Saturday, October 11, 2014

WATAKAOFAULU KIDATO CHA KWANZA 2015 MKOANI NJOMBE WAKIWA HAWAJUI KUSOMA NA KUANDIKA KURUDISHWA NYUMBANI




CHANGAMOTO kubwa inayoikabili sekta ya elimu nchini ya ukosefu wa ubora wa elimu, imelifanya Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kuingia kwenye orodha ya Wilaya zinazotarajiwa kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu nchini, baada ya kupitisha azimio la kutaka maafisa elimu msingi na sekondari wilayani humo kufanya usaili wa wanafunzi watakaofaulu kujiunga na elimu ya kidato cha kwanza 2015 unafanyika ili kubaini kama wanajua kusoma na kuandika au la.

Miongoni mwa maazimio yaliyoafikiwa na madiwani hao  ni pamoja na madiwani kuamua kuwabana wazazi ambao watashindwa kupeleka watoto wao shule na kujua idadi ya wanafunzi watakaofaulu mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka huu ili waweze kuhoji ufaulu wao ulitokana na nini kama hawajui kusoma na kuandika.

Imeelezwa kuwa, wakati wa maafikiano hayo baadhi ya madiwani walikataa kuafiki mkakati huo kwa lengo la kuwalinda wakuu wa shule za msingi walioruhusu watoto kufanya mtihani na endapo watafaulu wakati wakijua hawajui kusoma wala kuandika.

Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, wameeleza kuwa ni lazima maafisa elimu wote sekondari wahakikishe wanapata miongozo kutoka Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Ufundi ya jinsi ya kusimamia zoezi hilo kwasababu ndiyo kazi yao.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Sarah Dumba, diwani wa kata ya Ludewa, Monica Mchilo, ameeleza kuwa siku maadhimio hayo yalipoafikiwa haitasahaulika mashani mwake kwa yaliyotokea kutokana na baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo kutaka kuwakumbatia wakuu wa shule za msingi watakaobainika kuwa walifanya udanganyifu wa namna ya kuwafaulisha wanafunzi huku wakijua kuwa hawana sifa stahiki.

Alisema chanzo cha maamuzi hayo ni baada ya kutathimini hali ya taaluma katika Wilaya hiyo kuwa hairidhishi, na baada ya kukatazwa kuwa wasizungumzie suala hilo baadhi ya wajumbe wa baraza walijitenga.

Hata hivyo baada ya kufikishwa taarifa hiyo kwa bodi ya wazazi, baadhi yao walipokea kwa furaha suala hilo, huku wengi wao wakitaka umri wa wanafunzi kuanza shule uzingatiwe kwani wengi wa wanafunzi wanaoanza shule za msingi wilayani humo wanachelewa kuanza shule na kuwafanya kuwa na uelewa mdogo darasani na kushindwa kusoma kabisa.

Baadhi ya wajumbe wa bodi ya wazazi wameeleza kuwa mkakati wa madiwani hao hauna tatizo na kwamba tatizo la wanafunzi kushindwa kusoma na kuandika linatokana na uongozi dhaifu kuanzia ngazi ya familia hadi Wilaya ambapo walidai kuwa ukabila umeshamiri kwa walimu kujiona kuwa kabila ama ukoo fulani haustahili kupata elimu iliyo bora.

Kwa upande wa Ofisi ya Elimu Msingi wilayani humo, imesema kutokana na dhamira ya Baraza la Madiwani hao ni lazima kila mwanafunzi atakayefaulu kujiunga na elimu ya kidato cha kwanza atafanyiwa usaili huo. Pamoja na mambo mengine, imeelezwa kwamba usaili huo utasimamiwa na walimu wakuu wa shule husika na kwamba mwanafunzi atakayebainika kutojua kusoma au kuandika, atarejeshwa nyumbani.

via fikrapevu

0 Responses to “WATAKAOFAULU KIDATO CHA KWANZA 2015 MKOANI NJOMBE WAKIWA HAWAJUI KUSOMA NA KUANDIKA KURUDISHWA NYUMBANI ”

Post a Comment

More to Read