Sunday, May 18, 2014

JOHN BOCCO ATIKISA NYAVU NA KUIPA TAIFA STARS USHINDI WA 1-0 DHIDI YA ZIMBABWE




BAO pekee la mshambuliaji, John Raphael  Bocco `Adebayor` limeipa ushinda taifa Stars dhidi ya Zimbabwe katika mchezo wa raundi ya awali kabisa kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kushindania  tiketi za kushiriki kombe la mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco.

Bocco alifunga bao hilo katika dakika ya 13 kwa kumalizia pasi nzuri ya Thomas Ulimwengu.
Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, Taifa stars walionesha uwezo mzuri, lakini Zimbabwe nao hawakuwa wabaya.

Kukaa nyuma kwa wachezaji wa Zimbabwe kuliwasaidia kuokoa hatari nyingi langoni mwao.
Tatizo kubwa kwa stars lilikuwa ni viungo wake, Frank Domayo na Mwinyi Kazimoto  kushindwa kupiga pasi za kupenyeza, hivyo kuwalazimisha John Bocco, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samata kugeuka na kuchukua mipira kwa nyuma na kwenda mbele.

Aina hii ya mpira ilipunguza  kasi ya mashambulizi na kuwafanya Zimbabwe wacheze kwa kujiamini na kuona wanawaweza Taifa stars.

Sehemu ya ulinzi wa kati ya Taifa stars  ilikuwa nzuri, lakini beki wa kulia, Shomary Kapombe hakuwa katika kiwango chake na inawezekana ni kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu. Naye Oscar Joshua kwa upande wa kushoto alicheza vizuri , lakini alikuwa mzito kidogo.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo dakika ya kwanza tu Taifa stars walikosa bao, nao Zimbabwe wakakosa goli.

Dakika moja baadaye John Bocco `Adebayor ` alikosa nafasi nyingine baada ya kushindwa kumalizia krosi ya chinichini.

Bado tatizo la Stars lilikuwa kukosa umakini wanapofika langoni mwa Zimbabwe.
Mbwana Samata na John Bocco kwa nyakati tofauti walishindwa kuzibadili nafasi muhimu kuwa magoli na kuipa Stars kazi ngumu katika mchezo wa marudiano mjini Harare nchini Zimbabwe.

Mzani wa mpira katika kipindi hiki cha pili ulikuwa sawa, lakini Zimbabwe walioneka kuwa na mipango mizuri zaidi.
Hawakujibana katika eneo lao kama kipindi cha kwanza, walifunguka na kwenda mbele na kuifanya Taifa stars ihangaike.

Kwa soka walilocheza Zimbabwe kipindi cha pili wameonesha kuwa wanao uwezo wa kubadilika na kucheza kulingana na mazingira.

Ni dhahiri kwa wiki mbili zinazokuja kabla ya kwenda Zimbabwe, kocha Mart Nooij anatakiwa kufanya maandilizi mazuri zaidi kwasababu inaonekana mechi itakuwa ngumu.
Zimbabwe hawatakuwa na sababu ya kujibana langoni mwao, watashambulia kwa muda wote ili kufuta matokeo ya leo.

Moja ya kanuni ya mpira ni kumfunga magoli mengi mpinzani wako ukiwa nyumbani kwani siku zote ugenini mchezo huwa ni mgumu.

Hata hivyo, Taifa stars wanastahili pongezi kwa matokeo ya leo kwani kimfaacho mtu chake.

Huwezi kujua nini kitatokea Harare kwasababu hata Stars wanaweza kushinda pia.

0 Responses to “JOHN BOCCO ATIKISA NYAVU NA KUIPA TAIFA STARS USHINDI WA 1-0 DHIDI YA ZIMBABWE”

Post a Comment

More to Read