Sunday, August 10, 2014
WANAWAKE WOTE DUNIANI TUNALILIA AMANI – MAMA PINDA
Do you like this story?
MKE WA WAZIRI MKUU, Mama Tunu Pinda amesema wanawake wote
duniani wanalilia amani na hawapendi vita wala machafuko kwani husababisha
amani kutoweka kwenye familia na vifo vya watu wasio na hatia.
Ametoa wito huo leo mchana (Jumapili, Agosti 10, 2014)
wakati akitoa mada kama mzungumzaji mkuu (keynote speaker) kwenye Mkutano wa
Dunia wa siku tano ulioanza leo jijini Seoul, Korea Kusini.
Mkutano huo ambao umeandaliwa na taasisi ya Universal
Peace Federation (UPF) ambayo inatoa ushauri kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia masuala ya Uchumi na Kijamii unajadili masuala ya Amani,
Usalama na Maendeleo.
Akiwasilisha mada yake kuhusu usalama, amani na maendeleo
barani Afrika, Mama Tunu Pinda alisema: “Ninaiomba jamii ya Kimataifa duniani
kote tusimamie amani na usalama kwani kinyume na hapo ni kuleta machafuko na
vita. Wanawake hatupendi vita wala machafuko…,” alisema huku akishangiliwa.
Aliwataka washiriki wa mkutano huo wasimame katika nafasi
zao kama baba na mama, kama kaka na dada na kuhakikisha kuwa dunia inakuwa ni
mahali pazuri pa kuishi. “Ninawasihi tuendeleze maono ya Muumba wetu, tuweke
utu mbele kwa kuwajali wengine na tuache kutanguliza maslahi yetu binafsi,”
alisema.
Mapema, akiwakaribisha wajumbe zaidi ya 500 kutoka nchi 68
wanaoshiriki mkutano huo, Rais wa UPF, Dk. Thomas Walsh alisema taasisi hiyo
inasimamia misingi ya amani, usalama na maendeleo ya jamii kwa nia ya kujenga
umoja na mshikamano miongoni mwa mataifa mbalimbali.
Alisema anatumaini uwepo wa wakuu wa nchi mbalimbali na
viongozi mashuhuri, utasaidia kupata majibu ya changamoto inayoikabili dunia
juu ya upatikanaji wa amani ya kudumu.
Naye, Mfalme Letsie Mswati III kutoka Lesotho, akizungumza
katika mkutano huo alisema dunia inakabiliwa na changamoto nyingi za ukosefu wa
amani kubwa ikiwa ni uharibifu wa mazingira. Aliwataka wajumbe wa mkutano huo
kuhakikisha wanahimiza utunzaji wa mazingira kama njia ya kupunguza matatizo
yanayojikeza kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Alionya kwamba kuna haja ya kuweka mifumo madhubuti ya
kuhakikisha kuwa dunia haiendelei kuwa na matukio ya kigaidi na matumizi ya
silaha za maangamizi. “Kama tutakubali vita viendelee kutokea, na migogoro
isiyokwisha barani Afrika na nchi za Uarabuni, ni lazima tukubali kuwa
hakutakuwa na maendeleo katika mabara haya,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, AGOSTI 10, 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WANAWAKE WOTE DUNIANI TUNALILIA AMANI – MAMA PINDA”
Post a Comment