Saturday, May 31, 2014

WATOTO WATATU WAFUNGIWA NDANI MWEZI MMOJA KWA HOFU YA KUBAKWA IRINGA.


Huyu ndiye mama aliyefungia watoto wake, Eva Mdamu

Kushoto ni mwandishi wa habari wa Kwanza Jamii Mathias Canal, katikati ni Rajabu Michael Kigwamke Baba wa mtoto aliyelawitiwa, kulia ni Mwandishi wa habari wa Nuru Fm Victor Meena

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Tanangozi Bi Lucy Msigwa akitupa taaarifa ya tukio hilo.

Katikati ni Juma Msungu kijana anayetuhumiwa kwa ubakaji na kulawiti akitupa maelezo kuhusu tukio hilo.

Na Mathias Canal
Tukio hilo limetokea hivi karibuni katika kijiji cha Tanangozi kata ya Mseke Wilaya ya Iringa Vijijini, Mkoani Iringa ambapo mama aliyefahamika kwa jina la Eva Mdemu anayefanya biashara ndogo ndogo kijijini hapo alikutwa akiwa amewafungia watoto hao ndani ya nyumba yake kwa takribani mwezi mmoja.

Mama huyo amesema kuwa sababu iliyopelekea kuwafungia watoto hao katika chumba kichafu ambacho hutumika pia kwa haja kubwa na ndogo kwa watoto hao, ni kutokana na hofu ya kubakwa kwa watoto hao, ambao takribani miezi saba iliyopita mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka 10 alibakwa, na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 4 alilawitiwa na kijana aliyefahamika kwa jina la Juma Msungu mkazi wa Tanangozi mwenye umri wa miaka 20.

Eva amekiri kuwafungiwa watoto hao na kuwapa chakula dirishani, hata hivyo amesema kuwa yeye ni mama wa watoto sita ambao baba zao wote hawatoi huduma kwa watoto hao, na huwafungiwa pale anapoondoka kwa ajili ya kwenda kwenye biashara yake ambayo ndiyo inayomuwezesha kuwahudumia watoto hao.

Hata hivyo Eva amesema kuwa baadhi ya wanakijiji wamekuwa wakimtishia kumhamisha katika kijiji hicho huku Rajabu Michael Kigwamke ambaye ni baba wa mtoto aliyelawitiwa amemchukua mtoto huyo kwa lazima kutokana na kuogopa kupatwa na  magonjwa malimbali yanayoshabihana na uchafu, wakati hajawahi kumhudumia mtoto huyo tangu alipomzaa miaka sita iliyopita.

Sambamba na hayo mama huyo ameiomba serikali kumsaidia kutokana na adha kubwa aliyonayo ya kubakwa kwa watoto wake huku mtuhumiwa wa kesi hiyo ya ubakaji akiwa ameachiwa huru baada ya kuwa kizuizini takribani miezi sita tu.

Kwa upande wao wananchi waliojitokeza kwenye adha hiyo ambayo ilihudhuriwa na viongozi wa kijiji, wamekiri kufungiwa ndani kwa watoto hao ambao walikuwa  kwenye chumba chenye uchafu uliokithiri.

Sambamba na hayo wanakijiji hao wamesema kuwa mama huyo anajihusisha na mambo ya kishirikina, kwani ameanza muda mrefu kuwafungia watoto hao japo wakati Juma akiwa ameshikiliwa na jeshi la polisi watoto hao waliendelea kubakwa ndani kwao huku milango yote ikiwa imefungwa na kufuli.

Rajabu Michael Kigwamke ambaye ni baba wa mtoto huyo aliyewahi kubakwa alikanusha kutomhudumia mtoto huyo na kudai kuwa amekuwa akishirikiana na mke wake huyo katika baadhi ya huduma ikiwa ni elimu pamoja na mavazi.

Kigwamke amesema kuwa baada ya kupata taarifa ya kubakwa na kulawitiwa kwa watoto hao aliamua kumkamata Juma Msungu mtuhumiwa wa tukio hilo ila ajabu ni pale ambapo mtuhumiwa huyo alikuwa kizuizini lakini bado watoto hao waliendelea kubakwa.

Hata hivyo Juma Msungu kijana mwenye umri wa miaka 20 anayetuhumiwa kwa kulawiti na ubakaji wa watoto wa mama huyo, yeye amesema kuwa hajawahi kujihusisha na tukio hilo japo amekiri kukamatwa na kufungwa miezi sita.

Juma aliongeza kuwa kipindi ambacho yeye alikuwa gerezani watoto hao waliendelea kubakwa kitendo ambacho kimemuumiza sana kutokana na kufungwa pasipo sababu ya msingi, huku akiendelea kupata adhabu ya kuripoti katika mahakama ya Wilaya ya Iringa.

Aidha akitoa taarifa hiyo Afisa Mtendaji wa kijiji cha Tanangozi Bi Lucy Msigwa alisema kuwa tarehe 26 mwezi huu wa tano alipigiwa simu na mgambo wa kijiji Bw Rajabu Michael Kigwamke kwamba kuna watoto wamefungiwa ndani ya nyumba yake na  baada ya kufika katika eneo la tukio aliwakuta watoto hao wakiwa wamefungiwa ndani huku wakiwa uchi wa mnyama, watoto hao walikuwa watatu, wawili ni mapacha wana umri wa miaka 2 na Yule ambaye ni mkubwa ana miaka 5.

Afisa mtendaji alimuamuru balozi kuufunga ule mlango na kuwachukua watoto hao kwenda nao hadi ofisi za serikali ya kijiji hadi pale alipofika mama huyo na kukiri kuwafungia watoto hao kutokana na kuogopa watoto wake kuendelea kubakwa hivyo aliamua kumkabidhi mtoto mmoja wa kiume kwa baba yake.

0 Responses to “WATOTO WATATU WAFUNGIWA NDANI MWEZI MMOJA KWA HOFU YA KUBAKWA IRINGA. ”

Post a Comment

More to Read