Monday, July 14, 2014

IPTL YAMFUNGULIA KESI KAFULILA, YAMTAKA AOMBE RADHI NA KULIPA FIDIA YA BILIONI 310.



Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), imemfungulia kesi Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ikimtaka aombe radhi na kulipa fidia ya Sh bilioni 310.

Katika kesi hiyo ya madai, Kafulila anadaiwa kuidhalilisha kampuni hiyo, kutokana na kauli alizotoa dhidi yake (IPTL).

IPTL na walalamikaji wengine Pan Africa Power Solution (PAP) na Mkurugenzi wa PAP, Harbinger Seth wanamlalamikia Kafulila kuwatuhumu kuchukua fedha kinyume cha sheria katika akaunti ya Escrow iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Walalamikaji hao kupitia kwa Wakili wao, Augustine Kusalika wamefungua kesi hiyo, wakitaka Kafulila awalipe Sh bilioni 210 kama fidia ya kutoa kauli za udhalilishaji,  kuwasababishia hasara katika biashara na kuharibu mtazamo wa biashara zao.

Aidha, wanaiomba Mahakama iamuru Kafulila, awaombe radhi, pia awalipe Sh bilioni 100 kama hasara ya jumla pamoja na usumbufu walioupata, kutokana na kauli za udhalilishaji.

Kwa mujibu wa hati ya madai,  iliyopatikana mwishoni mwa wiki,  Juni mwaka huu Kafulila alitangaza kuwa IPTL na Seth, walijipatia fedha kutoka akaunti ya Escrow kinyume cha sheria na kumuita Seth ni 'Singasinga',  jambo lililomdhalilisha na kumharibia muonekano wake na biashara yake.

Walalamikaji hao wanadai kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii,  bila kuwa na haki, Kafulila alitoa taarifa hizo, kuwa IPTL inajihusisha na biashara zisizo halali na za uongo, jambo lililosababisha jamii kuamini na kuwaharibia mtazamo wa kibiashara.

Aidha, wanadai  Kafulila akiwa mbunge alipoteza kinga ya wabunge inayowalinda wakizungumza bungeni, kwa kuwa alitoa taarifa hizo nje ya shughuli za Bunge.

Walidai Kafulila anaendelea kutoka taarifa hizo,  licha ya kumpa taarifa kwa maneno na maandishi, wakimtaka kuacha kufanya hivyo, kwa kuwa anawaharibia biashara kitaifa na kimataifa.

Kwa mujibu wa hati ya madai, IPTL iliingia mkataba na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye shirika hilo, lakini kulitokea mgogoro kati ya IPTL, Kampuni ya VIP Engineering and Marketing na Tanesco, jambo lililosababisha wafike Mahakama Kuu.

Kutokana na mgogoro huo, Mahakama iliamuru Sh bilioni 200 zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow, zisitolewe hadi kesi hiyo itakapokwisha na  baada ya kesi kuisha, Mahakama iliamuru IPTL ichukue fedha hizo.

Walalamikaji hao wanadai licha ya Kafulila, kujua kuwepo kwa mgogoro huo, aliendelea kutoa tuhuma hizo, huku akijua kuwa IPTL imechukua fedha hizo kwa amri halali ya Mahakama.

Wakili huyo alisema wateja wake, wanaiomba Mahakama iamuru Kafulila awalipe Sh bilioni 310 kama fidia, aombe radhi, alipe gharama za uendeshaji wa kesi hiyo na amri nyingine, ambazo Mahakama itaona zinafaa.

0 Responses to “IPTL YAMFUNGULIA KESI KAFULILA, YAMTAKA AOMBE RADHI NA KULIPA FIDIA YA BILIONI 310.”

Post a Comment

More to Read