Friday, August 22, 2014
WIZARA YAFUTA AJIRA 200 ZA UHAMIAJI.
Do you like this story?
Wizara ya Mambo ya Ndani imefuta
ajira 200 za konstebo na koplo katika Idara ya Uhamiaji baada ya kubaini kuwa
kulikuwa na upendeleo katika usaili na sasa zitatangazwa upya na kusimamiwa na
wizara hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana,
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil alisema hatua hiyo imechukuliwa
baada ya kamati maalumu ya kuchunguza ajira hizo kubaini wazi kwamba waliopewa
nafasi hizo hawakukidhi vigezo.
Abdulwakil alisema wizara
imesikitishwa na udhaifu huo baada ya kubainika wazi kwamba malalamiko
yaliyotolewa na wananchi na kusababisha wizara kuingilia kati na kufuta usaili
wa kuitwa kwenye ajira kwa watu 200 ulikuwa sahihi.
Alisema baada ya kubainika kwamba
kweli kulikuwa na upendeleo wa dhahiri kwani watahiniwa wenye sifa na waliopata
alama za juu wakati wa usaili hawakuitwa na kukiukwa kwa vigezo vya wazi, ajira
hizo zitatangazwa upya na kusimamiwa moja kwa moja na wizara na siyo idara hiyo
kama ilivyokuwa awali.
“Kamati hiyo iliyoanza kazi yake
Agosti Mosi, mwaka huu ilibaini kwamba hata kigezo cha umri, ambacho ni miaka
25 kwa konstebo na miaka 30 kwa koplo hakikuzingatiwa kwani wenye umri zaidi ya
huo waliitwa kazini... “Lakini zaidi, baadhi ya wasailiwa walioitwa kazini ni
ndugu na jamaa wa watumishi wa Idara ya Uhamiaji,” alisema.
Alieleza kwamba utaratibu mpya wa
kuwapata watu wanaostahili utatangazwa kupitia vyombo vya habari na mamlaka ya
usimamizi imerejeshwa kwenye wizara husika badala ya kuachiwa kwenye idara
husika.
Alisema pamoja na kwamba miongoni
mwa udhaifu uliobainika ni kwamba matangazo ya kazi yaliyotolewa kwenye vyombo
vya habari hayakuainisha viwango na madaraja ya ufaulu kwa waliomaliza kidato
cha nne na cha sita, lakini hata wale waliofanya vizuri katika usaili
hawakuitwa kazini na hakuna sababu maalumu zilizotolewa.
Alisema ajira hizo zilizofutwa
zinahusisha pia nafasi 28 zilizokuwa zimetangazwa kupitia Idara ya Uhamiaji
Zanzibar.
Alisema si kosa kwa ndugu na jamaa
wa watumishi wa Idara ya Uhamiaji kuajiriwa katika nafasi hizo iwapo wanakidhi
vigezo vyote, lakini inapotokea kwamba hakuna msimamizi huru ni wazi kwamba
kunakuwa na upendeleo kama ilivyotokea na idara hiyo haichukui watumishi kutoka
Sekretarieti ya Ajira, kwa kuwa wanaohitajika ni askari.
Ajira hizo zilitangazwa Februari 17,
mwaka huu na watu 15,707 walijitokeza kuwania nafasi hizo 200, miongoni mwao,
waombaji 1,005 waliitwa kwenye usaili na 200 waliothibitishwa waliitwa kazini.
Hata hivyo, baada ya tangazo la
kuitwa kazini malalamiko yaliibuka kupitia vyombo vya habari na baadhi ya
mitandao ya kijamii, kwamba baadhi ya walioitwa katika ajira hizo walikuwa ni
watoto, jamaa na ndugu wa maofisa wa Idara ya Uhamiaji.
Baada ya kuibuka kwa malalamiko
hayo, wizara iliingilia kati na kuunda kamati hiyo ya watu watano Julai 31,
ambayo ilipewa siku 10 kukamilisha kazi yake na kutoa matokeo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WIZARA YAFUTA AJIRA 200 ZA UHAMIAJI.”
Post a Comment