Sunday, May 18, 2014
POLISI WANASA MTANDAO WA WATU WANAOSAFIRISHA WASICHANA KWENDA CHINA KUWATUMIKISHA KINGONO
Do you like this story?
BAADA ya kuwepo malalamiko ya wasichana wadogo wa nchini kusafirishwa kwenda China kutumikishwa katika biashara ya ngono pamoja na dawa za kulevya, sasa serikali imenasa mtandao huo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mathias Chikawe alitoa taarifa hiyo juzi bungeni wakati akihitimisha michango
kuhusu bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2014/15 iliyopitishwa.
Chikawe ambaye hata hivyo hakufafanua
kwa undani wa mtandao huo ulivyokamatwa, alieleza Bunge namna watoto hao
wanavyopatikana kabla ya kufikishwa nchi hiyo ya nje.
Kwa mujibu wa Waziri, watu hao wamekuwa
wakichukua watoto wadogo na kuwaambia kwamba wanawapeleka China hususani mji wa
Guanzhou kuwaajiri kwenye saluni na maduka.
Alisema kinara wa usafirishaji amekuwa
akitambuliwa kwa jina la ‘Mama’ ambaye baada ya kufika nchini humo,
huwanyang’anya watoto hao hati zao za kusafiria. Imebainika zipo hata wakala
zinazojihusisha na biashara hiyo haramu ya binadamu.
“Wakifika, Mama anawanyang’anya
pasipoti zao. Anawaambia ili kuwarudishia, lazima watimize masharti ya kumpa
kati ya dola 8,000 na 10,000 baada ya kutumika katika vitendo vya ngono,” alisema Waziri
Chikawe.
Aliendelea kueleza kuwa wanaposhindwa
kutimiza masharti hayo, hukutana na Wanigeria ambao huwapa hati bandia za
kusafiria na kisha kuwaingiza katika biashara ya kusafirisha dawa za kulevya
kwenda nchi mbalimbali.
“Tumenasa mtandao huu…polisi imenasa
mtandao,” alisema Waziri na kutoa mfano kwamba hivi karibuni, alikamatwa mtu
akiwa na hati ya kusafiria akimpelekea binti mmoja. Alisema binti huyo
alipoulizwa juu ya hati hiyo, alikuwa hafahamu anakokwenda.
Awali, taarifa juu ya kuwepo
usafirishaji wa wasichana wadogo kwenda China kwa ajili ya kutumikishwa katika
ngono, ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe baada ya kutoka ziarani nchini humo.
Membe alisema serikali inashirikiana na
ubalozi wa China katika kubaini wahusika wa biashara hiyo sanjari na mkakati wa
kuhakikisha wasichana hao wanarudishwa nchini.
Akielezea mikakati ya serikali katika
kukabili biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, Waziri Chikawe alisema
katika mwaka wa fedha 2013/2014 Sekretarieti ya kupambana na biashara hiyo
imeratibu vikao vinne vya Kamati ya kupambana nayo.
Aidha imeandaa kitabu cha anuani na
majina ya watoa huduma kwa waathirika wa biashara haramu ya usafirishaji
binadamu na vilevile kutengeneza rasimu ya kanuni za sheria ya kupambana na
biashara hiyo nchini.
Katika mwaka wa fedha 2014/2015
sekretarieti itakamilisha kutengeneza kanuni za Sheria ya kupambana na biashara
hiyo ya mwaka 2008. Pia itatoa elimu na kuimarisha mikakati ya kupambana na
biashara hiyo ya kusafirisha binadamu.
Watanzania zaidi ya 100 wakiwemo
wasichana 20 wamedaiwa wapo gerezani nchini China wakijihusisha na biashara ya
dawa za kulevya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “POLISI WANASA MTANDAO WA WATU WANAOSAFIRISHA WASICHANA KWENDA CHINA KUWATUMIKISHA KINGONO”
Post a Comment