa,” alisema.
Mchungaji Mtikila alikiri kupokea barua
kutoka Ofisi ya Bunge ikimweleza jambo moja; apeleke hoja yake kwa Rais Kikwete
aliyeteua Bunge la Katiba.
Hata hivyo, alisema hakusudii kwenda kumuona
Rais Kikwete baada ya kushauriwa kupitia barua ya Bunge kutokana na kutoa hoja
ya kutaka kuvunjwa kwa bunge hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SITTA AMPA BARUA MTIKILA AENDE KWA JK.”
Post a Comment