Monday, May 12, 2014
WAUGUZI WENYE VYETI FEKI WAFUKUZWA KAZI MKOANI MARA.
Do you like this story?
SERIKALI
mkoani Mara imewatimua kazi wauguzi ‘vihiyo’ sita waliobainika kuwa na vyeti
vya kughushi.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara,
Balthazar Kichimba, amethibitisha tukio hilo, wakati akihojiwa na Tanzania
Daima
ofisini kwake juzi.
“Kweli kuna wauguzi ambao wameghushi
vyeti vya shule na Serikali ya Mkoa wa Mara kupitia Katibu Tawala ambaye ni
mamlaka ya ajira, tayari imewafukuza kazi wauguzi sita wa afya waliokuwa
wakifanya kazi katika hospitali ya serikali baada ya kubainika kwamba
wameghushi vyeti vyao vya kidato cha nne,” alisema Kichinda.
Wauguzi hao wanadaiwa kupata ajira kwa
kudanganya elimu yao ya sekondari, hivyo kupata mafunzo ya uuguzi na kuajiriwa
na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kama wauguzi.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania
Daima
umebaini wengi wa watumishi hao walioajiriwa mwaka 2008/2009 wana elimu ya
darasa la saba, lakini wameghushi vyeti vya kidato cha nne vilivyowawezesha
kupata nafasi za mafunzo ya uuguzi katika vyuo mbalimbali mkoani Mara.
Mkoa wa Mara una vyuo vikubwa vitatu
vya uuguzi ambavyo ni Kisare Hospitali Teule ya Nyerere DDH mjini Mugumu
wilayani Serengeti na Shirati KMT wilayani Rorya ambavyo vyote vinamilikiwa na
Kanisa la Menonite Tanzania pamoja na chuo cha Musoma kinachomilikiwa na
serikali katika hospitali ya Mkoa wa Mara.
Alisema baada kuwafukuza, serikali
imewakabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru)
Mkoa wa Mara kwa ajili ya kuwachukulia hatua za kisheria.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mara,
Joseph Holle, alikiri ofisi yake kukabidhiwa watumishi hao na kwamba taratibu
za kisheria zimeanza kuandaliwa, ili waweze kuwafikisha mahakamani.
“Baada ya mamlaka ya ajira kuchukua
hatua sasa kazi yetu kubwa hapa ni kuandaa mashitaka ya jinai dhidi yao,”
alisema Holle.
Alisema watumishi hao walibainika baada
ya taarifa za siri kutoka kwa watu na uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo
ambao walifuatilia nyendo za watumishi hao.
“Tulipokuwa pale hospitalini kwa ajili
ya kazi maalumu ya kusimamia ukusanyaji wa mapato tulibaini kuwepo kwa baadhi
ya watumishi wanaotoa kauli zinazokwenda kinyume cha maadili ya kazi hiyo,
hivyo tukabaini kuna watu hawana maadili hatua ambayo ilituwezesha kuwakamata
hawa na tulichukua vyeti vyao na kupeleka Baraza la Mtihani ikabainika vyeti
vyao ni feki,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAUGUZI WENYE VYETI FEKI WAFUKUZWA KAZI MKOANI MARA.”
Post a Comment