Thursday, March 12, 2015
MAJANGA: NYOKA KUFIKISHWA MAHAKAMANI KAMA USHAHIDI.
Do you like this story?
NYOKA aliyepatikana katika nyumba ya
mshukiwa wa ulaghai jijini Nairobi, atatolewa kortini kama ushahidi kama
mahakama ilivyoagiza.
Upande wa mashtaka ulisema kuwa uko
tayari kuwasilisha nyoka huyo kesi dhidi ya raia wa Congo, Mangili Kayeba
itakaposikilizwa Machi 24 mwaka huu.
Mahakama iliambiwa kuwa mnyama huyo
anazuiliwa katika hifadhi ya wanyama ya Nairobi na ametaka mayai tangu apelekwe
huko mwaka jana.
Hakimu Mwandamizi wa Kibera Bw Tito
Gesora, aliagiza upande wa mashtaka kufikisha nyoka huyo kortini ili
kudhibitisha kesi dhidi ya Kayeba
Polisi walidai walimpata nyoka huyo
katika chumba kimoja walipokuwa wakifanya uchunguzi katika nyumba ya Kayebe
iliyoko eneo la Kilimani jijini Nairobi.
Inashukiwa kuwa mshtakiwa alikuwa akimtumia
nyoka huyo kufanya vituko vya ushirikina kwa kuwapumbaza watu aliolenga
kuwalaghai.
Polisi walienda katika nyumba yake
kufanya msako baada ya kumkamata akiwa na pesa bandia. Walimshtaki kwa
kupatikana akifuga mnyama kinyume cha sheria za kulinda wanyamapori
nchini mashtaka ambayo Kayeba alikanusha.
Kulingana na sheria, ni makosa
kwa mtu kupatikana akifunga mnyama wa porini bila kuwa na kibali kutoka
kwa shirika la kutunza wanyama pori nchini.
Aidha, Bw Kayebe alishtakiwa kwa
kupatikana na pesa bandia akiwa na nia ya kufanya uhalifu. Kesi yake
imepangiwa kuanza Machi 24 mwaka huu.
Bw Gesora alisema ni lazima upande wa
mashtaka uwasilishe mahakamani ushahidi ulio nao dhidi ya mshtakiwa ikiwa na
pamoja na nyoka huyo.
Wakati huo huo, mwanamume aliyepatikana
akitumia cheti cha mtihani wa kidato cha nne na kitambulisho cha mtu
mwingine akiomba kazi, alijipata pabaya aliposhtakiwa kwa wizi.
Upande wa mashtaka ulisema kwamba James
Butali, aliiba vyeti hivyo kutoka kwa Bw Joseph Kaptut ambaye nyumba yake
ilivunjwa mnamo Machi 9 mwaka huu mtaani Kawangware, Nairobi.
Kuvunja nyumba
Butali alishtakiwa kwa kushirikiana na
watu wengine ambao hakuwa kortini kuvunja nyumba ya Bw Kaptut eneo la
Kawangware ambapo ilidaiwa aliiba vyeti hivyo na nguo ikiwemo jezi
iliyokuwa na maandishi na nebo ya timu ya soka ya Chelsea.
“Ulipatikana na jezi iliyokuwa na nebo
ya timu ya soka ya Chelsea ukijua kwamba ilikuwa mali ya wizi au ukiwa umeiba,”
shtaka lilisema.
Kulingana na mashtaka,
aliwasilisha cheti na kitambulisho cha Bw Kaptut kwa kampuni moja kuomba
kazi na ndipo ikagunduliwa havikuwa vyake.
Hata hivyo, alikanusha mashtaka akisema
kwamba yeye ni shabiki damu wa Chelsea na haikuwa mara yake ya kwanza kuvaa
jezi hilo.
Hakimu Mkuu wa Kibera Bi Judith
Wanjala, aliagiza upande wa mashtaka kumkabidhi mshtakiwa nakala zote za
ushahidi kabla ya Juni 12 kesi itakaposikilizwa.
Alimwachilia kwa dhamana ya Sh50,000 na
mdhamini wa kiasi hicho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MAJANGA: NYOKA KUFIKISHWA MAHAKAMANI KAMA USHAHIDI.”
Post a Comment