Saturday, May 31, 2014
ASILIMIA 25 YA WALIMU HUFUNDISHA "MAKOROKOCHO"
Do you like this story?
Wakati
Serikali ikiahidi kuboresha elimu nchini kwa kuhakikisha inaajiri walimu wa
kutosha, imebainika kuwa asilimia 25 ya walimu huwafundisha wanafunzi mambo
yasiyo ya msingi.
Ripoti
ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco),
iliyozinduliwa Dar es Salaam hivi karibuni, imebainisha kuwa wakati wananchi
wakilalamika kuwa elimu inayotolewa haimsaidii mwanafunzi kupata ajira nzuri,
wanafunzi hawajifunzi mambo ya msingi yatakayowasaidia kupambana na changamoto
za maisha.
Akizindua
ripoti hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema
kuwa ripoti hiyo imeweka wazi ukubwa wa tatizo la ufundishaji, akieleza kwamba
jumla ya watoto milioni 250, duniani wanakosa mafunzo ya msingi ya kusoma,
kuandika na kuhesabu, ingawa wanaingia darasani.
“Tanzania
kama sehemu ya dunia, haijakwepa tatizo hilo. Baadhi ya watoto wetu wamekuwa
wakimaliza shule za misingi bila ya kuwa na ujuzi huo. Hii ni hali ya kushtua,
inayohitaji nguvu za pamoja za wadau wote wa elimu duniani,” alisema Kawambwa.
Alibainisha
kwamba ripoti hiyo imependekeza mpango wa elimu mwaka 2015, uzingatie ubora
utakaotokana na mipango sahihi inayotekelezeka akitaka tatizo la walimu
lipatiwe ufumbuzi wa kudumu kwa lazima ili kuwanusuru wanafunzi.
“Kama
suala la walimu halitapatiwa ufumbuzi sasa, tofauti kwenye ufundishaji
itakuwepo kwa vizazi vingi huku ikitoa tafsiri mbaya dhidi ya jitihada za
kuondoa umaskini duniani na kufikiwa kwa maendeleo endelevu,” alisema Dk
Kawambwa.
Aliongeza
kuwa kwa namna hali ilivyo sasa, Serikali inalazimika kuhakikisha inaajiri
walimu wenye dhamira ya kweli ya kufundisha na kutoa elimu bora.
Ripoti
ya Unesco inaeleza kuwa licha ya kuwepo kwa mafanikio ya kuridhisha katika
kipindi cha miaka kumi iliyopita, wananchi masikini ndiyo walioathirika zaidi
na tatizo la utoaji elimu mbaya sababu ikiwa kutokuwepo kwa walimu wenye
mafunzo ya kutosha.
Unesco
ilisema kuwa kutokana na matatizo ya walimu, wanafunzi 130 milioni wanaosoma
shule za msingi duniani, hawana uwezo wa kusoma hata sentensi moja, jambo
linalowafanya washindwe kujiunga na sekondari.
“Matatizo
ya elimu siyo tu yanaathiri malengo ya watoto ya baadaye, lakini pia uchumi wa
Serikali hizo. Gharama ya watoto 250 milioni kutosoma elimu ya msingi ni Dola
129 bilioni za Marekani,(Sh 212.85 bilioni), ambayo ni asilimia kumi ya
matumizi ya dunia katika elimu,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti
hiyo imelinukuu shirikali lisilo la Serikali la Uwezo, linaloeleza kuwa
asilimia 26 ya wanafunzi wa darasa la tatu ndiyo wanaoweza kusoma vizuri
hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili.
Akizungumza
na gazeti hili kuhusu takwimu hizo, Mratibu wa Uwezo-Taifa, Zaida Mgalla
alisema kuwa asilimia 44 ya wanafunzi wa darasa la tatu walifaulu jaribio la
hisabati la darasa la pili, huku asilimia 11 pekee wakifaulu kusoma hadithi ya
Kiingereza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ASILIMIA 25 YA WALIMU HUFUNDISHA "MAKOROKOCHO"”
Post a Comment