Thursday, August 21, 2014
FUNDI GEREJI ACHOMA MOTO WATOTO WAKE WAWILI,KISA KUCHELEWA KURUDI NYUMBANI WAKIANGALIA TV KWA JIRANI
Do you like this story?
Watoto wanaodaiwa kufanyiwa ukatili wakionyesha vidonda kwenye mikono yao ambavyo vinatokana na kuchomwa moto na baba ya mzazi nyumbani kwao Mbagala Kibondemaji jijini Dar es Salaam jana. |
Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyofanywa na baadhi
ya wazazi, vimezidi kukithiri nchini baada ya watoto wawili kudaiwa kuchomwa
moto mikono na baba yao kwa kutumia tambi za jiko jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo, anayetuhumiwa kufanya unyama huo ni
Salum Juma, fundi gereji wilayani Temeke, mkazi wa Mbagala Kibonde Maji, jijini
Dar es Salaam.
Watoto hao mmoja mwenye umri miaka saba na mwingine miaka
mitano (majina yao yamehifadhiwa), akiwamo wa kumzaa na wa kufikia walikutwa na
mkasa huo baada ya kwenda kuangalia runinga kwa jirani na kurudi nyumbani saa
5:00 usiku Alhamisi wiki iliyopita.
Jirani yao, Omar Fusi, alidai watoto hao walieleza kuwa
walichomwa na baba yao na kufichwa ndani, lakini baadaye majirani waliwaona
watoto hao wakiwa na majeraha.
Fusi alisema baada ya kuwaona wakiwa na majeraha, waliwahoji
ambapo walieleza kuwa walichomwa na baba yao baada ya kuchelewa kurudi kutoka
kuangalia televisheni.
Kwa mujibu wa Fusi, kitendo hicho kilifanyika huku mama yao
akiwa kwenye biashara zake za kukaanga mihogo.
Fusi alisema baada ya kubaini tukio hilo alitoa taarifa kwa
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibonde Maji ‘B’, Teofile Balae, ambaye
alitoa taarifa kwa Ofisa Ustawi wa Jamii kata ya Mbagala, Eliameresa Kaaya na
kuripoti polisi na kufanikisha baba huyo kukamatwa na kupelekwa katika Kituo
cha Polisi Maturubai ambako anaendelea kushikiliwa.
Balae alisema baada ya kushirikiana na Ofisa Ustawi wa Jamii
na baba huyo kukamatwa, waliwachukua watoto hao na kuwapeleka Kituo cha Polisi
Mbagala Kuu kwa ajili ya kupata fomu ya PF3 na kuwapeleka katika hospitali ya
Mbagala Rangi Tatu kupatiwa matibabu.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Erasto Kibara, alisema
walibaini watoto hao kufanyiwa ukatili huo baada ya kumkuta mmoja wao adukani
alikotumwa akiwa na majeraha na kumuuliza kilichompata kisha alitoa taarifa
hizo kwa mwenyekiti wa mtaa huo.
Ofisa Ustawi wa Jamii, Kaaya, katika Kituo cha Polisi
Maturubai , alisema kitendo walichofanyiwa watoto hao ni cha kikatili na
kuwataka wananchi kutoa taarifa pale wanapogundua ukatili katika mitaa yao ili
kutokomeza vitendo hivyo vilivyoshika kasi nchini.
Mwandishi wa habari hizi aliwashuhudia watoto hao katika
Kituo cha Polisi Maturubai huku wakiwa na majeraha mkononi wakati wakichukuliwa
maelezo na maofisa wa polisi wa kituo hicho.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, Dk.
Julius Nyakazilibe, alithibitisha watoto hao kupokelewa hospitalini hapo na
kupatiwa huduma ya matibabu kutokana na majeraha yaliyosababishwa na moto.
“Ni kweli watoto hao tuliwapokea hapa hospitalini wakiwa na
Ofisa Ustawi wa Jamii na walipatiwa matibabu,” alisema Dk. Nyakazilibe.
Mama mzazi wa watoto hao, Christina Menasi, akiwa katika
kituo cha polisi na mtoto wake mchanga huku akimnywesha uji, alisema wakati wa
tukio hilo, alikuwa katika biashara yake ya kuchoma mihogo na aliporudi
nyumbani na kukuta hali hiyo, aliingiwa na hofu ya kuripoti tukio hilo kwa
kumhofia mumewe.
Mama huyo alilaani kitendo hicho cha kikatili lakini alisema
akifungwa yeye ndiye atakuwa na mzigo mkubwa wa kulea familia hiyo.
“Inatakiwa tuache vitendo hivi vya kikatili, lakini ikiwa
mume wangu atafungwa, mimi ndiye nitakayebeba mzigo wa kulea hii familia,”
alisema Christina.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya Kihenya,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa
katika Kituo cha Polisi Maturubai na kwamba upelelezi unaendelea kabla ya
kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ FUNDI GEREJI ACHOMA MOTO WATOTO WAKE WAWILI,KISA KUCHELEWA KURUDI NYUMBANI WAKIANGALIA TV KWA JIRANI”
Post a Comment