Tuesday, January 20, 2015
TANESCO WAPEWA SIKU 7 WAUNGANISHE UMEME.
Do you like this story?
WAZIRI wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameitaka Bodi mpya ya Shirika la Umeme Nchini
(TANESCO) kuliongoza shirika hilo kwa ufanisi na kuhakikisha kuwa mteja mpya
anapoomba umeme anafungiwa ndani ya wiki moja.
Pia waziri huyo
ameitaka bodi hiyo kuhakikisha kuwa shirika hilo linajitegemea na hivyo
kupunguza utegemezi wa fedha kutoka serikalini.
Akizindua bodi hiyo
mwishoni mwa wiki, Profesa Muhongo alielezea kukerwa na suala la wananchi
kufungiwa umeme ndani ya siku 30 mara wanapopeleka maombi hayo Tanesco na hivyo
kuiagiza bodi hiyo kulishughulikia suala hilo ili siku hizo zipungue.
“Bodi simamieni
maombi ya kufungiwa umeme ambayo sasa yanaelezwa kushughulikiwa ndani ya siku
30, hii lazima ibadilike, Watanzania lazima wapewe umeme ndani ya wiki, zaidi
ya hapo haikubaliki. “EWURA (Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji) waelezwe
kuhusu suala hili ili kuona namna ya kupunguza hizi siku, sababu wao wanahusika
katika suala la upangaji wa siku husika,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Akizungumzia haja ya
Tanesco kujitegemea kifedha, alisema kwa kipindi kirefu, serikali imekuwa
inatoa fedha nyingi kuisaidia kutekeleza miradi katika maeneo ya uzalishaji,
usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Hivyo alitaka bodi
hiyo kuonesha jinsi itakavyolibadilisha Shirika ili misaada kutoka serikalini
ipungue na ifike mahala shirika hilo lijitegemee.
Kuhusu madeni ambayo
Tanesco inadai kutoka kwa Taasisi za Umma, binafsi na watu binafsi, Waziri
Muhongo aliiagiza Bodi hiyo kulisimamia suala hilo na kuja na mkakati
utakaoliwezesha shirika hilo kukusanya madeni hayo.
Alisema lengo la
Serikali ni kuona shirika hilo linakusanya madeni kutoka kwa wadeni wake
wakubwa na wadogo ili Shirika hilo nalo liweze kulipa madeni linalodaiwa na
wadau wake.
Aidha, Profesa
Muhongo ameiagiza bodi hiyo mpya kuhakikisha kuwa shirika hilo linashirikiana
na sekta binafsi katika miradi yake ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji
umeme ili kufanikisha lengo la serikali la kuzalisha umeme wa kiasi cha
megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
Alieleza kuwa,
kulingana na sera zilizopo, uendelezaji wa sekta ya umeme, unahitaji
ushirikishwaji wa sekta binafsi kwa kuwa uwekezaji katika sekta hiyo unahitaji
kiasi kikubwa cha fedha za kigeni, kiwango ambacho kinahitaji ushirikiano na
sekta hizo.
Alisema Tanesco
inapaswa kuonesha nia thabiti ya kuunga mkono juhudi za serikali za kukamilisha
majadiliano na wawekezaji na waendelezaji wa miradi bila kuwakatisha tamaa.
Awali, Naibu Waziri
wa Nishati na Madini, Stephen Masele aliieleza bodi hiyo kwamba serikali ina
imani kuwa uzoefu na weledi wa Mwenyekiti na wajumbe wa bodi hiyo utasaidia
katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya nishati ili sekta hiyo muhimu
ichangie katika kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kati.
Naibu waziri huyo
aliwaasa wajumbe hao kuhakikisha kuwa taaluma walizonazo wanazitumia katika
kuliboresha shirika hilo. Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dk Mighanda Manyahi
alisema majukumu waliyokabidhiwa ya kuisimamia Tanesco ni makubwa, lakini kwa
kutumia taaluma zao watahakikisha wanayatimiza ili kuhakikisha nchi inakuwa na
umeme wa uhakika kwa kuwa nchi ina rasilimali za kutosha zinazowezesha kutimiza
malengo hayo.
Mwenyekiti huyo wa
Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco anaongoza wajumbe nane ambao ni Kissa Vivian
Kilindu, Juma Mkobya, Dk Haji Semboja, Shaaban Kayungilo, Dk Mutesigwa Maingu,
Boniface Muhegi, Felix Kibodya na Dk Nyamajeje Weggoro.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TANESCO WAPEWA SIKU 7 WAUNGANISHE UMEME.”
Post a Comment