Saturday, May 17, 2014
WEREMA ALIKOROGA, ALINYWA, ALINYWA :ATOA KAULI YA KUWABAGUA WAZANZIBARI
Do you like this story?
Kwa
maneno ya siku hizi ni kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick
Werema ‘amelikoroga na kulinywa mwenyewe’, baada ya jana kutoa kauli ya kuudhi
alipomtaka mbunge kutoka Zanzibar akaulize swali lake visiwani humo,
iliyosababisha baadhi ya wabunge kususia Bunge na kutoka.
Kauli
iliyoonyesha kuwagawa wabunge katika mafungu mawili; wa bara na Zanzibar,
ilimlazimu Jaji Werema baadaye kusimama bungeni na kuwaangukia akiwaomba radhi
waliokerwa na kauli yake na pia kuliomba radhi Bunge, Spika wake, Anne Makinda
na wananchi.
Kuondoka
kwa wabunge hao kulitokana na mwongozo wa Spika ulioombwa na Mbunge wa Ole
(CUF), Rajabu Mbarouk Mohamed kutokana na majibu Jaji Werema kwa mbunge wa
Mkanyageni (CUF), Habibu Mnyaa aliyekuwa ameomba ufafanuzi wakati Bunge
lilipokaa kama kamati ya kupitisha vifungu vya Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2014/15.
Mnyaa
amesema Wizara ya Katiba na Sheria ni muhimu lakini imekuwa ndiyo ya kwanza
kuvunja sheria na haki za binadamu na akataka ufafanuzi.
Hata
hivyo, aliposimama kujibu swali hilo, Jaji Werema alimwambia Mnyaa kuwa mambo
mengine akaulize Zanzibar na siyo katika Bunge la Jamhuri kwa kuwa si kila kitu
kitaulizwa ndani ya Bunge hilo.
“Alichokizungumza
Mnyaa ni sahihi lakini hapa si mahali pake, namshauri kuwa akaulize huko
Zanzibar kwenye vikao vyao hapa sisi hatuna majibu,” alisema Werema.
Mara
baada ya Bunge kurejea, Mbarouk aliomba mwongozo wa Spika akitaka ufafanuzi wa
kauli hiyo kwamba ilikuwa ya kibaguzi.
“Mheshimiwa
Spika, huu ni ubaguzi na haupaswi kufanywa na mtu msomi kama Mwanasheria Mkuu
wa Serikali,” alisema Mbarouk.
Amesema
ubaguzi huo umewabagua wabunge ambao wamekula kiapo cha kulitumikia Bunge la
Jamhuri ya Muungano na unaonyesha namna ambavyo Wazanzibari wanabaguliwa.
“Mheshimiwa
Spika, yanapofanyika mambo kama hayo na wewe mwenyewe uko hapa unaona ni sawa
na kubariki jambo hilo, huu ni ubaguzi unaoufanya wewe kwa kuwa lilifanyika
ukiona bila hata ya kukemea,” alisema Mbarouk.
Hata
hivyo, Spika alipinga na kusema: “Hakuna mwongozo wowote kwa kuwa hata wewe
umevunja sheria kwani hata nilipokuambia kaa chini umeendelea kuzungumza,
tunaendelea.... Katibu (akimtaka Katibu wa Bunge kutoa mwelekeo wa shughuli
iliyokuwa inafuata ambayo ilikuwa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).”
Baada
ya kauli ya Spika, wabunge wa Zanzibar walihamasishana na kuamua kutoka nje kwa
wakati mmoja na huku wenzao wa upinzani wakiendelea kutafakari cha kufanya.
Wakati huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alikuwa akisoma
hotuba yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WEREMA ALIKOROGA, ALINYWA, ALINYWA :ATOA KAULI YA KUWABAGUA WAZANZIBARI”
Post a Comment