Saturday, October 11, 2014

MAOFISA POLISI 120 WATIMULIWA CCP





Moshi. Maofisa wa Polisi wapatao 120 wa Jeshi la Polisi, waliokuwa wakihudhuria mafunzo ya kupandishwa vyeo katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA), wametimuliwa chuoni hapo.


Vyanzo mbalimbali vililidokeza  kuwa, waliotimuliwa chuoni hapo ni maofisa ambao wana ulemavu wa aina mbalimbali walioupata wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya kazi.

Habari hizo zilisema hadi jana saa 9:00 alasiri, maofisa hao walikuwa ofisi za mkuu wa chuo hicho wakisubiri kupatiwa maelekezo ya namna ya kurejea katika vituo vyao vya kazi mikoa mbalimbali.

“Wako 120 hivi walikuja hapa (MPA) kwa ajili ya kuchukua kozi za Koplo, Sajenti, Meja na ‘Assistant Inspector’ (wakaguzi wasaidizi), lakini ndiyo hivyo wametuambia tuondoke,” kilidokeza chanzo chetu.

Hata hivyo, ofisa mmoja alilidokeza  kwamba mkuu wa zamani Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, ambaye amestaafu, ndiye wa kulaumiwa kwa kutoheshimu mapendekezo ya wataalamu.

“Tulimwambia IGP Mwema kwamba ni vizuri kama maofisa wenye ulemavu kama baadhi ya vigezo wanavyo basi wapewe vyeo huko huko mikoani, lakini wasiende chuoni,” alidokeza na kuongeza;

“Tulipendekeza yafunguliwe madarasa ya kanda wakishafanya mtihani wa kawaida wapewe vyeo huko huko, lakini wakija chuoni ni lazima wahudhurie vipindi vyote ambavyo vinafanya chuo kiitwe chuo.

“Chuo chochote kile kina vigezo vyake na kwamba ili mtu apate cheo alichokwenda kukisomea ni lazima ahudhurie asimilia 95 ya vipindi ikiwamo kwata, medani za kivita na kuzuia vurugu,”amesema.

Chanzo kingine kililidokeza  kuwa maofisa hao waliripoti chuoni hapo wiki mbili zilizopita na katika uchunguzi, walibainika wana ulemavu ambao hawawezi kumudu mafunzo ya ukakamavu.

Mmoja wa maofisa hao waliotimuliwa alilalamika kuwa kitendo hicho siyo cha kiungwana kwa kuwa ulemavu huo waliupata wakiwa kazini wakilitumikia Taifa na hawajashindwa kuingia darasani.

“Baadhi yetu tumefanya kazi miaka 20 wengine 25. Wamekatika miguu. Wako trafiki wamegongwa na polisi wengine wamepigwa risasi na majambazi wakapata ulemavu si sawa kutunyima vyeo,” alidai. (MWANANCHI)

0 Responses to “ MAOFISA POLISI 120 WATIMULIWA CCP”

Post a Comment

More to Read