Friday, June 20, 2014
UBUNGO MATAA KUFUNGWA KUPISHA UJENZI WA BARABARA.
Do you like this story?
KAMPUNI ya ujenzi ya
Strabag
inayojenga barabara ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) imetangaza
mabadiliko ya muda katika eneo la Ubungo jijini Dar es salaam kuanzia kesho na
kesho kutwa usiku kutokana na ujenzi unaoendelea wa barabara.
Akiongea na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Bwana Yahya Mkumba,
alisema kazi hiyo itahusu ujenzi katika makutano ya barabara za
Morogoro, Sam
Nujoma na Nelson Mandela katika eneo la
Ubungo.
Alisema ujenzi huo utakaoanza leo
utasababisha kufungwa kwa baadhi ya njia katika barabara hizo kuanzia saa nne
usiku hadi saa 12 asubuhi keshokutwa Jumamosi.
Akielezea zaidi alisema katika awamu ya
kwanza ujenzi huo utahusisha eneo la upande wa kulia la makutano la barabara ya
Sam Nujoma na Morogoro ambalo litafungwa.
“Hali hii itasababisha magari
yanayotoka maeneo ya Buguruni na Tabata kuelekea maeneo ya Mwenge kutoweza
kutumia njia ya Sam Nujoma watakapofika taa za Ubungo,” alisema.
Alifafanua kuwa magari hayo yatalazimika
kufuata alama zitakazowaelekeza kupita katika barabara za mradi zinazojengwa
hadi barabara ya Shekilango ambapo wataweza kukutana tena na Sam Nujoma kwa
kutumia barabara ya Igesa.
Pia magari yatakayokuwa yanatokea Sinza
kupitia barabara ya Igesa hayataweza kuelekea eneo la Ubungo yatakapofika
katika makutano ya barabara za Igesa na Sam Nujoma.
Alifafanua kuwa magari yanayotumia
barabara ya Morogoro kutokea maeneo ya Mbezi na Kimara yatalazimika kuchepuka
kulia na kutumia barabara za mabasi ya mwendo wa haraka yatakapofika eneo la
Kibo ambapo patakuwa na kizuizi.
Bw. Mkumba alisema katika awamu ya pili
ya ujenzi huo, eneo la upande wa kushoto la makutano ya barabara za Morogoro na
Nelson Mandela litafungwa siku ya Jumamosi kuanzia saa nne usiku hadi saa 12
asubuhi siku ya Jumapili.
Katika awamu hii, alisema, watumia
magari yatakayokuwa yanatokea eneo la Mwenge kutumia barabara ya Sam Nujoma
yatalazimika kuchepuka kushoto kukamata barabara ya Igesa kisha Shekilango.
Pia magari yatakayokuwa yanatokea
barabara ya Nelson Mandela na kutaka kuelekea mjini kwa kutumia njia ya
Morogoro yatalazimika kuchepuka kushoto na kwenda kugeukia eneo la Kibo ili
kuikamata barabara ya Morogoro.
“Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote
utakaotokea,” alisema Bwana Mkumba na kuongeza kuwa pamoja tunajenga na hivyo
usumbufu utakuwa ni wa muda mfupi.
Mradi wa Mabasi yaendayo haraka
unatarajiwa kuondoa adha ya foleni katika jiji hilo na kuleta ufanisi wa
usafiri.
Ubungo Tabata Diversion
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “UBUNGO MATAA KUFUNGWA KUPISHA UJENZI WA BARABARA.”
Post a Comment