Friday, January 30, 2015
PAC YAISHAURI SERIKALI NAMNA YA KUINUSURU KAMPUNI YA TTCL.
Do you like this story?
![]() |
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto (kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo Filikunjombe wakiwa katika majukumu yao. |
![]() |
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Dk. Kamugisha Kazaura (kushoto) akiwa katika majukumu. |
KAMATI ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa mapendekezo ya kuinusuru Kampuni ya
Simu Tanzania (TTCL) kutokana na hali mbaya ya kampuni hiyo kifedha kwa sasa
ambapo inaendeshwa kwa hasara huku ikiwa na madeni makubwa. PAC imetoa
mapendekezo hayo katika taarifa yao kwa bunge ya mwaka juu ya ukaguzi wa hesabu
za Serikali kwa mashirika ya umma iliyotolewa Januari 28 mwaka 2015.
Kwa mujibu wa
taarifa ya PAC hali ya mapato na matumizi ya TTCL kwa mwaka 2012 ilipata hasara
ya bilioni 20.883 huku kwa mwaka 2013 ikipata hasara ya bilioni 16.258. PAC
ilisema majumuisho ya hasara ya TTCL kupata hasara kwa takribani kwa miaka 10,
Kampuni sasa imekuwa na hasara ambayo kwa mwaka 2013 ilifikia bilioni 334.48, jambo
ambalo limeiondolea mvuto wa kukopeshwa na taasisi za fedha hata zile zenye nia
ya kuikopesha.
"...Ukosefu
wa fedha za kutosha kutekeleza miradi ya Kampuni umekuwa kikwazo kwa TTCL
kukabiliana na ushindani wa kibiashara. Kwa kipindi kirefu ufanisi wa TTCL
kiuwekezaji na kifedha umeendelea kudorora. Tangu TTCL ibinafsishwe mwaka 2001,
hakuna uwekezaji mkubwa uliofanyika na mpango wa kutafuta mkopo kutoka mabenki
ya ndani na nje ya nchi unakwamishwa na masharti ya kupata udhamini wa
Serikali," ilieleza taarifa hiyo ya PAC.
PAC iliongeza
kuwa ukiacha madeni yaliopo pia TTCL inadaiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa
Mawasiliano Tanzania (TCRA) jumla ya bilioni 25 hivyo kufanya jumla ya deni
kufikia bilioni 101.6. Kamati hiyo ya bunge imesema kuna umuhimu wa Serikali
kufanya maamuzi ya haraka ya kuikwamua TTCL ili iweze kuendelea kutoa huduma
kwenye Sekta ya Mawasiliano ikizingatiwa kuwa ndiyo inayoendesha Mkongo wa
Taifa wa mawasiliano.
Katika
mapendekezo ya PAC ili kuikwamua TTCL imeishauri Serikali kununua hisa asilimia
35 zinazomilikiwa na Bharti Airtel katika TTCL kwa gharama ndogo kwani Bharti
Airtel haikutimiza kikamilifu masharti ya mkataba wa mauziano ya hisa hizo hapo
awali kwani tangu inunue hisa hizo haijafanya uwekezaji katika Kampuni ya TTCL.
"...TTCL
isamehewe deni la Serikali Sh. 76.6 bilioni na deni la TCRA Sh. 25 bilioni
ambayo jumla yake ni Sh. 101.6 bilioni na fedha hizo zipelekwe kuongeza mtaji
ili Kampuni itoke kwenye kuwa na mtaji hasi wa Sh. 87.896 bilioni na kuwa na
mtaji chanya wa sh. 13.704 bilioni. Likifanyika hili basi Kampuni hiyo itaweza
kukopesheka. Serikali ikamilishe taratibu zake za kuimilikisha TTCL Mkongo wa
Taifa ili izidi kuuendeleza kwa ufanisi na kuongeza mapato ya TTCL,"
ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo
PAC imeshauri kuwa kuna umuhimu wa kufanya marekebisho ya muundo wa Kampuni ya
TTCL kwani kwa sasa ina idadi kubwa ya wafanyakazi (1549) isiyoweza kuwalipa.
Aidha, ilibainisha kuwa kwa sasa zinahitajika bilioni 32 kwa ajili ya
kugharamia urekebishaji wa muundo wa Kampuni ili uendane na mahitaji ya utoaji
wa huduma mbalimbali.
Mashirika
mengine yenye hali mbaya kifedha na uendeshaji ni pamoja na Shirika la Ndege
Tanzania, ATCL ambayo kwa sasa ina madeni makubwa huku ikiwa na ndege moja aina
ya Dash 8–Q 300, Wafanyakazi 142 na Jengo la ATC House lililoko mtaa wa Ohio,
Dar es Salaam.
*Imeandaliwa
na www.thehabari.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “PAC YAISHAURI SERIKALI NAMNA YA KUINUSURU KAMPUNI YA TTCL.”
Post a Comment