Wednesday, July 23, 2014
TFF HII TABIA YA KUONGEZA MUDA WA USAJILI NA KUPIGA KALENDA LIGI KUU ITAISHA LINI?.
Do you like this story?
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) jana limetangaza kuongeza muda wa usajili kwa wiki mbili ili kuzipa klabu
nafasi ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa.
Katika taarifa yake, TFF ilisema hatua
ya kwanza ya usajili inakamilika Agosti 17 mwaka huu badala ya Agosti 3 ya
awali.
Kutokana na marekebisho hayo, kipindi
cha uhamisho kinakamilika Agosti 17 mwaka huu wakati pingamizi itakuwa kati ya
Agosti 19 hadi 26 mwaka huu.
Pia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
itathibitisha usajili kati ya Septemba 1 na 2 mwaka huu.
Uhamisho wa kimataifa, usajili wa
wachezaji huru, na utatuzi wa dosari za usajili unatakiwa uwe umekamilika
kufikia Septemba 7 mwaka huu. Uthibitisho wa hatua ya mwisho ya usajili
utafanywa Septemba 15 mwaka huu.
Kwa upande wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
msimu wa 2014/2015 itaanza Septemba 20 mwaka huu, na ratiba itatolewa mwezi
mmoja kabla ya kuanza ligi hiyo.
Utaratibu huu wa kuongeza-ongeza muda
umezoeleka nchini Tanzania na kufikia hatua kuonekana kama ni ‘kasheria’
fulani. Mazoea hujenga tabia, ‘walishasemaga’ wazee wa zamani. Moja ya kanuni
ya maisha ni kuzingatia muda na kufuata mipaka uliyojiwekea.
Kama umepanga kufanya kazi kwa saa nne,
basi ikifika muda huo inabidi uache, labda kama kumetokea sababu ya msingi,
hapo unaweza kuongeza muda zaidi.
Barani ulaya, sheria zinaheshimika sana
ikiwemo hii ya dirisha la usajili. Siku zote sipendi kuifananisha Tanzania na
Ulaya, hatuwezi kuwa kama wao, lakini kuna vitu vyepesi vya kuwaiga kama hili la
kwenda na muda.
TFF wanaongeza muda wa usajili na
ukisoma sababu yao ni kuzipa klabu nafasi ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa.
Kwani klabu haziwezi kukamilisha taratibu hizo ndani ya muda uliopangwa? lazima
ziongezewe muda?
Ni jambo rahisi tu kubaki katika
misingi ya kanuni ili tuepukane na mazoea. Naamini wapo viongozi wa klabu huwa
hawahangaikii usajili ndani ya muda uliopangwa kwasababu wana uhakika kuwa TFF
itaongeza muda.
Kiongozi hasajili, akiulizwa
kwanini? Utasikia muda bado upo, tunafanya mambo yetu polepole.
Ukiangalia muda unaosema upo, unagundua unakaribia kwenye siku ya mwisho
(Deadline). Ni rahisi kujua kuwa kuna baadhi ya watu wanakuwa wanajua kabisa
kwamba TFF wataongeza muda.
Huku ni kuwazoesha watu kutofuata
kanuni na sheria. Kwanini watu wazembee kwa madai ya kuongezewa muda.
Wenzetu hawana taratibu za hivyo. Siku
ya mwisho ya usajili, makocha wanahaha kama hawajakamilisha. Unakumbuka usajili
wa Mesut Ozil kujiunga na Asernal kitokea Real Madrid?. Aserne Wenger alijua
kabisa inakula kwake, muda umekwisha na hajafanya mambo.
Unadhani Wenger aliwahi kuwaza kuwa
muda wa usajili utaongezwa?, lakini kwa Bongo ndio kwanza watu wanalala na
kuendelea na maisha mengine, huku `Deadline` ikikaribia.
Ifike wakati TFF ibaki katika misingi
ya kanuni ili kuondoa usemi wa `Hii ni Afrika` yaani `This is Africa`.
Tusipende kujipa mazoea nje ya kanuni.
Kila siku tunajadili kuendeleza soka,
tunaangalia upande mmoja wa tu yaani mpira wa uwanjani, hata suala la
kuzingatia kanuni na sheria ni sehemu ya mchezo.
Leo hii huwezi ukawa unaongeza muda
bila sababu ya msingi, mara ratiba inawekewa viraka, mara inasogezwa mbele
zaidi bila kuwa na sababu ya msingi.
Kwa mfano mwaka huu ratiba imesogezwa
kutoka Agosti 24 mpaka septemba 20 mwaka huu. Sababu kubwa ni kuipisha Yanga
itakayoenda kushiriki kombe la Kagame nchini Rwanda kuanzia Agosti 8 mwaka huu.
Kama Yanga watafika fainali, maana yake
watamaliza mashindano hayo Agosti 24 ambayo ndio siku ya fainali kwa mujibu wa
ratiba iliyotolewa na CECAFA siku ya jana.
Lakini kama Yanga watatolewa hatua ya
makundi, maana yake watarudi nchini kati ya Agosti 17 au 18 kwasababu mechi ya
mwisho ya makundi itakuwa Agosti 16 dhidi ya Coffee ya Ethipopia.
Kama watapambana na kufika fainali,
maana yake Kagame ingemalizika siku ambayo ligi inaanza kwa mujibu wa kalenda
ya awali ya TFF.
Lakini kwasababau hiyo ya kombe la
Kagame, TFF wakasogeza ligi mpaka septemba 20. Ukiangalia hapa, ni siku 26
zaidi baada ya kagame kumalizika. Hivi sababu ni Kagame au ndo mpaka haya mambo
ya usajili?
Wakati taarifa ya kusogeza mbele ligi
kuu inatolewa na TFF, ilielezwa kuna sababu mbalimbali za kufikia maamuzi hayo,
lakini kubwa ni kuisubiri Yanga.
Sababu mbalimbali hazikuweka wazi kwa
kumbukumbu zangu, lakini sasa nimegundua kuwa ni pamoja na klabu kutokamilisha
usajili.
Hii ni tabia isiyofaa kuendelea. Rais
wa TFF, Bwana Jamal Emil Malinzi, umeaminiwa na Watanzania wengi, japokuwa
kumekuwepo na dosari za hapa na pale kiutendaji, futa mazoea ya kutoka kwenye
kanuni.
Sioni sababu ya kuongeza muda wa usajili,
lazima tufuate kanuni. Najua ligi yetu ni fupi sana na ndio maana inapigwa
pigwa kalenda, lakini kuna njia nyingine ya kufanya ikiwa ni pamoja na
kurudisha mashindano kama Taifa Cup na mengineyo.
Nadhani kuna watu wa klabu wapo TFF,
kwahiyo wanafanya maamuzi kwa maslahi binafsi na kuja hadharani kama TFF.
Watu hawa wanakuja na suala la kuongeza
muda eti klabu hazijakamilisha taratibu. Mbona kuna timu zimemaliza kusajili?
Mazoea yana taabu. Ukishazoea kufanya
kitu kinyume na taratibu, utaona kanuni na sheria ni adau yako.
Ramadhani Karim!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TFF HII TABIA YA KUONGEZA MUDA WA USAJILI NA KUPIGA KALENDA LIGI KUU ITAISHA LINI?.”
Post a Comment