Tuesday, August 12, 2014

KAMATI YA WASSIRA YABARIKI ADHABU YA KIFO.




LICHA ya sheria ya kunyonga kupigiwa kelele na jumuiya za kimataifa, wajumbe wa kamati namba sita ya Bunge Maalumu la Katiba wamependekeza iendelee kutumika nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Steven Wassira, alisema hali hiyo ilijitokeza wakati wa kujadili Sura ya nne ya Rasimu ya Katiba.

“Wapo baadhi ya wajumbe walitaka adhabu ya kifo ifutwe, lakini wengi walipendekeza  adhabu hiyo iendelee, ingawa katika miaka ya hivi karibuni adhabu hiyo imekuwa ngumu kutekelezeka,” amesema.

Kwa upande wa suala la uraia wa nchi mbili, alisema wameliacha kiporo kutokana na kuwepo kwa mvutano miongoni mwa wajumbe.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo iliiacha kiporo sura hiyo na kuendelea kujadili sura nyingine.

“Kamati yetu hadi sasa imejadili sura ya pili, ya tatu na ya nne, Sura ya tano tuliiacha kiporo, hasa katika suala la uraia pacha,” amesema.

Alisema suala hilo halikufikia mwisho kutokana na kuwa na mjadala mkubwa kutokana na wajumbe kugawanyika na kwamba hata hivyo, suala hilo litapigiwa kura ili kupatiwa majibu.
“Maeneo mengi katika kamati yetu tumekubaliana, lakini yapo maeneo machache ambayo tunatofautiana,” alisema Wassira.
Alisema pamoja na kujadili sura hizo, kamati yake bado haijapiga kura kupitisha ibara za sura hizo ambayo kwa mujibu wa sheria inahitajika theluthi mbili ya wajumbe wote wakati wa kupitisha maamuzi.
Wassira alisisitiza kwamba Bunge la Katiba litaendelea na vikao vyake kama kawaida vya kutunga Katiba.

“Bunge hili haliwezi kuvunjwa kwa sababu watu wachache hawapo, kama ambavyo mnaona tunaendelea na vikao vyetu kama kawaida,” alisema

0 Responses to “KAMATI YA WASSIRA YABARIKI ADHABU YA KIFO.”

Post a Comment

More to Read