Wednesday, March 11, 2015
RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA MKUU WA MKOA WA IRINGA.
Do you like this story?
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: ikulucommpress@googlemail.com
Website : www.ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425 |
PRESIDENT’S OFFICE,
STATE
HOUSE,
1 BARACK OBAMA ROAD,
11400
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Amina Masenza
kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea tarehe 11 Machi, 2015 Mafinga katika
Mkoa wa Iringa katika eneo lijulikanalo kwa jina la Changarawe, ambayo imepoteza
uhai wa watu zaidi ya 40 waliokuwa wakisafiri kwa basi hilo na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Ajali hiyo
imetokea baada ya basi la Kampuni ya Majinja Express walilokuwa wakisafiria
watu hao kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam
kugongana na lori lililokuwa likitokea Dar es Salaam
kwenda Mbeya, hivyo kusababisha kontena lililokuwa limebebwa na lori hilo kuliangukia basi.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa
sana kufuatia taarifa za vifo vya watu zaidi ya 40 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa
katika ajali hii mbaya ambayo imesababisha simanzi na majonzi makubwa kwa
familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu”, amesema Rais Kikwete akiomboleza msiba
huu.
“Huu ni msiba
mkubwa, na Taifa kwa ujumla limepata pigo kubwa, hivyo naomba
upokee salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kutokana na ajali
hii iliyotokea Mkoani kwako. Naomba, kupitia kwako, rambirambi zangu na pole nyingi ziwafikie watu wote waliopotelewa
ghafla na wapendwa wao. Namuomba
Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Roho za Marehemu wote
mahala pema peponi, Amina”, ameongeza kusema Rais Kikwete.
Katika Salamu
zake hizo, Rais Kikwete amewahakikishia wafiwa wote kuwa yuko pamoja nao katika
kuomboleza msiba wa ndugu na jamaa zao, lakini amesema, pamoja na machungu yote
ya kupotelewa na ndugu na jamaa zao, anawaomba wafiwa wawe na moyo wa uvumilivu
na subira wakati huu wanapoomboleza vifo vya wapendwa wao.
Aidha, Rais
Kikwete amehitimisha rambirambi zake kwa
kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema watu wote waliojeruhiwa
kwenye ajali hiyo wapone haraka, ili waweze kuungana tena na ndugu na jamaa
zao.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
– Dar es Salaam.
11 Machi, 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA MKUU WA MKOA WA IRINGA.”
Post a Comment