Tuesday, April 1, 2014
MVUA ZALETA MAAFA MAKUBWA DAR, MIKOANI.
Do you like this story?
Dar/Pwani/Kagera. Mvua zilizonyesha maeneo mbalimbali nchini tangu wiki
iliyopita, zimesababisha maafa, uharibifu wa mali, miundombinu na kuacha zaidi
ya familia 150 bila makazi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini
kuwa athari za kifamilia zimeukumba zaidi Mkoa wa Kagera ambako familia zaidi
ya 125 zinahitaji msaada baada ya nyumba zao kuezuliwa paa na mashamba ya
migomba kuharibiwa.
Ingawa maeneo mengi ya nchi yameathirika,
hali inaonekana ni ya kiwango cha juu zaidi katika mikoa ya Dar es Salaam,
Bukoba, Lindi na Mtwara.
Jijini Dar es Salaam, maeneo kadhaa yamejaa
maji na hata kusababisha watu kuyakimbia makazi yao kama vile Jangwani, Bonde
la Mto Msimbazi na Mbweni ambako Serikali ilipima viwanja na kuvigawa kwa
wananchi.
Mkoani Kagera, maeneo yaliyoathirika zaidi ni
ya vijiji vya Bulembo, Kata ya Kamachumu wilayani Muleba.
Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage
alisema: “Hali siyo nzuri na timu ya watalaamu ipo eneo la tukio ili kufanya
tathmini zaidi kuhusu kadhia hiyo.
“Watu wa Msalaba Mwekundu wanajaribu
kurejesha paa upya katika baadhi ya nyumba zilizoezuliwa.”
Mkazi wa Kijiji cha Bulembo, Richard
Kichabeba alisema familia zilizokumbwa na tatizo la nyumba zao kuezuliwa paa,
zinaishi nje na mbaya zaidi nyumba zinazidi kuporomoka kutokana na mvua
zinazoendelea kunyesha.
“Hakuna muhogo wala mgomba. Mawe na upepo
vimevuruga kila kitu,” alisema mkazi huyo na kuongeza kuwa mbaya zaidi hata
hizo paa zao hazijulikani zimeangukia wapi.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi
alisema kuwa uongozi wa wilaya hiyo umelazimika kuifunga kwa muda usiojulikana
Barabara ya Msata – Bagamoyo baada ya maji kuifunika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha,
Halima Kihemba alisema kuwa hivi sasa Kata mbili za Ruvu na Kwala hazifikiki
baada ya madaraja kubomoka.
Alisema kuwa madaraja mawili ya Mto Ndwati na
Msua yamefurika maji hali iliyosababisha mafuriko makubwa, hivyo aliwataka
wakazi wa vijiji hivyo kuchukua tahadhari.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MVUA ZALETA MAAFA MAKUBWA DAR, MIKOANI.”
Post a Comment