Friday, May 23, 2014
ATCL YAREJEA KWA KASI KATIKA ANGA ZA ARUSHA NA ZANZIBAR
Do you like this story?
SHIRIKA la
Ndege la Taifa, Air Tanzania (ATCL) limerejea katika anga za Arusha na Zanzibar
na kuahidi kusafiri katika maeneo hayo yenye vivutio bora vya kiutalii mara
sita kwa wiki.
Katika safari
hiyo ya uzinduzi ya kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kupitia Arusha,
kulikuwa na mawaziri wawili wa pande zote za muungano ambao walionyesha
kufurahishwa na safari hiyo, mbali na kutoa nasaha kwa shirika hilo.
Ikitokea Dar
es Salaam kwenda Arusha, alikuwemo Waziri wa Maliasili na Utalii Bw. Lazaro
Nyalandu na wakati wa kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam, alipanda Waziri wa
Nchi katika Ofisi ya Rais Zanzibar (Utawala Bora), Dkt. Mwinyihaji Haji Makame,
wote wakiashiria kuwa safari hiyo imerejesha matumaini ya
kuwaunganisha watalii kutoka Arusha kwenda Zanzibar na kurudi Dar es Salaam.
Akizungumza
mara baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Arusha, Mh. Nyalandu, alisema
kurejea kwa ndege ya shirika hilo la Taifa katika njia ya Arusha na Zanzibar
kutakuza sekta ya utalii na kurahisisha uunganishwaji wa maeneo hayo muhimu
yenye vivutio vikubwa vya utalii.
“Ninayofuraha
ya kuwataarifu watalii, wageni wanaotembelea nchi yetu na watanzania wenzangu
kuwa Air Tanzania sasa imerudi angani.
Nimekuwa
miongoni mwa abiria wa kwanza kusafiri na ndege hii kuja hapa Arusha, kwa hiyo
nataka kuwahakikishia wote kuwa usafiri wa Air Tanzania ni tulivu, wanatoa
huduma nzuri ndani ya ndege, ni salama na utafurahia safari yako.
“Uzinduri wa
safari hii unadhihirisha kwamba sasa ushindani wa kweli katika sekta ya usafiri
wa anga umeanza. Shirika la Air Tanzania linatakiwa kuhakikisha linaendeleza
dhamira yake ya kutoa huduma bora ili liweze kurejesha imani lililokuwanayo kwa
abiria wake walio wengi,” alisema Nyalandu.
Naye, Kaimu
Mkurugenzi wa Biashara wa ATCL Bw. Juma Boma alisema safari ya Dar es Salaam –
Arusha – Zanzibar ni sehemu ya mkakati wa shirika lake wa kutanua huduma zake
katika maeneo mengi iwezekanavyo.
“Tunajivunia
kuendelea kutekeleza dhamira yetu ya kuimarisha huduma zetu tukiwa kama shirika
la Ndege la Taifa. Tukilenga kuendelea kutanua wigo wa huduma zetu ndani ya
nchi na kimataifa.
“Lengo letu
kubwa kama Shirika la Ndege la Taifa ni kuendelea kutoa huduma zenye gharama
nafuu, vile vile kuongeza uwezo wa abiria kusafiri kwa wakati wao”. Ndiyo
sababu tumeondoa adhabu kwa wale abiria wanaochelewa kufika uwanja wa ndege au
kushi ndwa kufika kabisa siku ya safari na wanaobadilisha tarehe za safari
zao,” alisema.
Aidha, Waziri
wa Zanzibar, Mwinyihaji Haji Makame, alisema inatia moyo kuona ATCL ikirejesha
safari zake Zanzibar baada ya kusitisha huduma zake katika kisiwa
hicho kwa zaidi ya miaka minne, lakini aliwataka ATCL kufuata muda na
kuhakikisha wanapunguza adha ya usitishaji wa safari endapo wanataka kurejesha
imani miongoni mwa abiria walio wengi.
Akizungumza
baada ya kupokea safari hiyo ya uzinduzi katika uwanja wa ndege wa Arusha, Mkuu
wa Wilaya ya Arusha mjini, Bw. John Mongela alisema uanzaji wa safari hizo za
ATCL katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Geneva ya Afrika
umerejesha sifa iliyokuwa nayo ndege hiyo ya taifa kipindi cha nyuma wakati wa
mikutano ya kimataifa jijini Arusha.
“Hii ni hatua
ya busara sana kwa ATCL. Jiji la Arusha alitoi tu fursa ya ndege hii
kusafirisha watalii moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kuja Arusha na
kuwaunganisha kwenda Zanzibar, bali pia inawapa fursa ya kusafirisha viongozi
wa kimataifa wanaosafiri mara kwa mara kuja Arusha kwa ajili ya mikutano,”
alisema.
Kwa sasa,
ATCL itakuwa ikitumia ndege yake aina ya Bombardier Dash - 8 yenye uwezo wa
kubeba abiria 50 katika njia hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ATCL YAREJEA KWA KASI KATIKA ANGA ZA ARUSHA NA ZANZIBAR ”
Post a Comment