Wednesday, July 9, 2014

CHUO FEKI CHA UUGUZI CHAFUNGWA NA MKUU WA WILAYA, WANAFUNZI WAHAHA KUJUA HATMA YAO.




Na Daniel Makaka, Sengerema
MKUU wa wilaya ya Sengerema, Bi Kalen Yunus amekifunga chuo cha uuguzi cha Huruma ya Mungu Yatosha baada ya kukiukwa kwa taratibu za usajili.

Mkuu huyo aliamua kukifunga chuo baada ya kupata taarifa za chuo hicho kuendeshwa bila usajili.

Pamoja na kufungwa kwa chuo hicho, wanafunzi wake wanaiomba serikali iwasaidie kurejeshewa fedha walizotoa katika chuo hicho kutokana na mwenye chuo kuwadanganya kuwa kimesajiliwa wakati akijua si kweli.

Wamesema walijiunga hapo baada ya kuona matangazo mbali mbali kuhusu chuo hicho kuwa kinatoa mafunzo ya uuguzi na maabara na kwamba inachukua watu wa kidato cha nne bila kujali matokeo.
Baada ya kupata matangazo hayo yaliyokuwa na namba za simu waliamua kupiga simu ili kupata maelekezo juu ya kujiunga na chuo hicho maelekezo waliyopewa ni kufika chuoni wakiwa na karo pamoja na fedha kwa ajili ya sale za shule.

Wamefafanua kuwa baada ya kufika chuoni hapo , kata ya Nyehunge wilayani humo mazingira ya chuo hicho yalikuwa na utata kutokana na kutokuwa na madarasa ya kutosha na wakazi wa maeneo hayo kutokuwa na taarifa ya  uwapo wa chuo hicho na kuwashangaa wanafunzi hao.

Wamefafanua kuwa baada ya kukaa kwa muda mfupi mabadiliko mbali mbali yalikuwa yanafanyika katika chuo hicho huku wanafunzi wakifukuzwa pasipo utaratibu kitendo ambacho kiliwatia shaka.

Aidha chuo hicho kilikuwa na mwalimu mmoja tu aliyekuwa anafundisha tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013.
Pia wamesema kuwa baada ya kujua kuwa chuo hicho bado hakijasajiliwa walimwomba mmiliki wake  kuzungumza nao ili kupata mwafaka wa swala hilo lakini alikata katakata na kuwatishia kuwafukuza endapo wakiendelea kumfuatafuata.

Kwa upande wake mmiliki wa chuo hicho Bw, Ballu  Clavery amekiri wazi kuwa chuo hicho hakijasajiliwa na alitumia namba ya zahanati iliyokuwa inamilikiwa na mjomba wake ili kuanzisha  chuo hicho.

Hata hivyo alivyoulizwa na waandishi wa habari juu ya hatima ya wanafunzi hao amesema kuwa  atakaana nao ili waweze kupata ufumbuzi wa suala hilo.

0 Responses to “CHUO FEKI CHA UUGUZI CHAFUNGWA NA MKUU WA WILAYA, WANAFUNZI WAHAHA KUJUA HATMA YAO.”

Post a Comment

More to Read