Tuesday, May 20, 2014
MWILI WA AMINA NGALUMA KUWASILI DAR IJUMAA HII
Do you like this story?
MWILI wa mwimbaji mahiri nchini
aliyefariki dunia wiki iliyopita nchini Thailand, Amina Ngaluma ‘Japanese’
unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Ijumaa wiki hii.
Kwa mujibu wa mume wa marehemu, Rashid
Sumuni tayari taratibu muhimu kuhusiana na kuuleta mwili huo nyumbani
zimefanyika na wana amini mambo yataenda kama wanavyotarajia.
“Naomba niwajulishe kuwa mwili wa mke
wangu utaondoka Thailand Alhamisi wiki hii kwa ndege ya KLM na utawasili Dar es
Salaam siku inayofuata saa tatu usiku.
“Tunaamini kama mambo yataenda kama
tulivyopanga baada ya mwili kuwasili basi Jumamosi tutamhifadhi mwenzetu. Msiba
upo kwa wazazi wa marehemu Kitunda, Machimbo, Dar es Salaam ambako ndiko maziko
yatafanyika.
“Kimsingi imekuwa ngumu kusema tutazika
lini, kwa sababu bado mwili haujaletwa, lakini tayari familia kwa kushirikiana
na sehemu alikokuwa anafanya kazi na Watanzania wengine waishio kule
tumeshamaliza taratibu zote zilizokuwa zikihitajika ili kuuleta mwili nchini,”
alisema Sumuni kwa masikitiko.
Pia alivishukuru vyombo vya habari kwa
kuwa karibu na familia yao wakati wa kipindi hiki kigumu, lakini akiomba
wanapotaka kutoa habari kuhusiana na msiba huo wawasiliane na wahusika wa
familia ili kupata taarifa sahihi zaidi.
Ngaluma aliyepata kung’ara na bendi
mbalimbali nchini, alifariki dunia Alhamisi iliyopita kwa shinikizo la damu
akiwa Thailand alikokuwa akifanya shughuli za muziki katika bendi ya Jambo
Survivor.
Wakati wa uhai wake alitamba na bendi
mbalimbali zikiwemo African Revolution ‘Tamtam’, Double M Sound
‘Mshikemshike’ na TOT Plus zote za Dar es Salaam.
Pia alipigia makundi ya Arusha Sangoma,
Sayari Band na Less Mwenge yote ya Arusha na Mangelepa na Sky Sound za Kenya.
Pia amepata kufanya shughuli za muziki kwa miezi sita nchini Uganda.
Baadhi ya nyimbo alizotunga wakati wa
uhai wake ni Manyanyaso Kazini na Mapendo alizotunga akiwa Tamtam, wakati
Double M Sound alitunga nyimbo za Wajane na Ukewenza.
Pia alitoa albamu yake binafsi iitwayo Jitulize yenye nyimbo kama Vidonge, Pete ya Uchumba, Good Night, Uombalo Hutopata, Jitulize na Mzigo wa Moto.
Baadhi ya nyimbo alizopata kuimba na
kumpatia umaarufu mkubwa ni Mgumba, Maisha Kitendawili, Ndugu Lawama,
Zawadi ya Watanzania, Ugumu wa Maisha na Call Box zote zikitungwa na Muumin
Mwinjuma ‘Kocha wa Dunia’. Mungu amuweke mahali pema peponi. Amin.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MWILI WA AMINA NGALUMA KUWASILI DAR IJUMAA HII”
Post a Comment