Saturday, May 17, 2014
DAWA YA TRUVADA YATUMIKA KUZUIA UKIMWI BADALA YA KONDOMU.
Do you like this story?
Wanawake wanaofanya biashara ya kuuza
miili na wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja sasa wanatumia dawa za
kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi aina ya Truvada kwa ajili ya kuzuia
maambukizi ya ugonjwa huo badala ya kutumia mipira ya kondomu.
Mwananchi lilizungumza na baadhi ya
wafanyabiashara ya ngono jijini katika maeneo ya Mwananyamala Hospitali,
Komakoma na Vingunguti ambao walisema kuwa wanatumia dawa hizo kwa ajili ya
kuzuia maambukizi ya VVU ili kuwaridhisha wateja wasiopendelea mipira hiyo.
Baadhi ya wafanyabiashara hao walidai
kuwa wanatumia Truvada kuzuia maambukizi pindi wanapokutana na wanaume wakware
ambao huwabaka au kuwalazimisha kufanya mapenzi bila kinga.
“Hizi dawa tunazipata katika hospitali
na wakati mwingine katika maduka makubwa ya dawa. Kwa sababu zinazuia
maambukizi ya Ukimwi na sisi ni watu ambao tunafanya kazi katika mazingira
hatarishi,” anasema Leyla Musa, mmoja wa wanawake hao.
Si hivyo tu, kwa kuwa hii ni biashara
baadhi yao hukubali kufanya mapenzi bila mipira ili kupata fedha nyingi kutoka
kwa wanaume.
Wengine hukimbilia huduma ya PEP
Baadhi ya wanawake hao wanasema kuwa
baada ya kufanya mapenzi na wanaume kadhaa asubuhi huenda katika kliniki
zinazotoa huduma za ARV na kudanganya kuwa wamebakwa na kisha hupewa huduma za
dharura za ARV zinazoitwa kwa kitaalamu Post-exposure prophylaxis.
Kwa kawaida mtu aliyebakwa au kujikata
hupewa dawa aina ya Lamivudine, Zerophidine au Truvada kulingana na uzito wa
tatizo.
“Tunatumia hizi dawa mara kwa mara
lakini tunafanya hivyo katika kliniki tofauti ili tusigundulike,” alisema mmoja
wao, mkazi wa Mwananyamala, Mariam Leshaniki.
Kwa maelezo ya Dk Rachel Baggaley,
mtaalamu wa masuala ya Ukimwi wa Shirika la Afya Duniani anasema dawa za PEP
zipo maeneo mengi duniani kwa sasa na zinafanya kazi kwa ufanisi pia hazina
madhara kwa mwanamke.
“Dawa hizi siyo sumu mwilini, zinaingia
kwenye mfumo wako wa damu kabla virusi havijajizatiti na inavizuia ili mradi
uzitumie ndani ya saa 72,” anasema Dk Baggaley.
Dawa ya Truvada, ambayo ina
mchanganyiko wa dawa aina ya Tenovofir na Emtricitabine, imethibitishwa kuwa
salama kwa kupunguza makali ya VVU pia kuzuia maambukizi mapya. Dawa hizi
zinazotengenezwa nchini India, zimekuwa msaada mkubwa wa tiba kwenye nchi
zinazoendelea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “DAWA YA TRUVADA YATUMIKA KUZUIA UKIMWI BADALA YA KONDOMU.”
Post a Comment