Tuesday, August 12, 2014
TAHADHARI EBOLA YATUA AFRIKA MASHARIKI
Do you like this story?
BAADA
ya ugonjwa wa Ebola kuripotiwa katika nchi za Afrika Magharibi sasa umebisha
hodi katika nchi za Afrika Mashariki.
Kwa
mara ya kwanza mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa huo hatari amegundulika Rwanda
na tayari amewekwa kwenye sehemu maalumu kwa uchunguzi wa madaktari kubaini
kama ana virusi vya ugonjwa huo.
Wakati
ugonjwa huo ukiingia Rwanda, nchini Tanzania hali katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam inaonyesha hakuna udhibiti wa aina
yoyote kama ilivyoahidiwa na Serikali.
Mgonjwa
aliyegundulika Rwanda ambaye ni raia wa Ujerumani aliingia nchini humo akitokea
Liberia ambako ugonjwa huo sasa umekwishakuua mamia ya watu.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi usiku na Waziri wa Afya wa Rwanda, Agnes
Binagwaho, mgonjwa huyo ni mwanafunzi wa udaktari.
Alisema
mwanafunzi huyo alibainika kuwa na dalili za virusi vya ugonjwa huo, hali
iliyowalazimu madaktari kumkimbiza katika Hospitali ya King Faisoil na
kulazimika kuchukuliwa vipimo.
Mbali
na hatua hiyo, pia madaktari wanaotoa huduma kwa mgonjwa huyo wamewekwa katika
eneo maalumu kwa ajili kufanyiwa uchunguzi.
“Mbali
na madaktari wanaotoa huduma kuwekwa katika eneo maalumu, hata watu ambao
walikuwa wanamsogelea nao wanafanyiwa uchunguzi wakiwa katika chumba maalumu,”
alisema Waziri Binagwaho.
Hata
hivyo, Ubalozi wa Ujerumani nchini Rwanda umesema kwa sasa hauwezi kuzungumzia
suala hilo hadi uchunguzi utakapokamilika.
Akizungumza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif
Rashid, alisema Serikali inafikiria kuviwekea viwanja vya ndege mashine maalumu
zinazojulikana kama ‘Thermos Canners’, ambazo zina uwezo wa kutambua joto kwa
waathirika wa Ebola.
Lakini
alisema kukosekana kwa kifaa hicho, haimaanishi kwamba kutaathiri udhibiti
uliowekwa na serikali.
“Tumekuwa
tukiuchukulia ugonjwa huu kwa uzito wa hali ya juu tangu ulipobainika kuingia
katika nchi za Afrika Magharibi, kwa sababu wizara imekuwa ikiushughulikia kama
vile uko Uganda, Rwanda, Burundi au Kenya,” alisema.
Dk.
Seif alisema hivi sasa uwezo wa kusimamia mipaka umeongezwa kwa kutengeneza
vyumba maalumu kwa ajili ya wagonjwa wanaohisiwa kuwa na maradhi hayo, ikiwamo
kuwapatia wahudumu wa afya sare maalumu za kujikinga wakati wa kuwahudumia
waathirika.
Alizitaja
njia nyingine kuwa ni kuwachunguza wasafiri wote wanaohitaji kuingia nchini
siku 21 kabla ya kuanza safari, kubaini sehemu walizotoka kama zina maambukizi
ya Ebola.
Njia
nyingine zinazotumiwa kudhibiti ugonjwa huo ni kushirikiana na wizara nyingine
kama Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara
ya Uchukuzi na Wizara ya Fedha, ambazo kwa pamoja zitaweka mikakati madhubuti
ya kupambana kuhakikisha ugonjwa huo haupati upenyo kuingia nchini.
Uongozi
wa Uwanja Ndege
Kutokana
na hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo, MTANZANIA ilifika kwenye Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na kushuhudia kwamba hakuna chumba
chochote kilichotengwa kwa ajili ya uchunguzi, hasa kwa abiria wanaotoka Afrika
Magharibi.
Mkurugenzi
wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Moses Malaki, alisema Mamlaka ya
Viwanja wa Ndege Tanzania (TAA) inashirikiana na wadau mbalimbali kudhibiti
ugonjwa huo.
Alisema
wadau hao wamekuwa wakikutana mara kwa mara kwa ajili ya kuangalia namna ya
kudhibiti ugonjwa huo pamoja na mafua ya ndege.
“Sisi
kazi yetu ni kusimamia usalama wa abiria wakati wa kupanda na kushuka ndege,
lakini masuala mengine yanasimamiwa na Wizara ya Afya,” alisema Malaki.
Ndege
zakwepa kutua Afrika Magharibi
Shirika
la Ndege la Emirates limetangaza kusimamisha kwa muda safari za ndege za kwenda
Guinea tangu Agosti 2 mwaka huu kwa sababu ya ugonjwa wa Ebola ambao umeua
zaidi ya watu 1,000 katika nchi za Afrika magharibi.
Katika
tovuti yake, Emirates limesema haliwezi kuwaweka hatarini abiria na wafanyakazi
wake.
Wiki
iliyopita Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Margaret Chan, alisema
virusi vya Ebola vinatapakaa haraka zaidi kushinda juhudi za kuvidhibiti.
Homa
ya Ebola ilianza Guinea na kutapakaa nchi jirani za Sierra Leone na Liberia.
Mashirika mawili ya ndege ya Afrika ya Arik Air la Nigeria na ASKY ya Togo
yamekwisha kutangaza kuvunja safari za kwenda nchi zilizoathirika.
Zambia
nayo imepiga marufuku kuingia nchini humo watu wote wanaotoka Afrika Magharibi
kama njia ya kudhibiti Ebola.
Waziri
wa Afya wa Zambia, Joseph Katema, alisema raia wote wa nchi hiyo na wageni
waliomo nchini humo wenye lengo la kusafiri kwenda nchi zilizoathiriwa na
Ebola, safari zote zimesimamishwa hadi itakapotangazwa tena.
“Watu
wote kutoka sehemu yoyote ya nchi walioathirika na virusi vya Ebola wanazuiwa
kuingia Zambia hadi itakapotangazwa tena,” alisema Waziri Katema.
Virusi
vya ugonjwa huo vilianza kugunduliwa mwaka 1976 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (Zaire) na kuua mamia ya wananchi.
Madhara
yake yalizua hofu kwa familia ambayo ingepata mgonjwa wa Ebola kutokana na
kuelewa moja kwa moja kuwa uwezekano wa mgonjwa kupona ni asilimia 10 tu.
Tangu
wakati huo, wanasayansi wamekuwa wakitafuta njia za kutibu maambukizi ya
ugonjwa huo au kuuzuia usitokee.
Ingawa
yamekuwapo mafanikio ya kuutibu, lakini uhakika ulitolewa Mei 28 mwaka huu
wakati Jarida la Lancet la Uingereza lilipoeleza matokeo ya watafiti juu ya
kupatikana dawa ya kutibu Ebola kwa asilimia 100.
SOURCE.MTANZANIA
NEWS PAPER
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TAHADHARI EBOLA YATUA AFRIKA MASHARIKI”
Post a Comment