Tuesday, May 13, 2014

MBEYA CITY FC YAANGUKIA KUNDI LA KIFO CECAFA NILE BASIN, MWAMBUSI APANGA MAJESHI YAKE.




WAGONGA nyundo wa Mbeya, klabu ya Mbeya City fc imepangwa kundi B katika michuano mipya ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA)  ijulikanayo kwa jina la `CECAFA Nile Basin` inayotarajia kushika kasi kuanzia mei 22 hadi juni 4 mwaka huu nchini Sudan ikijumuisha timu 16.

Katika droo ya michuano hiyo iliyopangwa leo, Mbeya City imepangwa  na timu za AFC Leopards ya Kenya),  El Merreikh Al Fasher ya Sudan na  Elman ya Somalia.

Kundi A: El Merreikh ya Sudan, Victoria University ya Uganda, Malakia ya Sudan Kusini na Polisi ya Zanzibar.
Kundi:  Al Ahli Shandi ya Sudan, Al Masry ya Misri, Defence ya Ethiopia na  Dkhill  ya Djibouti.

Kundi D: Hey Al Arab ya Sudan, Arab Contractors ya Misri, Flambeau ya Burundi na Etincelles ya Rwanda.

Mbeya City fc wamepata nafasi ya kushiriki michuano hii baada ya mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara,  Azam fc kujiondoa.
Uongozi wa Mberya City kupitia kwa mwenyekiti wake Mussa Mapunda umesema nafasi hii ni adimu ,  hivyo watahakikisha wanajiandaa vizuri ili kuiwakilisha vizuri Tanzania.

Mapunda alisema nguvu waliyokuwa nayo katika michuano ya ligi kuu ndio wanaipeleka Sudan na tayari wachezaji waliopo Mbeya wameanza mazoezi ,  wengine walikuwa nje ya jiji hilo wakiendelea kuripoti.

Kocha wa Mbeya City fc, Juma Mwambusi kwa upande wake amefurahishwa na kupata ratiba mapema, hivyo anaanza kusuka kikosi chake mapema.

Mwambusi aliyeiongoza Mbeya City fc kushika nafasi ya tatu msimu uliopita anatarajia kuwadhihirishia watanzania kuwa klabu hiyo si ya kubeza.

Kwa mara ya kwanza, Mbeya City mwanzoni mwa mwaka huu walishiriki michuano ya kombe la Mapinduzi inayoshirikisha klabu kutoka nchi za Afrika Mashariki, lakini walitolewa mapema na waliporudi ligi kuu waliendeleza kasi yao.

Hii itakuwa mara ya pili kushiriki michuano inayoshirikisha timu za nje ya nchi kama ilivyokuwa kwa michuano ya Mapinduzi, hivyo wapenzi wa soka nchini Tanzania wana hamu ya kuiona Mbeya City ikifanya vizuri.

0 Responses to “MBEYA CITY FC YAANGUKIA KUNDI LA KIFO CECAFA NILE BASIN, MWAMBUSI APANGA MAJESHI YAKE.”

Post a Comment

More to Read