Tuesday, August 12, 2014
MAGUFULI: NIPO TAYARI KUSHTAKIWA.
Do you like this story?
WAZIRI wa Ujenzi,
Dk. John Magufuli, amesema yupo tayari kufungwa jela kuliko kuendelea
kuwavumilia watu wanaokwamisha ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kukimbilia
mahakamani.
Sambamba na hilo,
pia amepiga marufuku uchimbaji wa mchanga pembezoni mwa mto uliokuwa eneo la
daraja la Lugalo, ikiwa ni pamoja na kuwapa tahadhari ya kuwafungia
wafanyabiashara walio karibu na eneo hilo endapo watashindwa kuwa walinzi wa
uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Hayo aliyasemwa
jijini Dar es Salaam jana, katika ziara yake ya kutembelea maendeleo ya ujenzi
wa miradi ya miundombinu ya barabara pamoja na madaraja unaoendelea katika
maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Amesema Serikali
imekuwa ikisikitishwa na vitendo vya uharibu wa miundombinu hiyo vinavyofanywa
na baadhi ya watu, licha ya serikali kutumia gharama kubwa katika ujenzi wa
miundombinu hiyo.
“Watanzania
wanapaswa kujifunza na kuacha ubinafsi katika shughuli za maendeleo ili
kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa katika kiwango kinachostahili, kwa kuwa
mstari wa mbele katika utunzaji wa miundombinu ya barabara.
“Kwa
kiasi kikubwa uharibifu wa miundombinu umechangia kuwepo kwa ucheleweshaji wa
kukamilika kwa baadhi ya miundombinu, kwani hadi sasa milingoti saba ya taa za
barabarani pamoja na mifuniko ya maji taka 12 imeshaibiwa,” amesema Dk. Magufuli.
Kutokana na hali
hiyo, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, kuhakikisha
anasimamia na kudhibiti vitendo hivyo kwa kuwachukulia sheria wahusika.
Amesema Serikali
hadi sasa imeshatumia Sh trilioni moja katika kukamilisha ujenzi wa miradi
saba, ambayo ni pamoja na mradi wa barabara za Mwenge-Tegeta uliogharimu Sh
bilioni 89, Morocco Sh bil 288, barabara ya chini Tazara Sh bilioni 1.2 pamoja
na fly over Sh bilioni 100.
Miradi mingine ni
pamoja na ujenzi wa daraja la Kigamboni lililogharimu Sh bilioni 214, ambapo
ujenzi wa madaraja mawili ya Lugalo pamoja na Mlalakuwa lenye uwezo wa kubeba
tani 180, yamekamilika na yameanza kutumika.
Alisema pia jumla ya
Sh bilioni mbili zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa taa zitakazotumika katika
barabara hizo, ambapo fedha zote zimetokana na ufadhili wa serikali ya Japan.
Akizungumza katika
ziara hiyo, Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada, amesema serikali yake
itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa shughuli za
kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na ukamilishaji wa miundombinu hiyo.
.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MAGUFULI: NIPO TAYARI KUSHTAKIWA.”
Post a Comment